Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Slaa: JK atwambie kwanini tunailipa Dowans

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk Willibroad  Slaa amemtaka Rais Jakaya Kikwete kuwaeleza Watanzania sababu za kuwabebesha mzigo wa malipo ya fidia ya Sh185 bilioni kwa kampuni ya Dowans, hali serikali yake ikihusika na uzembe uliosababisha fidia hiyo.
Akizungumza na gazeti hili jana, Dk Slaa alisema, Dowans iliingia nchini kwa uzembe wa serikali hivyo Rais Kikwete anapaswa kueleza kwanza serikali yake inawajibikaje, kabla ya kuwataka Watanzania walipe fedha hiyo.

"Kampuni ya Dowans iliingia nchini kwa baraka za Baraza la Mawaziri wakati Kikwete akiwa mwenyekiti. Uzembe huu ulifanyika yeye akiwa anaona na kama hajui basi yeye hakuwajibika, na kama alijua basi yeye ni sehemu ya uzembe huo. Atuambie kwa nini tulipe Dowans kwa uzembe wa serikali yake?" alihoji.

Aliendelea, "Ukilitazama jambo hilo kwa undani, utagundua kuwa baada ya Lowassa kujiuzulu katika sakata la Richmond, mtu aliyetakiwa kumfuata ni Kikwete, kwani ndiye aliyebariki ujio wa kampuni hiyo nchini na baadaye Dowans."

Alisema "Kikwete anahusika na Dowans kwani mwaka 2007 ndiye aliyekutana na waandishi wa habari Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kueleza kuwa ameshawasiliana na kampuni moja kuja nchini kuzalisha umeme kwa bei nafuu. Na siku chache baadaye, mfanyabiashara mmoja maarufu nchini (jina linahifadhiwa) akaleta mitambo hiyo."

Dk Slaa alisema hayo baada ya gazeti hili kumtaka aeleze endapo ana uthibitisho wowote, anapomtuhumu Rais Kikwete kuhusika na Dowans.

Jana baadhi ya vyombo vya habari nchini, viliinukuu Kurugenzi ya Habari na Mawasiliano ya Rais Ikulu ikieleza kuwa kitendo cha Dk Slaa kumhusisha Rais Kikwete na Dowans ni uzushi na kinalenga kumpaka matope.

Lakini alipotakiwa kuzungumzia suala hilo jana, Dk Slaa alisema hawezi kujibizana na Kurugenzi hiyo inayofanya kazi chini ya rais kwa kuwa siyo saizi yake.

"Waliomjibia Kikwete siwezi kujibizana nao kwa kuwa sio saizi yangu. Nataka Kikwete mwenyewe ajitokeza ajibu kama mimi nimesema wongo," alisema Dk Slaa.

Ulipaji wa fidia hiyo unafuatia uamuzi uliotolewa na Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Migogoro ya Biashara (ICC Court), Novemba 15, mwaka huu chini ya Mwenyekiti Gerald Aksen na wasuluhishi Swithin Munyantwali, Jonathan Parker uliamuru Tanesco iilipe Dowans kiasi hicho cha fedha.

Dowans ilifungua shauri katika ICC, ikilalamikia Serikali ya Tanzania kupitia Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), kuvunja mkataba kabla ya wakati na kinyume cha makubalino kwenye mkataba husika.

Awali baada ya uamuzi huo kufikiwa, Tanesco ilionyesha nia kwamba ingechukua hatua za kukata rufaa, lakini kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema kwamba haoni sababu ya kufanya hivyo inaonekana kama imeyeyusha ndoto hizo za Tanesco.
Mkurugenzi Mkuu wa Tanesco, William Mhando aliwahi kuwaambia wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari kuwa shirika lake lingeweza kutoa tamko kuhusu hatua za kuchukua kuhusu uamuzi wa ICC, lakini akaweka wazi kuwa walikuwa wakisubiri uamuzi huo kusajiliwa rasmi katika Mahakama Kuu nchini.

Hata hivyo,  kutokana na kauli ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, sasa ni rasmi kwamba hakutakuwa na hatua zozote za kisheria dhidi ya uamuzi wa ICC na badala yake Tanesco watatakiwa kujipanga kuwalipa Dowans mabilioni hayo ya shilingi kama walivyoamriwa.

