Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Slaa amuweka pabaya Salma

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Atumia nyenzo za serikali kumkampenia mumewe

Kinana amtetea


MWENYEKITI wa Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahaman Kinana amekiri kuwa Mke wa Rais, Salma Kikwete, hutumia ndege za Serikali wakati wa kumfanyia kampeni mume wake, Rais Jakaya Kikwete na wagombea wengine wa chama hicho katika nafasi za ubunge na udiwani.

Hata hivyo, Kinana amemtetea Salma Kikwete kwa kusema kwamba hakuna sheria iliyovunjwa kwa kuwa ndege hizo hukodishwa.

Kwa mujibu wa Kinana, hata mgombea urais wa CCM, Kikwete wakati mwingine hutumia ndege za serikali kwa kukodi pindi inapotokea ndege za mashirika binafsi zinazoaminika kwa usalama zimekodiwa na watu wengine.

Ufafanuzi huo wa Kinana unatokana na tukio la Mke wa Rais, Salma, kuwasili mkoani Mara kwa ndege ya Serikali aina ya Focker 50, yenye namba 5H-TGF na kupokewa na viongozi wa Serikali akiwamo Mkuu wa Mkoa, Enos Mfuru, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Maram, Robert Boaz, Mkuu wa Wilaya ya Musoma, Geofrey Ngantuni na viongozi wengine wa mkoa na ngazi ya wilaya, wote wakifika uwanjani hapo kwa kutumia magari ya Serikali.

Baada ya kuwasili na kupokewa na wana-CCM uwanjani hapo, tofauti na ziara nyingine ambazo zimekuwa zikitangazwa ili wananchi wajitokeze kumpokea, wakati huu haikutangazwa na hivyo alipokewa na watu wanaoaminika wafuasi wa CCM waliopewa taarifa kwa masharti ya kutotangaza ujio huo.

Kiongozi huyo baada ya kupokewa na kukagua vikundi vya ngoma alipanda katika gari lililokuwa na namba za kiraia aina ya VX V8 Land cruiser T206 BJY lakini linaloaminika kuwa ni la serikali; huku ujumbe wake ukitumia pia magari ya serikali kuelekea Ikulu ndogo, Mjini Musoma.

Akizungumzia hali hiyo, Kinana alikiri Salma kutumia ndege ya serikali na kwamba si katika safari yake ya Musoma tu bali hata alipokwenda Mwanza alitumia ndege ya serikali. Alisema ndege hiyo imekuwa ikikodiwa kutoka kwa Wakala wa Ndege wa Serikali na kwamba mtu yeyote anaruhusiwa kukodi ndege hizo.

“Tumekuwa tunatumia ndege za Serikali kwa kukodi hasa pale ndege za mashirika binafsi ambazo tunaziamini kwa maana ya usalama wake zinakuwa zipo kwenye matumizi mengine. Kwa hiyo hatuwezi kutumia ndege nyingine tusizoziamini kiusalama, na kwa hivyo tunakodi ndege hizo. Tunazo risiti za malipo na mtu yeyote anaweza kukodi ndege hizo,”

“Kuna upotoshaji tu unafanywa na watu ambao wanajua ndege hizo zinaweza kukodiwa na yeyote. Kwa hiyo mgombea wetu wa urais aliwahi kutumia ndege hiyo katika baadhi ya kampeni na Mama Salma ameitumia mara kadhaa,” alisema Kinana na kusisitiza kuwa CCM inatambua vyema masharti ya sheria zote za Uchaguzi Mkuu na haiwezi kufanya kinyume kwa kuwa sheria hizo zimepitishwa chini ya Serikali ya chama hicho.

Hata hivyo, Kinana hakufafanua matumizi ya magari ya serikali katika mikutano ya kampeni ya Kikwete ambayo Mama Salma anaifanya akiandamana na viongozi wa mikoa.

