Conservatives wapata ushindi, bila ya wingi wa kutosha
Chama cha upinzani cha Conservative nchini Uingereza kiko katika nafasi ya mbele kuweza kuchukua madaraka nchini humo leo Ijumaa baada ya kushinda viti vingi katika bunge katika uchaguzi uliokuwa na mpambano mkali na pia kupata kuungwa mkono na chama cha tatu kikuu nchini Uingereza.
Wakati chama hicho cha mrengo wa kati kulia cha Conservative kimeshindwa kupata ushindi wa moja kwa moja katika bunge la wawakilishi lenye wajumbe 650, na kusababisha kuwapo na uwezekano wa serikali ya mseto nchini Uingereza tangu mwaka 1974, chama hicho kina wabunge wengi zaidi ya chama cha mrengo wa kati shoto cha Labour, chama tawala kwa sasa.
Kiongozi wa chama cha Conservative, David Cameron, anatarajiwa kuelezea mipango katika taarifa baadaye leo hii, na chama chake kimesema atatoa maelezo ya jinsi gani atakavyoweza kuunda serikali ambayo ni imara na yenye nguvu ikiwa inaungwa mkono na wengi, na ambayo inafanya kazi kwa maslahi ya taifa.
Mtendaji huyo wa zamani wa masuala ya mahusiano na umma, mwenye umri wa miaka 43, amesema kuwa chama chake kitatekeleza kwa haraka na kwa kina upunguzaji wa matumizi kuliko chama cha Labour. Serikali yoyote mpya inakabiliwa na kazi ngumu ambayo huenda isiwapendeze watu wengi ya kupunguza nakisi kubwa katika bajeti ya taifa ya pauni bilioni 163 kwa mwaka wa fedha wa 2009/10.
Kiongozi wa chama cha Conservative, David Cameron, amesema kuwa yuko tayari kuiongoza Uingereza, akitoa mwaliko kwa chama cha Kiliberali kumsaidia kuunda serikali.
Nick Clegg amesema kwa kuwa chama cha Conservative kimeshinda viti vingi pamoja na kura nyingi katika uchaguzi huu, tunapaswa kupewa nafasi ya kuunda serikali. Na namshukuru kwa hilo. Kwa hiyo sasa tutaanza majadiliano na vyama vingine kuona jinsi ya kulitekeleza hilo.
Cameron ameongeza kuwa njia ya kutekeleza hatua hiyo ni kutoa uhakikisho wa maeneo fulani ya sera kwa vyama hivyo, na kutafuta makubaliano ya kuiruhusu serikali ya chama cha Conservative kuendelea kutawala bila ya nchi hiyo kukabiliwa mara kwa mara na kitisho cha serikali yake kuanguka. Moja ya maeneo hayo ya sera ni mabadiliko ya mfumo wa uchaguzi nchini humo ambao chama cha Kiliberali kinataka ubadilike.
Waziri mkuu, Gordon Brown, amesema katika taarifa baada ya uchaguzi kuwa alimwagiza katibu wa bunge la Uingereza kutayarisha muongozo wa bunge, utakaoweka pamoja makubaliano yaliyopo ambayo yanabainisha juu ya ya kuundwa serikali, ikiwa ni pamoja na mahali ambapo hakuna chama ambacho kimepata wingi wa kutosha.
Waziri mkuu, Gordon Brown, hajaondoa uwezekano wa kuendelea kuwapo madarakani, na kwa hivyo kuongeza hali isiyoeleweka ya hatima ya kisiasa ambayo imeleta hali isiyo tulivu katika masoko ya fedha ambayo tayari yanakabiliwa na kuporomoka kwa kiasi kikubwa kwa masoko ya hisa duniani pamoja na mzozo wa madeni ya Ugiriki.
0 comments