Akizungumza na Mwananchi baada ya hafla ya kuapishwa kwa Jaji Mkuu mpya, Mohamed Chande Othman Desemba 27, mwaka jana, Jaji Werema alisema ameshamaliza kuisoma hukumu hiyo na kufanya uamuzi ambao tayari ameukabidhi kwa Waziri wa Nishati na Madini William Ngeleja kwa ajili ya hatua nyingine baada ya kuridhika nayo.
 “Mimi kama Mwanasheria Mkuu wa Serikali nimeisoma hukumu hiyo kwa makini na nimeridhika nayo kuwa iko sawa,” alisema Jaji Werema.

Waziri Ngeleja juzi aliliambia Mwananchi kwamba serikali inaendelea kujipanga kutekeleza ushauri wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kuhusu Dowans.

Taarifa za ndani ya Tanesco, zinasema kwamba shirika hilo limeanza kuweka fedha kwa ajili ya  malipo katika benki moja (jina tunalihifadhi kwa sasa) jijini Dar es Salaam.

Comments Kwa hisani ya Mwananchi.com

0#14 Mahamed 2011-01-05 13:18
Ni ajabu kwamba Mheshimiwa Rais Jakaya Kikwete anasibishwe na ufisadi ambao haukumuhusu yeye binafsi, ila ilikua ni baraza la mawaziri. Pili, mbona Watanzania tumekua tukilipa mabilioni ya dola kwenye taasisi mbalimbali ikiwemo IMF na zingine kwa uzembe wa serikali zilizopita, na hakuna yeyote alie thubutu kum-bandika ufisadi rais walietangulia?
Quote
+1#13 Eddy 2011-01-05 13:10
Kama mkataba kati ya TANESCO na DOWANS uoneshavyo ni dhahiri kuwa unaelezea kuwa endapo mmoja akivunja masharti ya mkataba huo basi atatakiwa kulipia fidia,sasa je suala la kuwashirikisha wananchi kulipa BILIONI 185 linatokea wapi wakati wakisainiana mkataba sisis hatukuwepo,tuta lipaje ukizingatia maisha yenyewe ni kuokota makopo ya maji barabarani???????????????
Quote
+1#12 Mtafiti General 2011-01-05 12:57
tatizo kubwa mtanzania akishapata uhakiaka wa mlo wa siku na wa kesho yake basi anajifanya hili suala halimhusu. Hizi hela ni nyingi sana na hata kama zingekuwa chache kwa nini iwe hivi.
Quote
+1#11 MZAWA 2011-01-05 12:55
Ndugu watanzania tukubali kutokana na hali iliyopo na inayoendelea ni ngumu. Kukumbatia huu ukumbavu wa Dawans hautusaidii chochote. Rais kashindwa kututetea wananchi wake kaamua kukumbatia ufisadi. Na sisi tumuonyeshe ya kuwa kutokana na ukimya wake hatuwezi kuvumilia. Angekuwa mstari wa mbele kuwa na maamuzi ya kuchukua hatua haya mambo yasinge mkuta. Sasa aamke ashirikiane na wananchi aepukane na hawa mafisadi.


Awaambie hawa mafisadi kila mtu achukue msalaba wake. Rais aamue kuchukua msalaba wa watanzania. Ashirikiane na bunge kutekeleza majukumu yake. Haya mambo ya siri siri ndio hayo yanamchafua na kumuumbua. Dr Slaa anauchungu na Tz, ya leo na umasikini, na hali ya mtanzania ilivyo. Anajiuliza ni kwa nini Mtanzania hapigi hatua siku zote ni kudanganywa tu. Hotuba yake ya mwaka mpya hakuweza kulifafanua alipita juujuu tu. Ninawaomba ndugu zangu watanzania hili swala la Dawans si la chama cha CCM,CHADEMA, CUF WALA TLP. Tushirikiane wote tujie serikali yetu inafanya nini katika kumsaidia huyu mtanzania ili aweze kutoka kwenye ulimwengu wa giza na kuingia kwenye ulimwengu wa kisasa. Wanaomlaumu Dr SLAA hao ni watanzania wa IKULU ambao wanamshauri Rais upumbvu ili akae mbali na wananchi wake.
Quote
+2#10 lapa 2011-01-05 12:39
dr mimi huwa nakukubali sana nilijua tu hawa vilaza lazima watakurupuka kukujibu na wamekurupuka umewapa 7 za vichwa
Quote
0#9 Mchungu wa Bongo 2011-01-05 12:10
ICC kwa Ucampo kunawasubiri Mafisadi woote na huyu aliyetajwa na Dr Slaa hapa, ..."the day is coming..."
Quote
+1#8 Katikiro 2011-01-05 12:07
Eh!
Angekuwepo Nyerere angesema.
Hatulipi hiyo hela na mitambo tunachukua fanyeni mtakalo.


