BARAZA la Usalama la Taifa lililoketi chini ya Rais Jakaya Kikwete kujadili kuhusu milipuko ya mabomu iliyotokea siku mbili zilizopita katika ghala la kuhifadhia silaha la Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), kambi ya Gongo la Mboto jijini Dar es Salaam, limeshindwa kubaini chanzo cha tukio hilo.
Baraza la Usalama la Taifa ndicho chombo cha juu cha kumshauri Rais kuhusu masuala yahusuyo usalama wa taifa.
Hivyo katika mkutano huo ulioitishwa na Rais mara baada ya kutokea kwa maafa hayo, baraza limeagiza jeshi lifanye uchunguzi wake wa ndani kubaini chanzo cha tukio hilo kama Sheria ya Ulinzi wa Taifa inavyoagiza.
Kadhalika imevitaka vyombo vya ulinzi na usalama visaidie katika uchunguzi huo.
Kwa mujibu wa taarifa ya Ikulu iliyotolewa kwenye vyombo vya habari kuhusu maazimio ya mkutano wa baraza hilo, serikali ya Tanzania iziombe nchi rafiki zisaidie katika uchunguzi wa chanzo cha tukio hilo na kushauri namna bora zaidi ya kuimarisha usalama na uhifadhi wa mabomu na risasi katika maghala ya jeshi kote nchini.
Wakati baraza likishindwa kubaini chanzo cha milipuko hiyo ya mabomu iliyosababisha vifo vya watu zaidi ya 20, chanzo cha habari toka jeshini, kililidokeza gazeti hili kuwa mabomu yaliyolipuka toka katika kambi hiyo yalikuwa yameunganishwa wakati kitaalamu mabomu yanapohifadhiwa yanatakiwa kutounganishwa.
“Hayo yaliyolipuka yalikuwa yameunganishwa, chuma cha mbele na kile chuma cha nyuma kinachojulikana kama poda charge, chuma hicho kina podapoda ukifunga ndio linakuwa bomu kamili…sasa jiulize kwa nini walikuwa wameyaunganisha?” kilieleza chanzo chetu hicho.
Mbali na hilo serikali itagharamia mazishi ya marehemu waliopoteza maisha katika tukio la mabomu la Gongo la Mboto kokote ambako ndugu watakakoamua wakazikwe; na ndugu wa marehemu pia watapewa kifuta machozi.
Kwa upande wa waliojeruhiwa, Baraza la Usalama limeamua kuwa serikali igharamie matibabu yao na baadaye watakapotoka hospitali walipwe kifuta machozi kwa ulemavu walioupata.
Hali kadhalika, limeagiza Kamati ya Maafa ya Mkoa wa Dar es Salaam na Kitengo cha Maafa cha Taifa wazitambue mapema iwezekanavyo nyumba zilizoharibiwa na wenye nyumba hizo; na kuhakikisha kuwa matayarisho husika yanafanyika ikiwa ni pamoja na uthamini ili walipwe fidia wanayostahili bila kuchelewa.
Aidha kamati ya Maafa ya Mkoa imeagizwa kushirikiana na Kitengo cha Maafa cha Taifa kilichoko Ofisi ya Waziri Mkuu kuwahudumia wananchi waliopoteza makazi yao au waliolazimika kuyakimbia makazi yao kwa nia ya kuokoa maisha yao.
Pia ihakikishwe kuwa kwa haraka wanapatiwa makazi ya muda pamoja na huduma za malazi, chakula, maji, afya na usafi wa mazingira.
Vile vile Kamati ya Maafa ya Mkoa imeelekezwa kutengeneza taratibu nzuri zitakazohakikisha kuwa mapema iwezekanavyo, wananchi hao wanarejea makwao ili waendelee na shughuli zao za kawaida hasa sasa ambapo hatari ya milipuko katika maghala ya Gongo la Mboto haipo tena.
“Kamati ya Maafa ya Mkoa kushirikiana na Jeshi la Polisi kuwatafuta watoto waliopotea na kuwaunganisha na familia zao. Pia kuongoza, kuratibu na kusimamia utekelezaji wa masuala yote yahusuyo waliofariki, waliojeruhiwa na waliohama makazi yao na huduma zao stahiki,” ilieleza taarifa hiyo.
Pia wamewaomba wananchi watoe ushirikiano wa hali ya juu kwa jeshi kwa kuwapa taarifa wanapoyaona mabomu katika maeneo yo yote.
