IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
CHAMA Cha Demokrasia (Chadema), kimeandaa maandamano makubwa nchi nzima kupinga bei mpya ya umeme iliyotangazwa Desemba 20 mwaka huu na Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura).
"Tutawaunganisha wanachama wetu wote wa mikoani tujumuike pamoja katika maandamano hayo ili kudai haki zetu za msingi, "alisema Mkurugenzi wa Oganization na Mafunzo wa Chadema, Singo Kigaira.
Kigaira aliwataka wafuasi wa chama hicho, wanachama na wananchi kuacha woga akieleza kuwa kila kitu kinahitaji mipango na katika maandamano hayo, kiongozi wa mipango hiyo ni Chadema.
Awali akizungumza katika mkutano huo, Mkurugenzi wa Habari wa Chadema, Erasto Tumbo, aliwaambia waandishi wa habari kuwa chama hicho kimeamua kuandaa maandamano hayo baada ya kutambua kuwa bei hiyo mpya ya umeme inamwumiza mwananchi wa kawaida.
"Maandamano hayo tutayafanya mwezi Januari na tutaomba wananchi watuunge mkono kwa sababu hii ni haki ya msingi. Hakuna sababu ya kuonewa hapa. Junuari tutatangaza siku maalumu ya maandamano hayo,"alisema Tumbo.
Aliendelea "Katika hali ya kawaida kabisa, mtu anakuwa na matumizi ya Sh1000 kwa siku, leo hii unampandishia umeme kwa asilimia 18.5, unadhani maisha yatakuwa rahisi kweli?”
Kwa mujibu Tumbo, Serikali ingeweza kutumia njia nyingine mbadala kuboresha upatikanaji wa umeme nchini bila kuwapandishia wananchi bei ambao kimsingi ni mzigo kwao.
Alisema moja kati ya njia hizo ni kufunga mitambo ya kisasa ya kuzalisha umeme ndani ya bahari ili kundokana na tatizo la upungufu wa maji ya kuzalisha nishati hiyo.
Tumbo alisema baadhi ya nchi duniani, zinazalisha umeme kwa kutumia maji ya bahari jambo ambalo lingeweza pia kufanyika Tanzania kama viongozi wangekuwa wabunifu.
“Pia Serikali ilipaswa kuboresha vifaa vya kutengenezea umeme wa jua ili umeme huo uzalishwe kwa wingi na sio kupandisha gharama za umeme kiholela na kutuumiza (wananchi),”alisema.
Kwa mujibu wa Tumbo, kiini cha kupanda kwa bei ya umeme ni deni kubwa la Serikali katika taasisi zake, wizara na ofisi nyingine ambazo kwa kawaida hazilipi kodi hivyo kinachotakiwa ni kuwaeleza wananchi ukweli kuhusu madeni hayo.
"Lazima tuelezwe ukweli kwamba Serikali na vigogo wake wanadaiwa shilingi ngapi kwani ndio hasa chanzo cha ongezeko la bei za umeme hapa nchini. Wananchi tumeshachoka kuburuzwa kama hatuna elimu, "alisema Tumbo.
Alisema ongezeko hilo la bei ya umeme la asilimia 18.5, linaamanisha kuwa uniti moja sasa itakuwa inauzwa kwa Sh 367.80 kiasi ambacho kitamuumiza mwananchi wa hali ya chini.
Tumbo alienda mbali zaidi na kusema anaamini kuwa Serikali imeamua kupandisha bei hiyo ya umeme ili kupata fedha za kuilipa kampuni ya Dowans inayoidai Tanesco mabilioni
Alisema haiingii akilini kuona Tanesco inapandisha bei ya umeme wakati baadhi ya Watanzania hadi sasa wanashindwa kumudu gharama za kuingiza nishati hiyo majumbani mwao.
Desemba 20 mwaka huu Ewura, iliruhusu Tanesco kupandisha bei ya umeme kwa asilimia 18.5 kuanzia Januari Mosi mwakani.
Mkurugenzi wa Ewura, Haruna Masebu, aliwaambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam kuwa ongezeko hilo la bei ni chini ya mapendekezo ya Tanesco kwa asilimia 16.1.
Kwa mujibu wa Masebu, Tanesco ilipendekeza umeme upande bei kwa asilimia 34.6, lakini baada ya uchambuzi wa kina, mamlaka ilikubali kuruhusu nyongeza ya asilimia 18.5 kwenye nishati hiyo.
You Are Here: Home - - Chadema yaandaa maandamano kupinga bei mpya ya umeme
0 comments