Kila kitu kilikuwa wazi, hakukuwa na sababu ya kesi hiyo kushindwa, lakini hata kulipa hiyo Hela Serikali imekubali kuilipa Dowans.


Hii nchi sasa imetuchoka tufanye mageuzi makubwa sana mmoja mmoja, na kwa pamoja.
Quote
+2#7 Mtanzania Mpenda hak 2011-01-05 12:01
 Kwa ushauri wangu JK ajiuzulu ameshindwa kuongoza nchi kwanza yeye ndio FISADI number moja au ashtakiwe na kufugwa jela maana huu sio uugwana ni uwizi wa macho macho. Wananchi wenye kipato cha chini wanateseka kwa ajili ya JK na kuuza sura yake. Hatuko kununua sura au meno awajibishwe mara moja.
Quote
+2#6 ROMLI 2011-01-05 11:56
ama kweli tumefanywa vipofu watanzania na woga wetu ndio unaotutafuna. hawa viongozi wetu ndio wanaoliangamiza taifa na kufurahia jasho la damu la watanzania. Mtandao utakaonufaika ni uleule alioutaja Waziri Pinda kuwa ukiguswa utatikisa nchi.Hata kwa mtu ambaye hajasoma sheria, dowans walirithije richmond?Ni nani aliyesainisha makubaliano haya?Nani alipitisha maamuzi ya kuwaruhusu dowans kufanya kazi Tanzania?Wahusika ndio walipishwe. tunaomba misaada hata ya kujengewa matundu ya vyoo huku tukitoa billions kwa watu wachache wasio na mchango wowote ktk nchi yetu zaidi ya kutupora,kutuny onya hatimaye wanaomba uraiya nchi walikohamishia mali zetu. MFANO MZURI WA UOZO WA SERIKALI YA KIKWETE NI KIFO CHA UTATA CHA DAUDI BALALI(FAKE DEATH).Inauma sana ndugu zanguni.
Quote
+2#5 emmanuel 2011-01-05 11:52
Tushamjua mwenye DOWANS jamani haina haja ya kuuliza sana kifuatacho ni ACTION tu.MAANDAMANO na MIGOMO kwa kwenda mbele.Hakuna malaika wa kutuokoa ni sisi wenyewe wenye nchi yetu....
Quote
+3#4 JohnQ 2011-01-05 09:32
Ni kweli kabisa, ni lazima rais kikwete utuambie sababu za kuilipa dowans na pia tufafanuliwe hiyo dowans ni ya kina nani? Angekuwepo JK wa kwanza, kuoza huku kwa serikali na watendaji wake kusinge kuwepo.
Quote
+5#3 Peter Laizer 2011-01-05 09:04
Huu ufisadi tunaufumbia macho hadi lini? Bilioni 185???????? Hainiingii akilini kabisaa!!! Kwanza hao Wakina-Dowans ni nani????? Wananchi wanateseka kwa huduma mbovu za miundombinu huku wachache wakijichotea mabilioni huku Raisi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali wakibariki jambo hilo! JK azungumze juu ya hilo asikae kimya. Wananchi tumekosa imani kwa haya yanayoendelea.
Quote
+3#2 frank shimbo 2011-01-05 08:33
kwanza ninani mmiliki wa dowans
pili iweje tulipe wakati hatujui ninani hasa mmiliki wa hiyo kitu
tatu,hao mawakala walitumwa na nini,
ni wizi tu huo wakutaka kurudisgha hera ssem hizo so NO KULIPA HILO DENI
Quote
+3#1 Goodlife 2011-01-05 08:11
Jamani hii sasa imefikia pabaya yaani mnatufanya Watanzania wooote ni mazuzu na hamuoni aibu kuendelea kutupiga danadana kuhusu umiliki wa hii kampuni ya Dowans..sioni ugumu ulipo vinginevyo kuna chembechembe za ufisadi hapa..hiyo hukumu ni siri??iwekeni wazi kupitia vyombo vya habari tuone nani anatushtaki na sio kusema ''mmeisoma na kuridhika nayo'' ilhali watanzania ndio wanabebeshwa mzigo wa kulipa, je hamuoni kama na wao wana haki ya kusoma na kuridhia kabla serikali haijaidhinisha malipo??
Quote
Tags:

0 comments

Post a Comment