IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI Mkuu Mizengo Pinda, amemaliza mgogoro uliokuwepo baina ya uongozi wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) na wahadhiri wa chuo hicho kuhusu maslahi yao na wamekubali kuingia madarasani kuanzia leo.
Akizungumza na Jumuiya ya Wanataaluma wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOMASA) jana mchana katika ukumbi wa Chimwaga, Waziri Mkuu alisema matatizo ya chuo hicho ni matokeo ya mlundikano wa mambo kwa siku nyingi na mengi ni ya kiutendaji na yanaweza kuisha bila kupoteza muda.
“Nimezungumza na viongozi wa Udomasa na kuwaahidi madai yao ya posho yanaweza kukamilika Februari, nilitaka yaishe mwezi huu lakini kwa taratibu za Hazina sasa hivi wameshaanza kushughulikia mishahara ya Januari kwa hiyo marekebisho hayawezi kuwahi…wameniahidi mwezi ujao yatakamilika,” alisema huku akishangiliwa.
Pinda pia amemwagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) aende kukagua taarifa za mahesabu ya chuo hicho, ili kubaini tuhuma zilizojitokeza za watu kulipwa hundi mbili za mishahara.
CAG atatakiwa kukagua tuhuma nyingine za walioacha kazi kuendelea kuwemo kwenye orodha ya wanaolipwa mshahara huku wengine waliopo kazini kukosekana kabisa kwenye orodha hiyo.
“CAG atakuwa hapa kesho… mpeni ushirikiano ili aifanye kazi kwa urahisi, nia yetu ni kuangalia mfumo mzima wa fedha na utawala ukoje ili ikibidi urekebishwe,” alisema.
Kuhusu madai ya wanafunzi ya tatizo la maji, Waziri Mkuu alisema amemwagiza Naibu Katibu Mkuu (Fedha) John Haule ambaye alikuwepo katika ukumbi wa Chimwaga, alishughulikie.
Katika agizo hilo, alimtaka Haule afuatilie uhamisho wa ndani wa fedha katika Wizara ya Maji ili zipatikane Sh bilioni 1.66 zinazohitajiwa na Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka Dodoma (DUWASA), kuchimba visima maeneo ya Ng’ong’ona na Ihumwa na kutandaza mabomba hadi chuoni ili kupunguza shida ya maji haraka iwezekanavyo.
Alisema hilo ni suluhisho la muda mfupi kwa kuwa katika mipango ya muda mrefu, Duwasa inatarajiwa kupata dola za Marekani milioni 26 zitakazotumika kuchimba visima vingine na kujenga matangi yenye uwezo wa kuhifadhi lita milioni 12 za maji na kuondoa kabisa tatizo la maji chuoni hapo.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Idris Kikula alimweleza Waziri Mkuu kwamba mahitaji halisi ya maji chuoni hapo ni lita milioni 3.5 kwa siku na kati ya hizo, lita milioni 1.5 ni kwa matumizi ya wanafunzi peke yao na lita nyingine milioni mbili ni kwa matumizi ya ujenzi unaoendelea chuoni hapo.
Awali akizungumza na Kamati ya Makatibu Wakuu iliyoundwa na Katibu Mkuu Kiongozi, mara baada ya kuwasili mjini Dodoma jana asubuhi, Waziri Mkuu alielewa matatizo ya malipo ya posho na mishahara kwa watumishi na wahadhiri wa chuo hicho.
Naye Makamu Mwenyekiti wa Udomasa, Idd Mwerange alimwahidi Waziri Mkuu kwamba watarudi madarasani wakati wakisubiri madai yao yakamilishwe lakini aliomba kuwe na uwakilishi wa jumuiya hiyo katika timu ya watu watakaonana na CAG.
Akifunga mkutano huo, Prof. Kikula alimwahidi Waziri Mkuu kufuatilia maagizo hayo na kwamba leo menejimenti, idara ya uhasibu na Udomasa watakutana kuunda timu ya pamoja itakayobainisha stahili za walimu wote ili orodha hiyo iwasilishwe kwa Waziri Mkuu mapema iwezekanavyo kwa ufuatiliaji.
Juzi Waziri Mkuu alifanya vikao viwili, kimoja na uongozi wa UDOM na kingine cha Serikali ya Wanafunzi ambavyo vilidumu hadi saa 12.30 jioni na kumlazimu kuahirisha vikao viwili vilivyobaki hadi leo.
