Chadema: Dk Slaa kinara utafiti wa Synovate, KIKWETE AAHIDI TREKTA KWA WANAKIJIJI |
Monday, 20 September 2010 08:10 |
Boniface Meena,Siha MWENYEKITI wa Chadema, Freeman Mbowe amedai kuwa ana taarifa za matokeo ya utafiti uliofanywa na taasisi ya Synovate zinazoeleza kuwa mgombea wa chama chake, Dk Willibrod Slaa aliongoza kwa kukubalika, lakini taarifa hizo hazikuwekwa bayana. Wiki iliyopita Synovate, ambayo imekuwa ikifanya tafiti mbalimbali za kisiasa, kijamii na kiuchumi, ilitangaza matokeo ya utafiti wake juu ya jinsi ambavyo vyombo vya habari vimekuwa vikiripoti habari za uchaguzi mkuu, lakini taarifa hiyo haikuwa na kipengele ambacho kinazungumzia umaarufu wa wagombea na nani angeweza kushinda kama uchaguzi ungefanyika sasa. Lakini Mbowe amesema anazo taarifa kuwa Synovate wamefanya utafiti unaoonyesha kuwa Dk Slaa anaongoza kwa asilimia 45 na kufuatiwa na mgombea urais wa CCM, Jakaya Kikwete ambaye Mbowe alidai amepata asilimia 41. "CCM haitaki matokeo haya yatangazwe," alidai Mbowe wakati akihutubia umati mkubwa wa watu kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika Uwanja wa Isanja ulio Sanya Juu mkoani hapa. "Synovate haitakiwi iiogope CCM, itangaze matokeo ya utafiti wake bila ya kubadili ukweli. "Tuna hizo taarifa na niwaambieni tu, Synovate walifanya utafiti kujua ni mgombea gani na chama gani kinakubalika na utafiti wao unaonyesha kuwa Chadema inaongoza kwa asilimia 45 na CCM ina asilimia 41. Lakini, CCM inawatishia wasiitoe ripoti hiyo." Mbowe, ambaye aligombea urais mara moja kabla ya kuamua kugombea ubunge wa Jimbo la Hai, aliongeza kusema: "Nawataka Synovate watoe matokeo ya utafiti huo kwa kuwa ni muhimu sana kwa wananchi kuyatambua na kujua nini kinaendelea." Juhudi za kuwapata Synovate kuelezea kama utafiti kama huo umefanyika, hazikufanikiwa. Mbowe alisema kuwa nchi kwa sasa iko kwenye msiba mkubwa wa umasikini na kwamba uchaguzi mkuu ujao Oktoba 31, ndiyo njia pekee ya kuondokana na msiba huo. "Njia pekee ya kuondokana na msiba huu ni kuiweka Chadema madarakani ili kuondokana na umasikini uliokithiri," alisema Mbowe. Naye Dk Slaa alieleza kushangazwa na ahadi za Kikwete za kupandisha hadhi hospitali wakati zahanati zilizopo sasa hazina dawa. Akiwahutubia wananchi wa Arumeru kwenye uwanja wa Shule ya Msingi ya Usa River, Dk Slaa alisema kuwa ahadi hizo za Kikwete ni kiini macho kwa kuwa zinatoka wakati zahanati hazina dawa na wananchi wanaendelea kuteseka. Kikwete ameahidi kuzipandisha hadhi hospitali maalumu saba nchini kuwa za rufaa ili kuipunguzia mzigo Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MHN). Kutoka Kondoa, Fidelis Butahe anaripoti kuwa Kikwete aliwaahidi wananchi wa Kata ya Mrijo, Kijiji cha Mrijo atawapatia trekta la kulimia. Kikwete alitoa ahadi hiyo baada ya mwenyekiti wa kijiji hicho, Rashid Mdundo kusimamishwa na mgombea huyo wa urais aeleza matatizo ya wananchi wa kijiji hicho. "Shule za kata zote hazifundishi masomo ya sayansi na hakuna umeme, idadi ya walimu haitoshi, maji pia ni tatizo," alisema Mdundo, "Hapa kuna kisima kirefu tangu enzi za mkoloni, lakini kutokana na watu kuongezeka kwa wingi maji hayatoshi kabisa, kuna migogoro kati ya wakulima na wafugaji." Mwenyekiti huyo pia alisema kuwa matatizo mengine katika kijiji hicho ni ajira, kijiji kuwa mji mdogo pamoja na kutokuwa na barabara bora. Kikwete, ambaye aliwasili kijiji hapa saa 9:15 alasiri aliwaahidi wananchi hao kuwa atawadhamini ili wapate mkopo wa trekta kwa ajili ya kulimia. "Hili suala la kilimo nitawasaidia; cha kufanya nyinyi ni kuunda kikundi na mimi nitawasaidia ili mpate trekta kwa ajili ya kufanya shughuli zenu za kilimo bila kupata tatizo lolote, hii ni ahadi yangu na naahidi kuwa nitaitekeleza," alisema Kikwete. Kuhusu tatizo la umeme, Kikwete alisema: "Nimeona nguzo hapa sasa kama mnasubiri rais awavutie huo umeme jamani tutafika. Hii ni biashara; zungumzeni na watu wa Tanesco kwa kuwa wanafanya biashara." Aliwaahidi wananchi wa kijiji hicho kulifuatilia kwa ukaribu tatizo la maji katika kijiji hicho pamoja na kuiboresha barabara ya Handeni-Kondoa mpaka Singida kwa kuwa ipo katika ilani ya CCM. |
0 comments