Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Spika akuna kichwa kuikabili Dowans

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Spika wa Bunge, Anne Makinda amesema ofisi yake itapokea hoja ya mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, inayoandaliwa kuwasilishwa bungeni mwezi Februari,  huku akihadharisha kuwa atahakikisha haipingani na kanuni za mhimili huo wa dola wa kutunga sheria.

Desemba 5 mwaka jana, Kafulila ambaye ni mbunge kupitia NCCR-Mageuzi, alitangaza kusudio la kuwasilisha hoja binafsi bungeni kutaka serikali itoe maelezo juu ya mgawo wa umeme na matokeo ya hukumu ya ICC kuhusu kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco.

Jana Spika wa Bunge Anne Makinda, aliliambia gazeti hili kuwa Bunge litapokea hoja ya Kafulila, lakini kwa tahadhari kuhakikisha haikinzani na kanuni za bunge.

 Kauli ya Makinda, inakuja kipindi ambacho sakata hilo linatarajiwa kuibua upya majeraha ya sakata la Richmond lililoitikisa nchi wakati wa mkutano wa 16 wa bunge la 10 li Februari 2008.

"Ruksa kuleta hoja yake, akileta ipo kamati ya ufundi itakaa na kuipitia kifungu kwa kifungu... na kama itakuwa inakiuka kanuni basi kuna uamuzi utatolewa kulinda maslahi ya wananchi," alifafanua Spika Makinda.

Makinda alisema alichofanya Kafulila hadi sasa  ni kuwasilisha taarifa ya kusudio na si hoja yenyewe.   Alifafanua kwamba, kutokana na bunge kupokea taarifa ya kusudio imetoa ruksa kwa mbunge huyo kuwasilisha hoja yake rasmi huku akisisitiza, itaangaliwa kwa umakini. 
"Yeye mheshimiwa Kafulila taarifa yake inaeleza kusudio la kuwasilisha hoja inayohusu mambo ya umeme na hilo jingine ulilolitaja la Dowans na uamuzi wa ICC... lakini itakapokuja ndipo tutaweza kuichambua kupitia kamati yetu hiyo ya ufundi," aliweka bayana.

Alipoulizwa haoni hoja hiyo inaweza kuibua majeraha ya Richmond na wengine wakaitumia kutaka kujisafisha na uamuzi wa bunge kuhusu mkataba wa kifisadi wa Richmond uliomfanya Edward Lowassa, kujiuzulu uwaziri mkuu, alisisitiza kwa kuhoji, "Sasa si hadi hoja ije tuisome au?"

Naye Naibu Spika Job Ndugai alipotakiwa kuzungumzia suala hilo alisema kuwa uamuzi wa hoja binafsi ya mbunge kujadiliwa au kutojadiliwa, upo mikononi mwa Spika wa Bunge. 
Ndugai alifafanua utaratibu huo kuwa hoja ya mbunge huwasilishwa kwa Katibu wa Bunge ambaye naye huiwasilisha kwa Kamati ya Uongozi ya Bunge. Kamati hiyo ndiyo inayomshauri Spika wa Bunge kuikubali au kuikataa hoja hiyo.

“Kamati hii ya uongozi ya Bunge inamshirikisha Spika wa Bunge, Naibu spika, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni na wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge.
Nashindwa kulielezea hili kwani hata kamati hizo hazijaundwa mpaka sasa," alisema Ndugai na kuongeza:  Desemba 10 mwaka jana, Kafulila alitekeleza azma yake hiyo kwa kuwasisha barua ya kusudio la kupeleka hoja hiyo bungeni na bunge lilimjibu Desemba 14 mwaka jana kuwa:

