IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI Mkuu wa zamani, John Malecela, amesema kuwa CCM imewakosea adabu maaskofu hivyo inapaswa kukutana nao na kuwaomba radhi.Akizungumza na Mwananchi jana, Malecela alisema kitendo cha kuwashambulia maaskofu hao kilichofanywa na CCM mkoani Arusha ikiwa ni pamoja na kuwataka wavue majoho na kuingia kwenye siasa, ni utovu wa nidhamu.
Kauli ya Malecela ambaye pia ni kada wa CCM, imekuja siku mbili baada ya chama hicho mkoani Arusha kuwataka maaskofu mkoani humo, kuvua majoho na kutangaza kuingia kwenye siasa, badala ya kuingilia mambo ya siasa yasiyowahusu ya Meya wa Jiji la Arusha.
Januari 7 mwaka huu, maaskofu wa Makanisa ya Kikristo mkoani Arusha, walitoa tamko la pamoja la kutomtambua Meya wa Jiji la Arusha aliyeteuliwa na CCM na kuweka bayana kwamba "hawatampa ushirikiano".
Walitoa tamko hilo wakati wakilaani hatua ya polisi mkoani Arusha kutumia nguvu kupita kiasi katika kuvunja maandamano ya amani ya Chadema na hivyo kusababisha vifo vya watu wanne na kujeruhi wengine zaidi ya 20.
Akisoma tamko la umoja wa viongozi wa dini ya Kikristo mkoani Arusha, Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Arusha, Josephat Lebulu alisema Jeshi la Polisi ndilo lilikuwa chanzo cha vurugu hizo.
"Sisi kama viongozi wa dini hatuwezi kushirikiana na mtu ambaye hakushinda kihalali, kuna mtu alipiga kura si diwani wa Arusha, Chadema hawakushirikishwa na pia taratibu na kanuni za uchaguzi huo zilikiukwa," alisema askofu huyo.
Lakini, Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, aliwaambia waandishi wa habari juzi kuwa kitendo cha maaskofu hao kusema hawamtambui Meya wa CCM, Gaudence Lyimo, kimewashtua.
"Tunawaheshimu sana viongozi wa dini...Ila wanapoingilia masuala ya siasa ni bora wavue majoho tukutane viwanja vya siasa kama alivyofanya mwenzao Dk Slaa," alisema Chatanda.
Katibu huyo ambaye ndiye chanzo cha mgogoro wa uchaguzi wa umeya wa Arusha hasa kutokana na kupiga kura kama diwani wa Arusha, ilhali alichaguliwa mbunge wa viti maalumu kupitia Mkoa wa Tanga, alisema masuala ya kisiasa waachiwe wanasiasa.
Chatanda ambaye katika mkutano huo alikuwa na mwenyekiti wa CCM Mkoa, Onesmo Ole Nangole, alisema kazi ya maaskofu ni kuelekeza njia za imani za kwenda mbinguni na sio siasa.
"Waje kwenye siasa wagombee udiwani...ili wachague meya. Tulitegemea kabla ya tamko lao wangetuita sote na tukae na tutoe maelezo yetu na hapo ukweli wangeupta, lakini kusema uchaguzi haikuwa halali sio kweli," alilalamika Chatanda.
Wakati katibu huyo wa mkoa wa CCM akieleza hayo, Katibu Mkuu wa chama hicho, Yusuf Makamba alienda mbali zaidi na kuwataka maaskofu hao waende mahakamani au wawashauri Chadema kufanya hivyo kwa lengo la kupinga matokeo ya umeya.
Makamba alisisitiza kuwa msimamo wa CCM ni kwamba chama hicho ndicho kilichoshinda katika uchaguzi huo wa umeya Arusha.
Alisema hakuna njia ya kubadili matokeo hayo zaidi ya kufungua kesi mahakamani.
Lakini jana Malecela alisema CCM inatakiwa kutumia busara kushughulikia mgogoro wa umeya mkoani Arusha badala ya jazba na utovu wa nidhamu.
Alisema kauli ya katibu huyo wa CCM dhidi ya maaskofu inakera na ili kuweka mambo sawa, ni bora chama hicho tawala kiwaombe radhi viongozi hao wa dini.
"Ni wazi kwamba alichokisema Chatanda hakiwezi kuwa kauli ya chama. Hayo ni maneno yake na ni utovu wa nidhamu. Nasikitika sana kauli ni ya kwake na si ya chama hivyo aombe radhi," alisema Malecela ambaye alibainisha kuwa chama cha siasa hakina uwezo wa kuwataka maaskofu wavue majoho.
Kwa mujibu wa Malecela, viongozi wa dini wako tangu enzi za kale na wamekuwa wakiikosoa Serikali tangu wakati huo na haiajawahi kutokea kiongozi wa chama akawarukia kwa maneno makali kiasi hicho.
Malecela alisema hiyo sio kauli ya CCM, lakini kwa kuwa imetolewa na mwanachama wake, chama hakina budi kukutana na viongozi hao wa dini na kuwaomba radhi.
Kauli iliyotolewa ni ya kutokuwa na adabu kwa watu kama maaskofu," alisema Malecela.
You Are Here: Home - - Malecela: CCM imekosa adabu kwa maaskofu
0 comments