Katika siku ambayo vipaza sauti vilifedhehesha kutokana na vingi kutofanya kazi, wabunge waswili wapya wa Chadema walimchachafya Spika Makinda wakati wa zoezi la upigaji kura za kupitisha jina la Mizengo Kayanza Pinda kuwa waziri mkuu baada ya Rais Jakaya Kikwete kuwasilisha ombi lake jana jioni.
Makinda, ambaye amechukua nafasi hiyo kurithi mikoba ya Samuel Sitta, alitakiwa kutoa mwongozo na mbunge wa Ubungo, John Mnyika ambaye alitaka kujua dhana nzima ya usiri wa upigaji kura baada ya kubaini kuwa karatasi zilizoandaliwa zilikuwa na namba za mtiririko.
Hata hivyo, Spika Makinda alijibu kuwa karatasi hizo ziliandaliwa hata kabla ya kujulikana kwa jina lililopendekezwa na rais na kwamba kilichofanyika ni kuingiza jina baada ya pendekezo kuwasilishwa na kuchapwa kwa karatasi hizo.
"Kwa hiyo suala la serial number ni la mtambo... lakini hata katika usimamizi wa kura tumeweka watu tofauti hivyo wasingeweza kujua kura ni ya nani," alisema Makinda.
Lakini kibarua kigumu kilitolewa na mbunge mpya wa Singida Kusini, Tundu Lissu ambaye alihoji kitendo cha Spika Makinda kurukia hatua ya kupiga kura bila ya kumruhusu kiongozi wa upinzani bungeni kuchangia hoja iliyowasilishwa na serikali kama katiba inavyotaka.
Lisu, ambaye kitaaluma ni mwanasheria na ambaye anajuliakana kama mwanaharakati wa mazingira, alinukuu tafsiri ya kipengele cha 53 kinachobainisha kuwa kama hoja itawasilishwa bungeni na serikali, kiongozi wa upinzani anatakiwa apewe nafasi ya kuchangia, tofauti na hoja zinazopitia kwenye kamati za Bunge.
Alikuwa akimaanisha hoja iliyosomwa mbele yao na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Frederick Werema ya kuomba Bunge lipitishe jina la Pinda kuwa waziri mkuu.
Lakini Spika Makinda aliamua kuahirisha kutoa mwongozo wa suala hilo, akisema kuwa hatua ya zoezi la kupitisha jina ilishafikia mbali na hivyo hilo lingefanyika baada ya kura kuhesabiwa na matokeo kutangazwa.
Baadaye Spika Makinda alifafanua kuwa taratibu zilifuatwa kwa sababu hoja hiyo haikuwa ya serikali kwa kuwa "serikali bado haijaundwa" licha ya kwamba iliwasilishwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Makinda alisema kilichotokea kilitokana na hoja ya Kilango ambayo iliungwa mkono na wabunge na kuongeza utaratibuwa kujadili ulikuwa sahihi na kwamba wabunge kumi tu wakisimama kuunga mkono hoja ya mwenzao, kunakuwa hakuna haja ya kuendelea na mjadala.
Hoja ya Lisu ilitokana na pendekezo la mbunge wa Same Mashariki, Anne Killango ambaye alipewa nafasi ya kwanza ya kuchangia hoja ya Werema ya kuliomba Bunge lipitishe jina la Pinda.
Makinda, ambaye alipewa nafasi hiyo baada ya wabunge wa CCM kusimama kuashiria kuunga mkono hoja ya Werema, alitaka wabunge waipitishe bila ya kuijadili na kauli yake ikafuatiwa na wabunge wa CCM kusimama tena kumuunga mkono.
Kitendo hicho kilimfanya Spika Makinda aamue kutoendelea na mijadala licha ya kutangaza awali kuwa angetoa nafasi mbili na akataka wazunge wapige kura ya siri.
Wabunge 277 walimpa Pinda kura za ndio na wengine 49 walipiga kura za hapana.
Katika kinyang'anyiro cha unaibu spika, mbunge wa Kongwa, Job Ndugai aliibuka kidedea baada ya Habib Mnyaa wa (CUF) kujitoa huku kwa kile alichoeleza ni kuwania nafasi nyingine ya ubunge wa Sadc.
Hata hivyo, uamuzi huo ulipingwa na katibu wa kambi ndogo ya upinzani, David Kafulila ambaye alisema msimamo huo haukuwa wa kambi hiyo na kwamba, wao walipinga.
"Msimamo wa Mnyaa kujitoa ni wake binafsi. Msimamo wa kambi ndogo ni Mnyaa ndiyo mgombea. NCCR Mageuzi haiungi mkono Mnyaa kujitoa ingawa ni haki yake kikatiba na kanuni," alisema.
Ndugai aliibuka mshindi kwa kupata kura 276 sawa na asilimia 84.2 ya kura 328 zilizopigwa, huku mgombea wa Chadema Mustapha Akoonay akipata kura 46 huku kura 6 zikiharibika.
Shughuli hiyo ya jioni ilitawaliwa na fedheha za vifaa vilivyowekwa kwenye ukumbi huo wa kisasa wa Bunge kutofanya kazi.
Wakati akifunga Mkutano wa Tisa wa Bunge, kiongozi wa zamani wa chombo hicho, Samuel Sitta alitangaza kuwa ukumbi huo, ambao ulianza kutumika mwaka 2005, ungefanyiwa ukarabati mkubwa ili uweze kuendana na mahitaji ya Mkutano wa Kumi.
0 comments