Mb. wa Arusha Mjini Mh. Godbless Lema akiwa amelazwa kutokana na majeraha wakati wa vurugu Arusha
WANANCHI waliouawa kwa kupigwa risasi na polisi katika vurugu za kuvunja maandamano ya CHADEMA wiki iliyopita wanatarajiwa kuagwa kishujaa katika viwanja vya NMC mjini Arusha keshokutwa.
Siku hiyo itatumiwa na wanachama wa CHADEMA, wananchi wa Arusha na ndugu, jamaa na marafiki wa marehemu hao kuwaaga kwa kuwasomea dua marehemu hao: Ismail Omary (40) na Denis Michael Ngowi (30) ambao wanatajwa kufa kishujaa wakiwa katika harakati za kutetea demokrasia.
Tamko hilo lilitamkwa juzi na Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa, Freeman Mbowe, alipozitembelea familia za marehemu hao kwa ajili ya kuwafariji wafiwa na kutumia nafasi hiyo kuwaomba wasifanye mazishi mpaka siku hiyo watakapofanya maombolezo hayo.
Akiongozana na mbunge wa Arusha mjini, Godbless Lema, viongozi wa chama mkoani hapa sanjari na wabunge wa viti maalumu katika kuzitembelea familia hizo, Mbowe alisema lengo la kuwaaga marehemu wote kwa pamoja ni kuwapa fursa wananchi wote wakiwemo wafuasi wa chama hicho nchini kuwaaga marehemu hao kwa pamoja.
“Jamani haki haiombwi, haki inatafutwa hawa waliokufa ni mashujaa wa kweli hivyo sisi tunapanga kuwapa fursa wafuasi wote wa CHADEMA na wananchi kwa pamoja, ili tuwaage marehemu katika eneo la NMC na kila mtu atoe heshima zake za mwisho,” alisema Mbowe.
Hata hivyo, Mbowe alisema chama chao bado kinafanya mawasiliano na familia za marehemu hao ili kuangalia uwezekano wa kuwaaga marehemu hao kwa pamoja huku akisema bado chama chao pia kinafanya juhudi za kufuatilia maiti mbili zilizopelekwa hospitali ya KCMC majira ya usiku siku ya tukio hilo zikiwa na risasi mwilini.
Akizungumza kwa hisia Lema alisema ya kuwa kitendo cha kuwafyatulia risasi na kuwaua marehemu hao ni cha kinyama kwani wengine siku hiyo walikuwa wakisaka mkate wao kwa ajili ya kupelekea familia zao na kudai kuwa kitendo cha jeshi la polisi kuwaua raia hao huenda kikazisababishia ukali wa maisha familia zilizofiwa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa CHADEMA mkoani Arusha, Samson Mwigamba, aliiambia Tanzania Daima kuwa mazishi hayo yatafanyika katika viwanja hivyo kulingana na imani za marehemu hao pamoja na wananchi kutoa heshima zao kabla ya viongozi wa chama hicho kutawanyika kwenye makundi mawili, moja litasindikiza mwili wa marehemu Omary kuelekea kijiji cha Laki Tatu kata ya USA River kutakakofanyikia mazishi yake na lingine likielekea Rombo Mkuu mkoani Kilimanjaro kutakakofanyika mazishi ya Ngowi ambapo huko watapokelewa na mbunge wa jimbo hilo, Joseph Selasini, pamoja na viongozi wengine wa chama.
Hata hivyo, alisema kuwa mwili wa Raia wa Kenya, Paul Njuguna Kayele, ambaye polisi walidai anaitwa George Waitara bado hawajajua utazikwa lini ila kwa sasa chama hicho kinaendelea kufanya mawasiliano na balozi mdogo wa Kenya pamoja ndugu wa marehemu.
Mwigamba alisema CHADEMA imegharamia mazishi hayo ambapo imetoa ubani wa sh 500,000 kwa kila familia ambapo shughuli hizo zinaratibiwa na kamati ndogo ya mazishi iliyoundwa na chama hicho inayoongozwa Magoma Derrick Jr.
Januari 5, mwaka huu polisi walipambana vikali na wafuasi wa CHADEMA hadi kusababisha vifo vya watu wanne na wengine 16 kujeruliwa vibaya.
Aidha polisi wanadaiwa kuendeleza udhalilishaji kwa kuwapiga waandishi wa habari mkoani Arusha pamoja na kuwajeruhi vibaya ikiwa ni pamoja na kuharibu vitendea kazi vyao zikiwamo kamera.
Wakati huohuo, Chama cha Mapinduzi (CCM) kimesema wao si wa kulaumiwa katika sakata hilo.
Kadhalika, chama hicho kimewaeleza viongozi wa dini kuwa wana haki ya kutoa sauti zao pale wanapobaini kuwa kuna ukiukwaji wa demokrasia kama ilivyotokea kwenye uchaguzi wa Meya na Naibu katika jijiji la Arusha.
Kauli hiyo ilitolewa jana jijini Dar es Salaam na Katibu Mkuu wa CCM Taifa, Yusuf Makamba, alipozungumza na Tanzania Daima kwa njia ya simu ya kiganjani.
“Kama uchaguzi haukuwa wa haki wanayo haki ya kusema kile walichoshuhudia kwani maaskofu ni Watanzania na wanaishi Arusha.
“CCM sio iliyoharibu uchaguzi, kilichotuponza ni kushangilia …wa kulaumiwa ni msimamizi wa uchaguzi huo,” alisema Makamba.
Makamba alisema hakuna cha ajabu kwa viongozi hao wa dini kupinga matokeo hayo, kwani ni Watanzania na kazi yao ni kusimamia maadili na haki katika jamii.
