Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - SUMAYE: MSICHAGUE MAFISADI MWAKA HUU

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Waziri mkuu mstaafu, Frederick Sumaye.
WAZIRI mkuu mstaafu, Frederick Sumaye jana aliibuka hadharani na kutoa hotuba kali ya kukemea wagombea wanaotoa rushwa, akisema kuwa njia pekee ya kuwadabisha ni kuwanyima kuta Oktoba 31.Sumaye, ambaye alijaribu karata yake kwenye urais mwaka 2005 na kuangushwa, alisema tatizo kubwa linaloikabili nchi kwa sasa, hasa wakati wa uchaguzi ni rushwa, na hivyo akashauri wananchi watumie silaha yao ya kura kuwashikisha adabu wote wanaotaka uongozi kwa kutoa rushwa.

Sumaye, ambaye hotuba hiyo ni kali ya kwanza kwake tangu astaafu uwaziri mkuu mwaka 2005, alisema: “Rushwa ni tatizo kubwa Tanzania hasa nyakati za uchaguzi.. lazima sote kama taifa tupige vita tukatae utaratibu wa watu wanaotaka uongozi kwa kutununua kama njugu sokoni na tuanze katika uchaguzi huu.”

Sumaye alitoa kauli hiyo katika ibada ya kuwekwa wakfu na kuingizwa kazini kwa askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Pare, Charles Mjema na msaidizi wake, Mchungaji Timothy Msangi.

Sherehe hizo zilihudhuriwa na maaskofu 25 kutoka ndani na nje ya nchi, wakiongozwa na mkuu wa kanisa hilo, Dk Alex Malasusa, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe na viongozi wa serikali na wananchi.

Sumaye alisema watu wanaochaguliwa kwa kutoa rushwa huwa hawawathamini wananchi wanapopata uongozi na kwamba hutumia kipindi chao cha miaka mitano kukusanya fedha nyingine kwa ajili ya kuhonga tena wananchi ili warejeshwe madarakani.

"Hivi sasa inaonekana huwezi kushinda uchaguzi bila kuhonga wapigakura. Kwa staili hiyo mshindi anakuwa kiongozi si kwa sababu anapendwa na watu bali kwa sababu ya kununua uongozi," alisema mbunge huyo wa zamani Hanang, ambaye alikumbwa na tuhuma nyingi za kashfa wakati akielekea kuwania urais.

“Kiongozi anayepatikana kwa njia ya rushwa yeye mwenyewe lazima ni mwizi na ni fisadi, vinginevyo hizo fedha za kuhonga angezipata wapi. Kiongozi mtoa rushwa ni mali ya watu fulani, yaani wale waliompa fedha.”
Waziri mkuu huyo mstaafu alisema kiongozi wa aina hiyo hawezi kuwa na huruma kwani anawaona wananchi wake kama bidhaa sokoni.
“Mimi nasema hivi; hata kama mgombea ni wa chama chako lakini unajua alihonga; hata kama na wewe hizo fedha zilikufikia na ukazila, usimpigie kura Oktoba 31. Hivyo ndio njia pekee tutakayowashikisha adabu.”

Sumaye ambaye hotuba yake ilikuwa ikikatishwa mara kwa mara kwa makofi ya kumshangilia, alisema kiongozi anayeingia madarakani kwa rushwa atatumia miaka yake mitano kutafuta fedha za kuwahonga wananchi kwa kipindi cha pili.
Naye Askofu Mjema alisema KKKT haishabikii chama chochote cha siasa wala mgombea lakini linao wajibu wa kuwahimiza waumini wake kuchagua viongozi watakaoweka mbele maslahi yao.

“Tunahitaji kupata viongozi waadilifu na waaminifu. Ni aibu kwa Mtanzania kurubuniwa kiasi cha kuuza haki yake ya msingi ya kuchagua kiongozi anayefaa. Tumesikia ipo minong’ono ya watu kununua shahada hii ni dhambi,” alisema.
Askofu Mjema alisema moja kati ya mambo yanayotoa dalili mbaya nchini ni namna neno “wapinzani’ linavyotumika kiasi kwamba wapo walioko upinzani ambao biashara zao zimehujumiwa, kutishwa maisha au kubambikiwa kesi.

“Hii ni ishara tosha kuwa na tunaweza kufikia mahali tukakifanya kisiwa cha amani duniani (Tanzania) kikawa kisiwa cha vurugu duniani. Ni vyema Watanzania, vyombo vya dola na wanasiasa tukawa makini na jambo hili,” alisema.
Askofu Mjema ametoa wito kwa wataalamu wa Kiswahili kutafuta msamiati mbadala wa neno “wapinzani” ambao utatumiwa na Watanzania kutambuana katika uwanja wa siasa kuliko wa sasa unaoibua hisia za mgawanyiko.
Alipendekeza mwaka ujao uwe mwaka wa kutimiza ahadi na kurudisha mambo katika mstari na kuitaka serikali kuutumia mwaka kesho kujitathmini na kanisa linapeleka serikalini mambo ambayo hawajayakamilisha.

Askofu huyo alisema zipo taarifa hivi sasa kuwa wawekezaji mbalimbali wanaoikimbilia Tanzania kwa ajili ya kuchukua malighafi mbalimbali wataliachia taifa hili mashimo matupu na jangwa kwa kizazi kijacho pasipo kuwaachia urithi.
“Matatizo makubwa ya nchi za Afrika ni ukosefu wa viongozi watumishi. Wengi wa viongozi wanaoibukia katika rushwa na ufisadi kwa hiyo wanajitajirisha wenyewe na kuwaacha wananchi wao masikini,” alisema.

Alitumia mkusanyiko huo kuzipongeza serikali za rais mstaafu Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kwa namna walivyojituma katika kushughulikia mgogoro wa dayosisi hiyo uliodumu kwa miaka 12.
Askofu Mjema alisema anatumia siku hiyo ya jana kuutangazia ulimwengu kuwa mgogoro uliokuwepo sasa umekwisha na hiyo jana wachungaji wa Dayosisi ya Pare na ile iliyokuwa ikijiita ya Mwanga waliingizwa kazini kwa pamoja.

Alihidi kutumia nafasi yake kama askofu, kusimamia na kulinda upendo na amani miongoni mwa wachungaji, waumini na wazee wa kanisa katika wilaya za Same na Mwanga na akaomba ushirikiano katika kufikia malengo hayo.
Tags:

0 comments

Post a Comment