IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
RAIS wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume ameeleza kusikitishwa na viongozi wa kisiasa wanaopita mitaani wakihamasisha wananchi kususa kura ya maoni ya kuundwa kwa serikali ya umoja wa kitaifa visiwani hapa.
Karume ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM (Zanzibar), alitoa kauli hiyo juzi jioni, wakati akifungua kongamano la viongozi wa matawi ya CCM katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu kwenye Hoteli ya Bwawani mjini hapa.
Kiongozi huyo alikwenda mbele na kusema ni jambo la kusikitisha kwamba miongoni mwa watu wanaopinga suala hilo ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, kikao ambacho ndicho kilichobariki azimio hilo.
Mbali ya hilo, Karume alisema iko siku ambayo hakuitaja, atalazimika kuwataja kwa majina wanasiasa hao wanaokwenda kinyume na matarajio mema ya Wazanzibari.
“Acheni kutia aibu katika suala hili kwa kushawishi wananchi kukataa kupiga kura ya maoni juu ya serikali ya umoja wa kitaifa…hili ni muhimu sana kwetu.
“Sitaki kuendelea zaidi katika suala hili kwa sababu hapa hapa katika mkutano huu wapo na wanajijua wenyewe, kwa hivyo kwa leo bora niishie hapa maana naweza kuwaumbua, viongozi wanaopinga suala hili wapo hapa,” alisema Rais Karume.
Pamoja na hilo, aliwataka viongozi wa matawi wa chama hicho katika vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu nchini kutumia vyema elimu yao kwa kusimamia umoja, mshikamano, amani na utulivu.
Akiizungumzia CCM, alisema kuwa imeweza kujenga misingi madhubuti ya kusimamia umoja, amani, mshikamano na utulivu kwa lengo la kupata mafanikio zaidi hali ambayo vijana wanapaswa kuitekeleza kwa nguvu zote.
Kwa sababu hiyo alisema anawashangaa wajumbe wa NEC ambao wamepitisha serikali ya umoja wa kitaifa katika vikao halali vya chama, wakigeuka na kupita kushawishi watu kukataa serikali ya aina hiyo wakati ndiyo yenye ufumbuzi wa matatizo ya muda mrefu ya kisiasa yanayoikumba Zanzibar.
Alisema kitendo cha kupinga hilo ni sawa na kupinga maamuzi halali ya chama kinachongoza na kuwa kitendo hicho hakiwezi kuvumilika hata kidogo.
Karume alisema watu wanaopita mitaani na kushawishi watu wasipige kura wakati ukiwadia, ipo siku watatajwa hadharani ili jamii iwatambue.
Aidha, alisema kiongozi yeyote asiyependa umoja wa kitaifa ni hatari sana na anatakiwa kuogopwa na kila mmoja kwa sababu kamwe hawatakii mema wananchi wa Zanzibar wala Tanzania.
You Are Here: Home - - Karume afichua siri nzito Asema kuna viongozi CCM wanapinga maridhiano
0 comments