Wakati CCM ikitoa ufafanuzi huo wa matumizi ya Salma Kikwete ya ndege ya serikali, taarifa zaidi kutoka mkoani Mara kuhusu ziara ya mama huyo zinaeleza kuwa, alizuru Wilaya ya Bunda baada ya kumaliza shughuli zake wilayani Musoma.

Akiwa wilayani Bunda alifanya mkutano wa ndani wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT) na pia ratiba ilimuelekeza kwenda Jimbo la Mwibara, Jumatatu wiki hii, lakini alishindwa kufanya hivyo kutokana na eneo hilo kuwapo mgombea wa urais wa CHADEMA, Dk Willbrod Slaa.

Taarifa hizo zinabainisha kuwa pamoja na kuwapigia debe wagombea wa CCM akiwamo mumewe Rais Jakaya Kikwete, Salma amekuwa akijitahidi kufanya usuluhishi wa makundi ili kuvunja kambi zilizoibuka wakati wa mchakato wa kura za maoni ndani ya CCM.

Hoja ya ufisadi inayotumiwa kumtambulisha Dk. Slaa ikionekana kumbeba katika taswira ya kukubalika zaidi kwa wapiga kura, imekuwa pia ikitolewa ufafanuzi na Salma Kikwete katika ziara zake hizo.

Kwa mujibu wa taarifa zilizotufikia, Salma amekuwa akizungumzia hoja ya ufisadi kwa maelezo kuwa Serikali ya CCM imefanya na inaendelea kufanya kazi kubwa kupambana na vitendo hivyo ambavyo alidai vilikuwapo tangu enzi za TANU. TANU ndiyo moja ya chama kiasisi cha CCM, kikiwa na rekodi ya kuongoza mapambano ya kudai uhuru.

“Jamani hata nyumba haiwezi kujengwa kwa siku moja. Nawaomba sana kuvunja makundi na kuwa pamoja na walioshindwa kura za maoni ili kuhakikisha CCM inashinda na hili ndilo lengo kuu la ziara yangu hapa. Muende nyumba hadi nyumba kueleza mafanikio ya Serikali ya Rais Kikwete ili wananchi watambue pumba na mchele ni upi,” alisema

Miongoni mwa wagombea ubunge aliowanadi Salma katika ziara yake hiyo ni pamoja na mgombea ubunge wa Musoma Mjini, Vedastus Mathayo na wagombea udiwani 13 wa kata za jimbo hilo. Mathayo anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mgombea ubunge jimbo hilo wa CHADEMA, Vicent Kiboko Nyerere.

Inaelezwa kuwa Mathayo awali alisitisha kuzindua kampeni zake kutokana na kile kilichoelezwa kuwa upepo wa kisiasa kuvuma vibaya baada ya Vicent Kiboko Nyerere kuanza kampeni. Mathayo anadaiwa kuahirisha uzinduzi huo wa kampeni ili kusubiri nguvu ya kiongozi wa kitaifa, ikitajwa kuwa alikuwa akimsubiri mgombea mwenza wa CCM, Dk. Gharib Bilal ili uzinduzi huo upate mshindo.

Katika ziara zake hizo, mke wa Rais, Salma amekuwa akiongozana na “waandishi wa habari” waliokuwa wamevalia makoti ya CCM yaliyoandikwa “Kikwete Press 2010”. Inadaiwa kuwa waandishi wa habari mkoani Mara ingawa walialikwa katika mkutano wa kampeni Musoma Mjini, lakini hawakupewa mwaliko wa kushiriki ziara za mke huyo wa Rais kwenye wilaya za mkoa huo.

Wakati Salma akimsaidia mumewe maeneo tofauti nchini, taarifa kutoka timu ya kampeni ya Kikwete inaeleza kwamba mgombea huyo wa CCM ameahidi kuwa akichaguliwa Serikali yake itanunua mashamba makubwa ya ardhi isiyotumika ili kuigawa ardhi hiyo kwa wananchi wanaoihitaji.

