MTIKISIKO umeikumba Wizara ya Ujenzi, baada ya baadhi ya vigogo wa Wakala wa Ufundi na Umeme (Temesa), kuandika waraka mzito kwa Waziri wa ujenzi na naibu wake, ukiwataka kuingilia kati matitizo ya menejimenti inayokabili wakala huyo.
Temesa, anayehusika na usimamizi wa matengenezo wa magari ya serikali, ikiwamo baadhi ya Ikulu, imeingia kwenye mgogoro wa chichini wa menejimenti, Dk John Magufuli kushauriwa kumuondoa aliyekuwa Ofisa Mtendaji Mkuu, Manase Lekujani.
Hata hivyo, mgogoro huo sasa unaonekana kufikia hatua ya juu baada ya baadhi ya wakurugenzi kuandika waraka huo, ambao gazeti hili unao ukionyesha kupinga uteuzi wa Mathaline Magesa, kuwa Kaimu ofisa mtendaji mkuu wa wakala huyo.
"Tunaandika waraka huu, kueleza msimamo wetu kupinga uteuzi wa mama Mathelina Magesa kuwa Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu.
Tatizo letu kubwa, uteuzi huo haukuzingatia vigezo vya madaraja ya utumishi wa umma," inasema sehemu ya waraka huo ambao nakala inakwenda Ikulu kwa Katibu Mkuu Kiongozi na kusisitiza:
"Uteuzi haukuzingatia kwamba aliyeteuliwa hakuwahi kuongoza hata kitengo, zaidi ya kuwa mhandisi wa kawaida. Hivyo, kwa utaratibu waliopaswa kuteuliwa ni watu waliofikia ngazi ya ukurugenzi.
Hivyo, basi tunaamini waziri wetu, Dk Magufuli na Naibu Dk (Harrison) Mwakyembe ni wasikivu, mtakaa na kusikia msimamo wetu na kutengua uamuzi huo ambao umetokana na ushauri kwa Ofisi ya Kaimu Katibu Mkuu, vinginevyo mambo hayakwenda."
Katika kuonyesha msisitizo waraka huo wenye kurasa 15 unaongeza: "Kwakuwa tunajua waziri na naibu mmeshauriwa..., basi kingine tunachosisitiza ni kwamba Kaimu Katibu Mkuu, Balozi Hurbet Mrango, akimaliza muda wake na kustaafu Agosti mwaka huu, basi tusingependa kuona tena akiongezewa mkataba, kwani ndiye aliyeshauri uteuzi huo kwenye mazingira tata."
Vigogo hao katika waraka huo, waliweka bayana kwamba kwa utaratibu aliyepaswa kukaimu ni mtu mwenye ngazi ya ukurugenzi, kwani atakuwa na uzoefu wa kuingia kwenye vikao vya menejimenti sio mhandisi wa kawaida asiyekuwa na kitengo.
Dk Magufuli alipopigiwa simu jana kuhusu waraka huo, ilikuwa ikiita bila kupokelewa, huku Dk Mwakyembe akaihidi kuzungumza na mwandishi akipata nafasi.
Lakini, tangazo ambalo limetolewa na wizara hiyo mapema mwezi huu, limetaka watu mbalimbali wenye sifa kuomba nafasi hiyo ya Ofisa mtendaji mkuu (CEO) wa Temesa ambayo sasa ikaimiwa na Magesa.
0 comments