Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wakristo waguswa na mtafaruku wa Arusha

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter JUMUIYA ya Kikristo Tanzania (CCT), katika Ibada ya Kitaifa ya Krismasi kesho, itaweka msingi katika kuombea amani taifa hasa kwa maeneo yenye mtafaruku ikiwemo Jiji la Arusha kulikokumbwa na machafuko ya kisiasa katika uchaguzi wa meya hivi karibuni.

Maombi hayo yatafanyika yakisimamiwa na ujumbe wa mwaka huu unaosema “Amani Mbinguni na Duniani kwa Watu Aliyowaridhia.

Yesu Kristo Mfalme wa Amani,” ambaye amekuja kusambaza amani kwa jamii. Kumekuwa na mvutano wa nafasi ya umeya wa Arusha baina ya CCM na Chadema mkoani humo kuanzia Desemba 19, mwaka huu baada ya CCM na TLP kuchagua Meya aliyekataliwa na Chadema
kwa madai kuwa taratibu hazikufuatwa, hali iliyosababisha vyama hivyo viwili kila kimoja kuchagua meya wake.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na gazeti hili jana, Katibu Mkuu wa CCT, Mchungaji Dk. Leonald Mtaita na Askofu Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoliki la Dar es Salaam, Eusebius
Nzigirwa, walisema maadhimisho ya Krismasi yanaashiria amani ulimwenguni hivyo ni
muhimu kuomba na kuidumisha.

Dk. Mtaita alisema ujumbe wa mwaka huu unahusu amani, hivyo CCT imeona ni vyema kuusimamia ujumbe huo ili kukazia umuhimu wa kutunza amani iliyopo nchini na kwamba maombi yatafanywa kesho Kitaifa kuombea hali ya nchi ikiwemo hali iliyoko Arusha.

“Kutokana na ujumbe wa mwaka huu, CCT tunataka amani idumu, tofauti zetu za kiitikadi katika siasa zisituvuruge, tuvumiliane katika hizo ili kudumisha amani, kwa mfano mambo yanayoendelea Arusha na kwingineko, hayo ni ya kuombea hasa,” alisema Katibu Mkuu huyo.

Katika hilo, alisema CCT inaheshimu tunu na urithi mkubwa wa amani ulioachwa na waasisi wa taifa hili, walioongozwa na Mungu mwenyewe hivyo hizo tofauti hazipaswi kusababisha tunu hiyo ipotee, bali ziwaweke watu pamoja.

Alisema njia pekee ya kudumisha amani ni kukubaliana katika tofauti hizo na zile za kiimani kwa kutambua kuwa zipo na zitaendelea kuwepo na kuwataka Wakristo kote nchini na ulimwenguni kuruhusu Mfalme wa amani (Yesu Kristo) alete amani hiyo duniani.

Kwa upande wake, Askofu Nzigirwa alisema masiha (Yesu Kristo) alikuja duniani miaka 2000 iliyopita kuleta upatanisho baina ya binadamu na Mungu hivyo njia pekee ya kudumisha amani ni kumtii Mungu na kuacha kujitetea tunapokosa bali kuomba msamaha.

Alipoulizwa kuhusu hali ya kisiasa Arusha na masuala ya Katiba, Nzigirwa alisema “Nchi yetu ina tunu ya pekee aliyotuachia Baba wa Taifa (Mwalimu Julius Nyerere), tumejengwa katika misingi ya umoja na upendo, kuna dalili za mwelekeo wa ubinafsi kuliko mshikamano,
wanasiasa waache hayo, waweke mbele maslahi ya taifa na si yao binafsi.”

Kuhusu ratiba ya Ibada ya Krismasi Kitaifa kesho, Dk. Mtaita alisema itaanza saa 3.00 asubuhi katika Kanisa la Menonite, Upanga jijini Dar es Salaam na itaongozwa na Askofu Mkuu wa Kanisa hilo nchini na Mkuu wa Dayosisi ya Pwani, Stephen Mang’ana.

Ibada ya Misa ya usiku ya Krismasi leo kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Arbogast Mushi, itafanyika Kitaifa katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu (St Joseph) kuanzia 4.00 usiku na itaongozwa na Askofu Nzigirwa.

Desemba 25 kila mwaka, Wakristo nchini na ulimwenguni kote huadhimisha Sikukuu ya Krismasi ya kuzaliwa mwokozi wa ulimwengu, Yesu Kristo miaka 2000 iliyopita.

Mbali na ibada hizo za Kitaifa, makanisa mbalimbali yatafanya ibada zao kwa utaratibu wao.
Tags:

0 comments

Post a Comment