“Na jambo kubwa zaidi tunawakumbusha wananchi kutii maelekezo ya jeshi ya kutokuyagusa au kuchezea mabomu au hata vipande vipande vya mabomu vilivyodondoka katika maeneo yao,” ilieleza taarifa hiyo.
Serikali pia imewataka wananchi waliohama kurejea kwenye makazi yao kwani kipindi cha hatari ya mabomu kulipuka kimekwishapita.
Aidha imewatahadharisha watu wajiepushe kuchezea mabomu yaliyodondoka katika maeneo yao ambayo bado hayajaondolewa.
Mabomu Magereza Ukonga
Wakati jiji hususan wakazi wa maeneo ya Gongo la Mboto wakiwa bado na hofu ya milipuko ya mabomu, taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa baadhi ya mabomu yalitua hadi katika gereza la Ukonga.
Hali hiyo ilisababisha hofu miongoni mwa wafungwa waliokuwa selo na kusababisha kuvunja milango ya selo hizo na kukusanyika uwanjani kujihami.
Hilo pia lilisababisha mfungwa mmoja kutoroka na askari magereza wapatao wawili kujeruhiwa.
Mkuu wa Jeshi la Magereza, Agustino Nanyaro, alipoulizwa kuhusu mabomu kutua katika ardhi ya gereza hilo alijibu: “Sasa Ukonga si ardhi kama zilivyo ardhi nyingine?”
Aidha wafungwa kuvunja selo na kukusanyika uwanjani alisema kwa kifupi kuwa hawakuvunja ila labda walifunguliwa milango. Kuhusu mfungwa kutoroka alisema kuwa hilo hajalisikia.
Majeruhi afariki Muhimbili
Mmoja wa majeruhi aliyefikishwa hospitalini hapa amefariki dunia jana na hivyo kufanya jumla ya watu waliofariki kufikia 21.
Akizungumza na gazeti hili, Afisa Uhusiano wa Muhimbili Aminieli Aligaesha alisema kuwa idadi ya majeruhi imeongezeka kutoka 80 hadi 106.
Alisema majeruhi watoto wako wawili na wamelazwa katika wodi ya Kibasila kwa ajili ya upasuaji mdogo wa mlipuko wa mabomu. Wakati wajawazito waliopatwa na mshituko ni wawili na wamelazwa Mwaisela.
Aidha waliopoteza viungo ambao wamelazwa katika hospitali ya Muhimbili ni wawili ambao ni Saida Rajab aliyekatika mkono na mtoto anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 12 ambaye ambaye pia amekatika mkono.
Wakati huo huo, Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Balozi Seif Ally Idd naye jana alitembelea hospitalini hapo jana kuwafariji majeruhi.
Hospitali ya Amana
HALI ya wahanga wa milipuko ya mabomu katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam, inaendelea vizuri huku wengi wao wakiendelea kutibiwa na kuruhusiwa kurudi nyumbani.
Hayo yalisemwa jana na Mganga Mkuu wa hospitali ya hiyo Dk. Meshack Shimwela, alipokuwa akitoa taarifa ya wagonjwa kwa viongozi na wageni mbalimbali waliotembelea hospitali hiyo ili kujua hali zao.
Alisema hadi kufikia jana alfajiri bado waliendelea kupokea wagonjwa katika hospitali hiyo na kufikia 218 huku wagonjwa 35 wakihamishiwa hospitali ya Taifa Muhimbili kutokana na hali zao kuwa mbaya sana.
“Toka ilipoanza kutokea milipuko hadi sasa tumepokea wagonjwa 218 na maiti 13, lakini mpaka sasa tumebaki na wagonjwa 50, kati yao wanne ni wanaume, watoto wadogo ni wawili na wanawake ni 44,” alisema Dk. Meshack.
Dk. Shein atembelea wahanga
Rais wa Zanzibar Dk. Alli Mohamed Shein, jana alikuwa ni miongoni wa viongozi wa serikali waliotembelea wagonjwa hao katika hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam.
Akizungumzia tukio hilo la mabomu alisema hakuna wa muda wa kulaumiana ila serikali imejipanga kuhakikisha milipuko hiyo haitokei tena nchini.
Profesa Lipumba atembelea Gongolamboto
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba, naye alikuwa ni miongoni mwa viongozi waliotembelea wahanga wa mabomu katika eneo la Gongo la Mboto na Hospitali ya Amana jana.
Alisema ili kuepuka na hali hiyo ni lazima serikali kupitia kwa Waziri mwenye dhamana ya ulinzi na jeshi la kujenga Taifa Dk. Hussein Mwinyi, kuandaa utaratibu wa kutoa elimu kwa wananchi hasa wanaoishi karibu na kambi za jeshi.
Dk. Mwinyi na Mwamunyange nao
Ilipotimu majira ya saa sita mchana Waziri wa Ulinzi na Jeshi la kujenga Taifa Dk. Hussen Mwinyi, alifika hospitalini hapo akiwa ameongozana na Mkuu wa majeshi nchini Davis Mwamunyange.
Dk. Mwinyi, alisema wao wamefika hospitalini hapo kwa ajili ya kuona wahanga hao wa mabomu waliolazwa katika hospitali hiyo kwa ajili ya kupatiwa matibabu na wala si kujibu maswali ya waandishi wa habari waliokuwepo katika hospitali hiyo.
“Sisi hatukuja kwa ajili ya kufanya Press, ila tumekuja kuona wagonjwa na kama ni hoja tayari taarifa ya baraza la usalama wa Taifa imeshatolewa na Rais, ila nendeni makao makuu ya jeshi watalaamu wanatoa taarifa ya milipuko sawa,” alisema Dk. Mwinyi.
Uwanja wa Taifa
Idadi ya watoto waliopotezana na ndugu zao wakati wa kujihami na milipuko hiyo ya mabomu imepungua na kufikia watoto 37 hadi jana jioni.
Akizungumza na wabunge wa jamhuri ya muungano wa Tanzania wanaowakilisha mkoa wa Dare s Salaam, wakati akipokea misaada iliyotolewa na marafiki wa wabunge hao Kaimu mkuu wa mkoa huo Sadiq Meck Sadiq, alisema idadi hiyo imetokana na wazazi wengi kujitokeza na kuwatambua watoto wao.
Alisema watoto hao ambao bado hawajatambuliwa na ndugu zao wamehamishiwa katika viwanja vya maonyesho vya Saba Saba, na kwamba kama hali hiyo ya kutokutambuliwa itaendelea mpaka kesho, serikali ya mkoa itawahamishia eneo la Gongo la Mboto ili iwe rahisi kwa ndugu zao kuwafuatilia.
Nao marafiki wa wabunge hao ambao ni Watanzania wenye asili ya Yemen kupitia kwa katibu mkuu wao Hashim Saggaf, walisema msaada walioutoa ni magodoro (200), shuka (200) mchele tani (3) mabero ya mitumba (60) pamoja na tende, vyote vikiwa na jumla ya shilingi milioni 36.
Wabunge wapeleka posho zao Gongo la Mboto
Spika wa Bunge, Anna Makinda, amesema posho za wabunge na watumishi wote wa mhimili huo walizotakiwa kupata jana zitapelekwa kwa ajili ya kuwasaidia waathirika wa mabomu ya Gongolamboto.
Alizungumza hayo muda mfupi baada ya kumalizika kwa dua ya kuliombea Bunge na dakika moja ya kuwa kimya kuwakumbuka walikufa kutokana na mabomu, Mnadhimu wa Kambi ya upinzani bungeni Tundu Lissu kuomba mwongozo wa spika kwa mujibu wa kanuni za bunge ili kutengua kanuni na kujadili suala la mabomu hayo kama hoja ya dharura.
Akijibu mwongozo huo spika Makinda alisema hakuna haja ya Bunge kujadili suala hilo kwa vile tayari serikali imeanza kuchukua hatua hivyo kikao cha bunge kiendelee na shughuli zake kama kawaida.
Makinda alisema hatua ya wabunge na watumishi wa Bunge kutoa posho zao ni agizo la Spika baada ya kushauriana na wajumbe wa kamati ya uongozi.
Kwa siku mbunge hulipwa kati ya sh 160,000 na sh 180,000 kwa ajili ya posho ya kikao ambayo ni sh 70,000 nyingine zinahusisha posho ya malazi, chakula na usafiri ambapo Bunge la sasa linahusisha wabunge 350 kutoka vyama mbalimbali, huku watumishi wa Bunge wakipata sh 50,000 posho ya siku.
0 comments