Kwa mujibu wa ratiba ya chuo hicho, mara baada ya kukutana na Serikali ya Wanafunzi, Waziri Mkuu alipangiwa kukutana na wanachama wa Udomasa na kisha kufanya majumuisho katika ukumbi wa Chimwaga kwa kuzihusisha pande zote tatu.
Katika vikao vyote viwili, Waziri Mkuu alielezwa matatizo yanayokikabili chuo hicho, ikiwemo uhaba wa maji, uhaba wa walimu, vifaa vya masomo na mlundikano katika mabweni.
Kabla ya kufanya mikutano hiyo miwili, Waziri Mkuu alifanya ziara chuoni kukagua miundombinu ya maji safi, maji taka, vyumba vya kulala katika mabweni ya Chuo cha Sanaa na Sayansi za Jamii pamoja na mabweni ya Skuli ya Tiba na Uuguzi na ujenzi wa visima vya maji.
Wakati Waziri Mkuu akishughulikia mgogoro huo, Chama cha Wafanyakazi wa Taasisi za Elimu ya Juu, Sayansi, Teknolojia, Habari na Utafiti (RAAWU), jana kimetoa wiki mbili kwa Serikali na menejimenti za taasisi na mashirika yaliyo chini ya chama hicho, kulipa malimbikizo na mishahara yote ya wafanyakazi wa taasisi hizo.
Chama hicho kiliitisha mkutano na waandishi wa habari na kuonya kuwa baada ya muda huo kumalizika bila kuona hatua za kumaliza tatizo hilo, kitalazimika kuchua hatua za kisheria dhidi ya Serikali na menejimenti hizo.
Katibu Mkuu wa Raawu Taifa, Adelgunda Mgaya alisema wafanyakazi waliopo chini ya chama hicho wamekuwa wakidai malimbikizo yao na mishahara mipya kwa muda mrefu sasa bila mafanikio.
Alisema tangu Julai mwaka jana Serikali ilipopandisha mishahara ya wafanyakazi kwa viwango tofauti, miezi minne imeshapita wafanyakazi walio chini ya chama hicho hawajalipwa kiwango
hicho kipya pamoja na malimbikizo yao.
“Tayari baadhi ya wafanyakazi wameshaanza kuonesha kuchoka kuvumilia na kuanza kuandamana, na malalamiko yao yanatokana na ukweli kuwa ulipaji wa mishahara mipya haujaanza na tatizo kubwa lipo kwa taasisi za umma zilizo chini ya Msajili wa Hazina zikiwamo za elimu ya juu,” alisema Mgaya.
Alisema chama hicho katika kufuatilia ulipaji huo, kiliahidiwa kuwa ifikapo Novemba mwaka jana ulipaji wa mishahara hiyo mipya ungeanza.
“Tunakiri kuwa taasisi nyingi zililipwa
kulingana na ahadi lakini nyingine hadi sasa hazijalipwa,” alisema na kutoa mfano wahadhiri wa UDOM. Mgaya alisema pamoja na
ucheleweshwaji wa mishahara hiyo, pia wafanyakazi walio chini ya chama hicho wamekuwa wakilalamikia ucheleweshwaji wa malimbikizo ya mishahara yao.
Kutokana hali hiyo, Raawu imeitaka Serikali na menejimenti hizo zirekebishe hali hiyo haraka iwezekanavyo na kuhakikisha kuwa matatizo kama hayo hayajirudii tena katika miaka ijayo.
Alisema tatizo la mishahara na malikimbizo wakati mwingine linasababishwa na Serikali lakini pia na menejimenti zinahusika kutokana na uzembe na kuitaka Serikali kuchunguza
menejimenti hizo na zitakazobainika kuhusika, zichukuliwe hatua za kinidhamu.
Mgaya alisema suala hilo tayari limeshachukua muda mrefu kwa hiyo wanatoa wiki hizo mbili hadi mwishoni mwa mwezi huu, hatua ziwe zimeanza kuchukuliwa vinginevyo chama hicho
kitaishtaki Serikali pamoja na menejimenti kwa kuwa mshahara ni haki ya mfanyakazi kwa mujibu wa sheria na Katiba.
Chama hicho pia kimewataka wafanyakazi kutulia na kusubiri Serikali ichukue hatua na iwapo hali itakuwa tofauti, Raawu haitosita kuchukua hatua za haraka kuepusha kupanuka kwa migogoro. Naibu Katibu Mkuu wa Raawu, Herzon Kaaya alisema ni vyema Serikali iyashughulikie matatizo hayo kabla ya bajeti ya 2011/2012
You Are Here: Home - - Pinda amaliza mgomo UDOM
0 comments