Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mazungumzo TUCTA, serikali yakwama

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter HATIMAYE mazungumzo yaliyokuwa yakisuburiwa kwa hamu kubwa kati ya viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA) na serikali yaliyofanyika Mei 8 mwaka huu yamekwama.
Hatua ya kukwama kwa mazungumzo hayo, imesababisha viongozi wa TUCTA kutoa siku 21 kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi wa Umma), Hawa Ghasia, kutoa tamko la serikali juu ya mapendekezo aliyowasilisha siku hiyo.

Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojiano maalumu katika ofisi za shirikisho hilo mjini Dar es Salaam jana, Kaimu Naibu Katibu Mkuu, Nicholaus Mgaya, alisema tamko la serikali ndilo litakalotoa msimamo mzuri wa kuahirisha mgomo au kuutangaza upya.

“Mtakumbuka Mei 8 mwaka huu, tulikutana na serikali kwa ajili ya kukaa meza moja kwa ajili ya mazungumzo ambayo kila mmoja wetu aliamini yatafungua ukurasa mpya, lakini siku hiyo hakuna makuabaliano yoyote yaliyofikiwa, sasa tumetoa siku 21 kwa waziri mwenye dhamana kutoa tamko la serikali,” alisema Mgaya.

Mgaya akizungumza kwa kujiamini, alisema mambo yote yaliyojadiliwa mwishoni mwa wiki hayakuwa na hoja mpya, hivyo kusababisha pande zote mbili kuondoka bila chochote kilichoafikiwa.

“Hapakuwa na muafaka wa aina yoyote baina ya wajumbe wetu na serikali, kwani hakuna makubaliano yaliyofikiwa, jambo kubwa tulilokubaliana ni uamuzi wa Waziri Ghasia kutoa tamko litakalojibu hoja zetu.

“Endapo atashindwa kuchukua hoja za upande mmoja na kuzifanya kama maamuzi, basi aturudishe katika mazungumzo tena,” alisema Mgaya.

Alisema jana ndiyo ilikuwa siku ambayo walikuwa wakiandaa na kujadili hoja hizo ili kutengeneza ripoti inayohusu majadiliano hayo ili waitoe mbele ya vyombo vya habari leo kwa nia ya kuweka wazi mambo yote.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, shirikisho hilo lilitoa tamko kuwa Rais Jakaya Kikwete hana mamlaka ya kubatilisha mgomo ulioitishwa bali chombo chenye mamlaka pekee ni Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi.

Katika tamko hilo, walisema endapo Rais Kikwete atafanya hivyo atakuwa anakwenda kinyume na Sheria ya Ajira na Mahusiano namba 6 ya mwaka 2004.

Walisema njia pekee ambayo Rais anatakiwa kuifanya ni kutoa majibu ambayo yangeweza kutatua matatizo sugu ya wafanyakazi ambayo yameanza muda mrefu kuliko kutoa vitisho.

Mei 3 mwaka huu, Rais Kikwete aliwaita ‘wazee wa mkoa wa Dar es Salaam’ kwenye Ukumbi wa Daimond Jubilee na kuzungumza nao mambo mbalimbali ukiwemo mgomo wa wafanyakazi.

Katika mazungumzo hayo, Rais Kikwete aliwaonya wafanyakazi hao kuwa yeyote ambaye angejaribu kushiriki mgomo huo angepambana na vyombo vya dola.

Lakini Rais Kikwete, alikwenda mbali zaidi kwa kuwaita viongozi wa TUCTA kuwa ni waongo, wanafiki na wazandiki ambao wanapaswa kuogopwa kwa kuupotosha umma.

Baada ya kauli hizo za Rais Kikwete, aliahidi pande zote mbili ya viongozi wa serikali na TUCTA kukutana kwenye meza ya mazungumzo kwa lengo la kupata muafaka, lakini mambo yameonekana kuwa bado mazito.
Tags:

0 comments

Post a Comment