Hata hivyo, Rais Kikwete amesisitiza kuwa suala hilo litakuwa la makubaliano kati ya serikali na wenye mashamba hayo na kamwe serikali haitataifisha mashamba hayo kutoka kwa wenyewe.

“Kamwe hatutataifisha mashamba ya watu. Tutazungumza mpaka tuelewane”, Rais Kikwete alisema mwanzoni mwa wiki hii wakati aliposimama katika eneo la Kwashemshi, mkoani Tanga, kusalimia wananchi wakati wa mikutano yake ya Kampeni ya Uchaguzi Mkuu katika mkoa wa Tanga.

Mahitaji ya ardhi ya wananchi kujilimia mazao yao ya chakula na biashara yalikuwa moja ya vilio ambavyo Rais Kikwete amekumbana navyo katika mikutano mingi wakati wa ziara hiyo ya kampeni.

Kila changamoto hiyo ilipoibuliwa na wananchi, Rais Kikwete ameambiwa kuwa baadhi ya mashamba makubwa, hasa ya mkonge yaliyotaifishwa, yametelekezwa na wenyewe wakati wananchi wanaendelea kuhangaika bila kuwa na ardhi ya kujilimia.

Wananchi katika eneo la Kwashemshi, kwa mfano, wametoa mfano wa mwekezaji mmoja ambaye wanadai kuwa tokea anunue shamba hilo la mkonge kwenye eneo hilo miaka 13 iliyopita, hajapata kuonekana tena.

Mgombea huyo wa CCM leo amefanya mikutano ya kampeni na kusalimia wananchi katika maeneo ya Gombero, Maramba, Daluni, Mashewa, Matonge, Magoma, Makorora, Kwemazandu, Kerenge, Korogwe Mjini, Kwashemshi, Dindira na Bangalai, Bumbuli na Soni.

Mjini Korogwe, Rais Kikwete alirudia kuwahakikishia wananchi kuhusu azma ya Serikali ya kuhakikisha kuwa wananchi wanapata ardhi, akisisitiza kuwa Serikali yake inalijua tatizo la uhaba wa ardhi, na katika maeneo mengine ukosefu wa ardhi, na kuwa akichaguliwa tena kuongoza Tanzania atachukua hatua za kupunguza tatizo hilo.

“Hili la mashamba tuachie tuhangaike nalo. Hatutaweza kupata mashamba yote, lakini ni dhamira yetu kuzungumza na wenye mashamba makubwa ambayo hayatumiki na tuna matumaini kuwa matokeo ya mazungumzo hayo yatakuwa mazuri,” alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Tutachukua hatua za kuhakikisha tunawapatia wananchi wetu ardhi. Tutaifanya kazi hiyo kwa namna ambayo hatutatisha wawekezaji kwa sababu hawa ni watu muhimu kwetu. Tutakapokuwa tumeamua kupata ardhi basi tutazungumza na wenye ardhi ili waweze kutuuzia ardhi hiyo na tutawafidia kwa haki kabisa.”

Katika eneo la Magoma, wananchi wamemwambia Rais Kikwete kuwa kiasi cha wakazi 3,000 wa eneo hilo hawana ardhi ya kulima pamoja na kwamba shamba la mkonge katika eneo hilo limetelekezwa bila kuendelezwa.

Katika eneo la Matonge ambako wananchi wamemshukuru Rais Kikwete kwa kuwa Rais wa kwanza wa Tanzania kutembelea eneo hilo, pia ameelezwa tatizo la ukosefu wa ardhi ya wananchi kujilimia.

Rais Kikwete pia amewaambia wananchi katika maeneo mbali mbali ambako amesimama kuwa Serikali yake imedhamiria kuongeza kasi ya ujenzi wa barabara nchini na kwa maeneo aliyopitia amesema kuwa barabara ya Soni-Bumbuli-Dindira-Kwashemshi-Korogwe itajengwa kwa kiwango cha lami.
Tags:

0 comments

Post a Comment