IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
UTAFITI umeonyesha kuwa zaidi ya nusu ya mawaziri waliotajwa kuwa makamanda katika Serikali ya Awamu ya Nne wanaweza kupoteza nafasi zao za ubunge kwenye Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2010.
Kwa mujibu wa asasi isiyo ya kiserikali, Nyota, iliyofanya utafiti huo katika kipindi cha miezi sita iliyopita, hali ni tete katika majimbo ya mawaziri hao.
Mawaziri hao wako hatarini kukosa ubunge kutokana na wananchi wengi wa majimbo hayo kukosa imani nao, baada ya kaulimbinu ya ‘maisha bora kwa kila Mtanzania’ kushindwa kuonekana kwa vitendo majimboni mwao.
Taarifa ya awali iliyotolewa na Mratibu wa asasi hiyo, Vincent Kornald Mkisi, ilisema kuwa mazingira ya mawaziri na manaibu hao kupoteza nafasi zao yalianza kuonekana tangu Januari mwaka huu.
Mkisi alitaja majina ya mawaziri walio katika hali mbaya kurudi bungeni kuwa ni pamoja na Profesa Peter Msolla ambaye anakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa aliyewahi kuwa Mbunge wa Jimbo la Kilolo, Venance Mwamoto ‘Motto’.
Duru za kisiasa zinasema kuwa Profesa Msolla alitarajia kudra za Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuligawa Jimbo la Kilolo na kuwa mawili, hivyo alijipanga kuwania ubunge katika eneo la Ilula ambako anakubalika zaidi kuliko maeneo mengine.
Profesa Msolla baada ya kubaini kwamba yuko katika hali mbaya kisiasa, aliamua kumtumia Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Dk. Athuman Mfutakamba, kumfanyia kampeni za wazi katika maeneo ya vijijini na wakati mwingine ‘kudandia’ ziara za mkuu huyo wa wilaya ili kuweza kuwafikia wapiga kura wengi.
Tanzania Daima Jumatano iliwahi kunasa barua ya waziri huyo kwenda kwa Mfutakamba, akimtaka amwandalie mikutano ya hadhara ya kichama huku akijua fika kwamba kiongozi huyo ni wa serikali.
Waziri mwingine anayetajwa kuwa katika kaa la moto kwa mujibu wa utafiti huo, ni Profesa Jumanne Maghembe, anayekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa mwanasheria wa kujitegemea, Joseph Tadayo.
Inaelezwa kuwa baada ya Tadayo kuweka bayana nia ya kuwania ubunge katika Jimbo la Mwanga, waziri huyo alianza mkakati wa kutumia nguvu kulazimisha kukutana na wazee kwa nia ya kuwaweka sawa na kujihakikishia kuilinda nafasi yake ya ubunge.
Hata hivyo, Profesa Maghembe anapaswa kujilaumu mwenyewe kutokana na kile ambacho wananchi wa Mwanga wamekuwa wakikitaja kuwa ni ubabe na kujiona ana haki ya kifalme ya kuliwakilisha jimbo hilo.
Lakini pia watafiti wanasema ameshindwa kuwaunganisha wananchi wa Mwanga, na kwamba hata waziri mkuu mstaafu ambaye pia alikuwa mbunge wa jimbo hilo, Cleopa David Msuya, hakubaliani naye.
Nyota imeonyesha kuwa pamoja na kuwa sura za vijana katika Baraza la Mawaziri ilionekana kuwa nuru mpya kwa wananchi na kuwafanya kuwa na imani na Serikali ya Rais Jakaya Kikwete, mawaziri wake wawili vijana, William Ngeleja wa Nishati na Madini na Dk. Lawrence Masha wa Mambo ya Ndani wako juu ya kaa la moto.
Ngeleja anakabiliwa na mchumi mwandamizi na mwanamageuzi wa kilimo anayeendana na falsafa mpya ya ‘Kilimo Kwanza’, Francisco Kimasa Shejamabu, ambaye pia ni meneja na mmiliki mwandamizi wa Kampuni ya Tanwat ya jijini Mwanza.
Aidha, habari zinasema kuwa Masha, anayeongoza Jimbo la Nyamagana, anakabiliwa upinzani mkali kutoka kwa kijana mmoja msomi kutoka kwenye moja ya vyuo vikuu nchini na ambaye ameonyesha nia ya kukabiliana naye ndani ya CCM.
Kana kwamba mchakato ndani ya CCM hautoshi, Masha na Ngeleja pia wanakabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa wagombea wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), wanaokubalika katika majimbo hayo kuliko ilivyo kwa mawaziri hao.
Habari zinasema kuwa Ngeleja alikuwa akiandaa mkakati wa kutaka matawi na kata za CCM katika Jimbo la Sengerema kutoa tamko la kumtangaza kuwa mgombee pekee ili aweze kupitishwa bila kupingwa.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa mpango wake huo umekwama kutokana na kuwapo kwa kundi kubwa la wanachama wa CCM walioamua kupingana na dhana hiyo na kutaka kuwapo demokrasia ndani ya chama chao.
Mwingine anayekabiliwa na hali mbaya ni Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Kapteni George Huruma Mkuchika (Newala), Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Diodoros Kamara (Nkenge), Waziri wa Sheria na Katiba, Mathiasi Chikawe (Nachingwea), Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkullo (Kilosa Kati), Waziri wa Kilimo na Chakula, Stephen Wassira (Bunda) na Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Mary Nagu (Hanang).
Kulingana na utafiiti huo wa Nyota, Mkisi alisema wanaamini kuwa baadhi ya mawaziri hao huenda wakaondoa majina yao kwenye mchakato ndani ya CCM kwa hofu ya kupata aibu.
Mbali na mawaziri hao waandamizi, utafiti huo pia umewataja manaibu waziri walio katika hali mbaya majimboni mwao.
Mawaziri hao ni pamoja na Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk. Emmanuel Nchimbi (Songea Mjini), Naibu Waziri wa Kazi, Ajira na Vijana, Dk. Milton Makongoro (Ukonga). