Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - CCM kufumuliwa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kinaonekana kugundua kilipojikwaa na sasa kimedhamiria kukabiliana na kizingiti hicho, ili kurejea kwenye mstari na kujihakikishia ushindi zaidi miaka ijayo.

Pamoja na kubaini kiini hicho, chama hicho tawala kimesema hakina budi kujipanga na kujifanyia mageuzi makubwa kama ambavyo nyoka hujibadilisha anapozeeka.

“Chama hiki kimekuwa madarakani kwa muda mrefu na hivyo kusababisha baadhi ya watu kukichoka na kutaka mabadiliko tu hata kama kimefanya mazuri,” alisema Mwenyekiti wa Chama hicho Rais Jakaya Kikwete jana.

Kikwete alikuwa akihutubia kilele cha maadhimisho ya miaka 34 ya CCM yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini hapa.

“Tutafanya kama nyoka, ambaye kila mara hujivua ngozi yake na kurudi kuwa mpya … nasi katika CCM tutafanya hivyo,” alisema Rais.

Alisema chama hicho katika mabadiliko makubwa kinachotarajia kuyafanya, kitahakikisha kinarejesha mvuto hususan kwa vijana na kuwataka wanachama wakiwamo viongozi, kukubaliana na hatua hiyo.

Alisema lazima chama kihuishwe ili kukiongeza mvuto mbele ya watu. Muundo utazamwe kama unakidhi haja, viongozi watendaji nao watazamwe kama wanakidhi haja na kama si mzigo unaokipaka matope chama hicho.

“Wale tunaoweza kuachana nao sasa tuachane nao kwa maslahi mapana ya chama chetu.

“Lengo letu kuu ni kutambua nguvu zetu na udhaifu wetu uko wapi na makosa gani tulifanya katika uchaguzi uliopita.

Lengo letu ni kuimarisha nguvu zetu na kurekebisha kasoro zetu na kusahihisha makosa yetu.

“Katika tathmini hiyo pia tuangalie nguvu za wapinzani wetu zilikuwa kwenye maeneo gani na udhaifu wao ulikuwa wapi na kisha tutumie udhaifu huo kwa manufaa yetu,” alisema.

Sambamba na hatua hiyo, aliagiza kufanyika kwa tathmini kuanzia ngazi ya chini hadi Taifa na kusema ni wazi kuwa katika mchakato wa uchaguzi mwaka jana kulikuwa na kununiana katika kura ya maoni.

“Hali ya kununiana ilijitokeza katika kura hizo, hivyo sasa ni muhimu kusameheana na kuwa wamoja ili kujenga chama imara kitakachohakikisha ushindi zaidi mwaka 2010 … tuanze maandalizi sasa,” alisema.

Kikwete alisema tathmini hizo zinatakiwa kufanywa kwa utulivu na kuepusha jazba kama zilizojitokeza katika mchakato wa uchaguzi mwaka jana.

Alisema makosa yaliyofanyika katika uchaguzi huo, yaliwanufaisha wapinzani hata kujiongezea viti vya ubunge na udiwani, kwani hata baadhi ya wana-CCM kwa hasira waliamua kuwapigia wapinzani na wengi hawakujitokeza kabisa.

“Katika maeneo mengi tuliyoshindwa au hata kufanya vibaya katika uchaguzi, mgawanyiko wakati wa kura za maoni ulichangia sana.

Baadhi ya wana-CCM waliacha kupiga kura au hata kudiriki kupigia kura wagombea wa upinzani kwa sababu ya hasira,” alisema.

Aliwasihi wana-CCM kuendelea kuhamasisha watu kujiunga na chama hicho na pia kujiandikisha kupiga kura “kwani wapiga kura ni waliojiandikisha na si vinginevyo,” alisema.

Aliwataka pia wanachama wa CCM kuachana na malumbano huku wakitakiwa kujua kwamba chama chao ni chama kikongwe ambacho kimeongoza nchi kwa miaka 34 na kuwaletea maendeleo wananchi.

Alisema pamoja na kuwapo changamoto ndani ya chama hicho, ni kawaida ya chama chochote duniani na hakuna kiongozi ambaye anaweza kumaliza changamoto zake katika uongozi. “

Jamani Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere aliongoza kwa zaidi ya miaka 20 hakumaliza changamoto zote akaja Mzee Ruksa hakumaliza na Mzee Mkapa naye hakumaliza, itakuwa mimi?

Lakini nataka nikuhakikishieni kuwa nitajitahidi kupunguza changamoto hizo zinazokikabili chama,” alisema Kikwete.

Aidha, alisema ili kuhakikisha nguvu za chama zinaimarika, chama hicho kitakuwa tayari
kuachana na wanachama ambao wanaonekana kuwa wasumbufu na hawakubaliani na uamuzi wa chama hicho tawala.

Alisema kwa sasa chama kina mikakati ya kujiimarisha ili kurejesha majimbo yote na kata zote ambazo zimechukuliwa na vyama vya upinzani.

Kikwete alisema pamoja na kelele nyingi za baadhi ya wanasiasa bado hawana uwezo wa kushika madaraka makubwa katika nchi, kwani viongozi wengi wanafanya kazi zao kwa jazba.

Alisema wapo baadhi ya wanachama wananuniana kutokana na makosa mbalimbali yaliyojitokeza katika vipindi hivyo.

Alisisitiza chama kujiimarisha kiuchumi akisema hali ya kifedha ya chama hicho si imara na kinategemea zaidi ruzuku inayotokana na ushindi kwa upande wa wabunge na madiwani.

Kwa ajili hiyo, vyanzo vya asili vya chama kupata fedha za kujiendesha vimesahaulika, kwani miaka yote ada na michango ya wanachama vilikuwa ndizo nguzo na vyanzo vikuu vya mapato ya chama.

“Hatuwezi kuacha jukumu la kugharimia uendeshaji wa chama chetu mikononi mwa wafadhili matajiri. Tunahatarisha uhuru wa chama chetu,” alionya na kuongeza:

“Bahati mbaya safari hii ruzuku hiyo imepungua kwa sababu ya nguvu ya vyama vya upinzani kuongezeka.

Uchaguzi ujao nguvu ya upinzani ikiongezeka zaidi tutakuwa na hali mbaya.”

Alisisitiza pia uundwaji wa Katiba mpya akisema ni jambo lisiloepukika na kuwataka wananchi kushiriki kikamilifu mchakato utakapoanza na kujiepusha na jazba.

”Niwaombe, kuwa wakati huo ukifika wana-CCM na wananchi kujitokeza kwa wingi katika kutoa maoni na katika kupiga kura ya maoni itakayoidhinisha Katiba hiyo.

Katiba ni mali ya wananchi, hivyo tunataka tuwashirikishe kwa ukamilifu katika hatua zote muhimu,” alisema.
Tags:

0 comments

Post a Comment