IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
WAZIRI wa Nishati na Madini, William Ngeleja, ameitaka Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Nishati na Maji (Ewura), kufanya ukaguzi wa mafuta kwenye kampuni zilizowekewa vina saba ili kubaini iwapo zimechakachua au la.
Hatua hiyo imekuja baada ya Ewura kuweka vina saba kwenye kampuni ya mafuta ili kudhibiti uchakachuaji.
Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Ngeleja alisema Ewura ilifanya hivyo awamu ya kwanza ya kudhibiti mafuta hayo ambayo inamalizika mwishoni mwa mwaka huu.
Ngeleja alisema kutokana na hali hiyo, ifikapo Januari mwaka huu, Ewura inapaswa kufanya ukaguzi katika kampuni zote kubwa na ndogo kuhakiki kama vina saba bado vinatumika au zimeshachakachua.
“Tulifanya kazi ya kuweka vina saba katika mafuta tangu mwezi wa tisa, lengo ni kudhibiti tabia ya baadhi ya wafanyabiashara kuchakachua, jambo ambalo lingeweza kuleta madhara kwa watuamiaji na wananchi kwa ujumla,” alisema Ngeleja.
Aliongeza kuwa zoezi hilo linamalizika mwishoni mwa mwaka huu na kwamba, Ewura wanapaswa kupita kwenye kampuni hizo kukagua upya kabla ya kuingia awamu ya pili.
Alisema ikiwa baadhi ya kampuni zitabainika kuchakachua, zitachukuliwa hatua kali ikiwamo kuwafikisha kwenye mamlaka husika kwa ajili ya kuchukuliwa hatua za kisheria.
Waziri Ngeleja alisema kutokana na hali hiyo, tatizo la uchakachuaji mafuta kwa baadhi ya wafanyabaishara wasio waaminifu linaweza kupungua.
Alifafanua kuwa, tatizo hilo sio la Ewura peke yake au wizara husika, bali wananchi wote kwa sababu wanahusika kwa namna moja au nyingine kuhakikisha usalama wa mafuta uko mikononi mwao.
Aliwataka wananchi kushirikiana na mamlaka husika kutoa taarifa iwapo watabaini tatizo hilo ili wahusika waweze kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
You Are Here: Home - - Ngeleja aishtua Ewura kuhusu wachakachuaji
0 comments