IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Jaji Omar Makungu
Salim Said
MJADALA wa katiba sasa umeingia sura mpya baada ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ) Jaji Omar Makungu kutaka iundwe katiba mpya inayokidhi matakwa ya Watanzania, akipingana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema anayetaka katiba iliyopo, iwekewe viraka.
Jaji Makungu ni mteule wa kwanza wa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein mara tu baada ya kuapishwa kuwa rais wa visiwa hivyo, kama ilivyo kwa Jaji Werema ambaye pia ni mteule wa kwanza wa Rais Jakaya Kikwete mara tu baada ya kuapishwa kuongoza nchi katika kipindi kingine cha miaka mitano.
Jaji Makungu aliliambia gazeti hili jana kuwa katiba mpya ni muhimu kwa sasa kwa kuwa itasaidia kuweka misingi imara ya taifa, akipingana na Jaji Werema ambaye aliweka bayana kuwa “Kuandika Katiba mpya hapana, lakini kufanya marekebisho kwa kuondoa au kuongeza mambo fulani kwenye katiba, ruksa,”.
Lakini Jaji Makungu kwa upande wake alisema "Hoja ya katiba mpya ni nzuri na watanzania wanapaswa kukaa na kutafakari ili kuweka misingi imara ya nchi yao kwa sababu misingi ya nchi inapatikana katika katiba tu,". “Kwa nini kusiwe na umuhimu wa katiba mpya sasa? Nadhali wananchi wamesema na wameonyesha kuwa kuna mahitaji na umuhimu wa kuandikwa Katiba mpya.
Hilo hatuhitaji kujadili kwa sababu wao ndio wenye nchi,” aliongeza Jaji Makungu ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).
Alisisitiza, “Ni vizuri watu wakakaa, wakatafakari na kuandaa mapendekezo ya hoja zao kisha kuyawasilisha serikalini. Serikali nayo ni wanadamu, kukiwa na hoja ya msingi watabadilika. Tume itaundwa na mchakato wa kuandikwa katiba mpya utaanza.”
Jaji Makungu alisema wazo la kuandikwa Katiba mpya ni jema lakini watu wanatakiwa kuwa makini katika kutoa mapendekezo yao, kwa sababu hapo ndio wanapoweza kuweka misingi ya taifa lao, watoto na wajukuu zao.
“Watu wafanye wasichoke, kama CUF walivyofanya wameandaa mapendekezo yao wamewasilisha serikali, Chadema nao wafanye, NCCR-Mageuzi na vyama vingine, wanaharakati na wadau wengine nao wafanye, serikali itabadilika tu,” alisema Jaji Makungu.
Kwa kauli hiyo Makungu ambaye aliteuliwa hivi karibuni kuwa Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar, anaungana na Rais Mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mawaziri wakuu wa zamani, Joseph Warioba na Frederick Sumaye na Jaji Mkuu Mstaafu Agostino Ramadhan kuunga mkono hoja ya kuundwa katiba mpya.
Madai ya Katiba mpya pia yamewahi kutolewa na Mamakamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Rwekaza Mukandala na Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ambaye alisema bayana kuwa katiba mpya iandikwe mapema kabla ya mambo kuwa mabaya.
Wakati Jaji Makungu akisema hayo, baadhi ya Watanzania wanaoishi ughaibuni wamesema suala la kuandikwa kwa katiba mpya ya Muungano halitakiwi kucheleweshwa tena.
Kauli hiyo ilitolewa na Jumuiya ya Wazanzibari wanaoishi nje kusema hatua ya Watanzania kudai katiba mpya kwa nguvu zote inathibitisha uelewa wao wa kiwango cha juu wa mapungufu yaliyomo katika Katiba iliyopo. Watanzania hao wanaoishi katika nchi mbalimbali za Ulaya na Marekani pia wamekipongeza chama cha CUF kwa uthubutu wao wa kuandaa rasimu ya katiba na kulazimisha kuiwasilisha serikalini kwa maandamano ya amani.
Katika taarifa yao kwa vyombo vya habari Jijini Dar es Salaam jana na kusainiwa na Katibu wake Abdulla Abdulla, ilibainisha suala la katiba mpya ni jambo lisiloepukika kwa sasa.
“Kwanza tunawapa pole na kuwafariji wanachama wa CUF na wananchi wote waliojeruhiwa au kukamatwa katika maandamano ya kuwasilisha rasimu ya katiba mpya; lakini tunawapongeza sana viongozi na wananchi waliojitolea kushiriki katika maandamano hayo na kufanikiwa kuiwasilisha rasimu hiyo,” alisema Abdulla.
Abdulla aliongeza, “Hatua hiyo waliyoichukua inathibitisha uelewa wao wa kiwango cha juu wa mapungufu yaliyomo katika Katiba iliyopo sasa ambayo haikidhi matakwa ya wananchi wengi wa Tanzania.” “Tunaamini kuwa rasimu hiyo ni kielelezo halisi cha matakwa ya wananchi walio wengi na itakidhi kabisa hoja zote za kikatiba na kisheria ambazo kwa muda wote zimekuwa ni miongoni mwa matatizo ya msingi yanayoidhoofisha demokrasia nchini,” alisema Abdulla.
Alisema wananataraji hatua iliyochukuliwa na wananchi itakuwa ni changamoto muhimu sana kwa viongozi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika ngazi zote na kila mmoja wao ataikubali na kuitafsiri kuwa ni kichocheo cha kufungua kwa upana zaidi milango ya siasa za uwazi na dira kamili ya demokrasia iliyokamilika.
“Tunaziomba taasisi zote za kiserikali na zile ambazo si za kiserikali kuunga mkono rasimu hiyo ili nchi yetu iweze kupata katiba mpya na tuachane na tabia ya kutia viraka kwani kufanya hivyo ni kuongeza matatizo badala ya kuyatatua,” alisema Abdulla.
You Are Here: Home - - HOJA KATIBA MPYA:Mwanasheria Mkuu Zanzibar ampinga Werema
0 comments