Dola za Kimarekani zamponza mfanyakazi |
MFANYAKAZI wa Uwanja wa Kimataifa wa Ndege wa Mwalimu Nyerere, Said Kajembe, 28), jana alifikishwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala kujibu shtaka la kupatikana na pesa za kigeni kinyume cha sheria.
Mfanyakazi huyo ameshtakiwa kwa kosa la kukutwa na dola 39,800 za Kimarekani (karibu Sh54 milioni za Kitanzania), kinyume cha sheria.
Mrakibu wa polisi, Naima Mwanga alidai mbele ya Hakimu Janeth Kaluyenda kuwa Aprili 29 mwaka huu, saa 3:45 usiku mtuhumiwa akiwa uwanja huo alikamatwa na mmoja wa maofisa wa polisi na baada ya kupekuliwa alikutwa akiwa na kiasi hicho cha fedha.
Hata hivyo mtuhumiwa alikana alikana kufanya kosa hilo na mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Mei 18 mwaka huu itakapotajwa tena baada ya upande wa mashtaka kudai upelelezi bado haujakamilika.
Wakati huohuo, wakazi wawili wa Buguruni wamepandishwa kizimbani kwenye Mahakama ya Mwanzo ya Kariakoo kujibu tuhuma za kumshambulia kwa kumpiga mgambo wa manispaa hiyo na kumnyofolea vifungo vya sare za kazi.
Karani wa mahakama hiyo, Atanawe Kitogo aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Jabir Abdalah, 42, na Amini Athuman, 32, ambao ni wakazi wa jijini Dar es Salaam.
Wawili hao wanadaiwa kutenda kosa hilo Mei 2 wakiwa Mtaa wa Kongo ambako walimfanyia fujo askari huyo kwa kumnyofolea vifungo vya shati na kusababisha simu ya mkononi yenye thamani ya Sh80,000 kupotea.
Mtuhumiwa alikana kufanya kosa hilo na mahakama imeahirisha kesi hiyo hadi Mei 18.
0 comments