 “Ninapenda kukuarifu kuwa kusudio lako linafanyiwa kazi na iwapo itakidhi masharti ya katiba, kanuni na sheria kwa mujibu wa kanuni ya 55 (9) ya kanuni za Bunge utaombwa kuwasilisha maelezo ya hoja husika ili hoja hiyo iweze kuingizwa kwenye kitabu cha shughuli na orodha ya shughuli za bunge kulingana na maelezo ya Spika,” 
Barua hiyo yenye kichwa cha habari Kusudio la kuwasilisha hoja binafsi ya bunge kuitaka serikali kutoa maelezo juu ya mgao wa umeme na matokeo ya hukumu ya ICC kuhusu kesi ya Dowans dhidi ya Tanesco ambayo Mwananchi imefanikiwa kuiona, ilisainiwa na Eliakimu Mrema aliyekuwa anakaimu nafasi ya Katibu wa Bunge.

Kwa mujibu wa Kanuni hiyo ya Bunge, 55(9),"Spika hataruhusu hoja yoyote inayokiuka Katiba au Sheria au Kanuni za Bunge na Katibu atairudisha hoja hiyo pamoja na vielelezo vyake vyote kwa Mbunge mhusika na maelezo ya sababu za kukataliwa kwa hoja hiyo."  Lakini Kafulila wakati anatangaza kusudio la kuwasilisha hoja alionya kwamba endapo atawekewa mizengwe, atapeleka suala hilo kwa wananchi.

Kafulila alieleza msingi wa hoja yake hiyo kuwa ni serikali kufumbia macho miradi ya umeme ya uhakika, ambayo ingetoa majibu ya kudumu ya tatizo hilo la uhaba wa umeme nchini, badala yake imebaki kusimamia sekta ya nishati hiyo kwa kudunduliza ikitumia mitambo ya kukodi kwa miaka mingi. 
Kafulila alitaja mitambo inayotumika na serikali kuzalisha umeme usiokidhi mahitaji kuwa ni pamoja na mitambo ya kampuni ya IPTL ya tangu mwaka 1994, mitambo ya kampuni za Aggreko, Songas, Richmond na hata Dowans.  Kwa mujibu wa Kafulila, uzalishaji wa umeme kwa kutumia mitambo hiyo, ni kunyonya uchumi wa taifa.

Kafulila alisema asilimia 86 ya mapato ya Shirika la Umeme nchini (Tanesco), yamekuwa yakitumika kulipia umeme unaozalishwa na mitambo ya kukodi inayozalisha takriban asilimia 45 tu ya umeme wote.

Mbunge huyo alieleza kuwa mitambo ya kukodi inayotumika sasa ni ya Songas na IPTL pekee baada ya Aggreko kumaliza mkataba na Dowans kufutwa mkataba wake.  Alisema Tanesco wanailipa kampuni ya Songas takriban Sh 266milioni kila siku kwa kununua megawati 186 za umeme, wakati mitambo ya IPTL ikiwa imewashwa, wanailipa kampuni hiyo Sh300 milioni kwa siku.

“Itakumbukwa kuwa Tanesco walikuwa wanapaswa kuilipa kampuni ya Richmond/Dowans Sh152 milioni kila siku kwa kununua megawati 100 za umeme,” alisema Kafulila.

Alisema tangu mwaka 2006, serikali imeshindwa japo kupunguza tatizo la mgawo wa umeme na kwamba, viongozi wakuu wa serikali, hasa Waziri wa Nishati na Madini mara kadhaa, wamekuwa wakipotosha Watanzania kuwa serikali inashughulikia na kwamba, mgawo wa nishati hiyo utakuwa historia.

Alisema wakati sasa Watanzania wakiwa wanazungumzia mgawo wa umeme, bado wanakabiliwa na deni la Sh97 bilioni ambazo Mahakama ya Usuluhishi ya Kimataifa (ICC), inaitaka Tanzania iilipe Dowans. 
Alisema mkataba huo ulikuwa ni wa miezi 24 na wenye thamani ya Sh. bilioni 172, lakini kwa ukosefu wa uongozi na siasa duni ndani ya mfumo wa utawala, serikali inalipia fedha hiyo tena bila kupata umeme.  
Tags:

0 comments

Post a Comment