Alisema kuwa uchaguzi umefanyika na meya ametangazwa na msimamizi wa uchaguzi ni vema viongozi wa dini wakatumia ushawishi wao kwa kuwashawishi wale wote wanaopinga matokeo hayo wakaenda mahakamani.
“Kama sheria za uchaguzi za nchi hii zinavyoelekeza kuwa ni matokeo ya rais pekee ndiyo hayawezi kupingwa mahakamani, lakini haya mengine yote yanawezekana kupingwa hivyo ni bora waende mahakmani kuyapinga ili haki itendeke,” alisema Makamba.
Makamba aliendelea akitoa ufafanuzi kwa kusema meya aliyechaguliwa ni wa jiji la Arusha ambaye anatoka CCM hivyo si busara kusema meya huyo ni wa CCM.
Alisema chama chake hakistahili kutupiwa lawama kutokana na matokeo ya uchaguzi huo, kwani mchakato mzima wa uchaguzi huo ulisimamiwa na msimazi ambaye ni mkurugenzi wa jiji la Arusha ambaye anaweza kujibu maswali yote yanayohusiana na mkanganyiko wa uchaguzi huo na si CCM.
Makamba alitahadharisha kuwa si busara kwa viongozi wa vyama vya siasa nchini kushabikia maandamano kama kigezo cha kudai haki kwani njia kama hizo zinaweza kuligawa taifa.
Aidha, Makamba amewataka viongozi hao wa dini kujaribu kuwashauri viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kuacha kutafuta haki yao kwa kutumia maandamano na badala yake waende mahakamani ili sheria ifuate mkondo wake.
“Hawa viongozi watambue kuwa haki haipatikani kwa sala tu wala kwa maandamano haramu bali haki hupatikana kwa kupiga kura ama kwenda kwenye vyombo vya sheria ambako ni mahakamani pekee,” alisema Makamba.
Makamba aliwataka Watanzania kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa vyama vya siasa kuwa wasikubali kuiingiza nchi kwenye machafuko na badala yake wavitumie zaidi vyombo vya sheria ambavyo ni suluhu ya matatizo.
Wakati huohuo, sakata la kujiuzulu kwa Naibu Meya, Michael Kivuyo, limewafanya viongozi wa CCM Wilaya ya Arusha kufanya kikao cha dharura hadi usiku.
Habari za uhakika kutoka ndani ya kikao hicho zinasema suala la kujiuzulu kwa Naibu Meya ni mshtuko mkubwa kwa chama hicho ambapo hivi sasa wanalazimika kujipanga kwa mikakati mipya.
Habari hizo zinaeleza kikao hicho kiliitishwa mara moja baada ya kupata taarifa za kujiuzuru kwa Kivuyo ambaye walikuwa wakiamini yuko katika msimamo mmoja na chama hicho.
Kikao hicho kiliitishwa na Katibu wa CCM Mkoa wa Arusha, Mary Chatanda, na kufanyika katika ofisi za chama hicho huku hofu ya kurudiwa kwa uchaguzi ikitawala katika kikao hicho.
Aidha, baadhi ya viongozi wa chama hicho mjini hapa wanaona fedheha kwa chama hicho kuendelea kumuacha katibu huyo wa mkoa kushughulikia suala hilo wakati yeye ndiye chanzo cha vurugu zote hizo.
“Unajua hivi sasa chama kama vile hakina mwenyewe kwa sababu kila mwenye nafasi ndani ya chama anafanya anavyotaka bila kuonywa ama kushughulikiwa kutokana na udhaifu ulioko makao makuu,” alisema mmoja wa viongozi wa chama hicho.
Aliendelea kusema kuwa hata kushindwa kwa uchaguzi jimbo la Arusha mjini kulitokana na uongozi wa mkoa kipindi cha uchaguzi kuanza kuhamisha watumishi hovyo hata madereva hivyo kufanya watumishi kuishi kwa hofu.
Alifafanua hali hiyo ilipelekea kila mtumishi kufikiria jinsi ya kulinda kibarua chake badala ya kufikiria kukisaidia chama kupata ushindi hali iliyopelekea mgawanyiko mkubwa.
Akijibu maswali ya waandishi wa habari juzi katibu wa mkoa Mary Chatanda kuhusiana na madai ya yeye kuchangia kupoteza jimbo la Arusha alijibu kuwa wanaomtuhumu hawajui Katiba wala utaratibu wa chama hicho.
Aidha, wiki moja baada ya machafuko ya kisiasa jijini Arusha, jeshi hilo mkoani Kilimanjaro limefuta mikutano iliyoitishwa na CHADEMA kwa lengo la kuwashukuru wapigakura wao.
Kamanda wa Polisi Wilaya ya Moshi (OCD), Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Silvin Lukaga, alisema katika barua yake ya Januari 6 mwaka huu yenye kumbu namba namba MOS/A.7/3/A/VOL.1/31 kwa Katibu wa CHADEMA Manispaa ya Moshi kuwa kwa ujumla hivi sasa hali ya kisiasa si shwari, jeshi hilo haliwezi kutoa ruhusa ya mikutano ya kisiasa kwa sasa.
“Ofisi yangu inapenda kukujulisha rasmi kwamba ombi lako la kupatiwa kibali cha kufanya mkutano wa hadhara siku ya Jumamosi tarehe 8/1/2011 kwenye kiwanja cha Manyema kata ya Bondeni, hakijatolewa.
“Hii ni kutokana na hali halisi ya kisiasa kutokuwa shwari kwa ujumla mpaka ofisi ya OCD itakapopata maelekezo mapya,” ilisomeka barua hiyo ambayo Tanzania Daima inayo nakala yake.
0 comments