Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Niliyozungumza kuhusu Katiba, ni maoni yangu binafsi-Werema

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Frederick Werema ametetea kauli yake ya hivi karibuni iliyotaka Katiba iliyopo ifanyiwe marekebisho badala ya kuandikwa upya na kusema, yalikuwa ni maoni yake binafsi.

Aidha, amejibu hoja iliyoanzishwa na baadhi ya wanasiasa na wadau mbalimbali wa Katiba inayomtaka ajiuzulu kwa kujifananisha na mwanafunzi aliyekuwa wa mwisho darasani ambapo alisema haambiwi aache shule.

Katika mazungumzo yake na gazeti hili kwa njia ya simu jana Werema alisema, “sikuzungumza kwa kificho na kila mtu alinisikia nikitoa maoni yangu, sielewi ni kwa nini jambo hili linakuzwa, sasa hao wanaotaka nijiuzulu nao wajiulize, ina maana mwanafunzi akiwa wa mwisho kwenye mtihani darasani watamwambia ajiuzulu kusoma?

“Nafikiri hilo litakupa majibu ya swali lako, kwa sasa nipo likizo, naomba niishie hapo,” alisema Werema na kusisitiza kuwa Watanzania hawapaswi kusema tu na kushabikia mambo bila kuyafanyia kazi.

Mjadala kuhusu kauli ya Werema na Waziri wa Katiba na Sheria Celina Kombani kuwa Katiba mpya haihitajiki kwa sasa, ulichukua sura tofauti baada ya Rais Jakaya Kikwete kubariki kuanza kwa mchakato wa kupata Katiba mpya.

Wachambuzi wa mambo ya siasa na wananchi wenye mitazamo tofauti wameibua maswali mengi ikiwamo yale yaliyohoji uwezo wa kisheria wa Werema na Kombani na kupendekeza Rais awafukuze kazi au wajiuzulu wenyewe, kwa sababu maelezo yao kuhusu Katiba yalipingana na ya tamko la Rais.

Rais Kikwete alitoa msimamo wake wa kuunga mkono Katiba mpya Desemba 31, mwaka jana wakati akilihutubia Taifa kwa njia ya televisheni, lakini pia aliwataka Watanzania kutoa maoni yao hata yanayopingana kwa staha na kuvumiliana.

Hata hivyo, maoni ya viongozi hao, pamoja na kuzungumza kuwa ni maoni yao binafsi yalitafsiriwa na wengi kama msimamo wa serikali uliokosolewa na baadhi ya wananchi kwa madai kuwa haukuzingatia maoni ya wengi.
Tags:

0 comments

Post a Comment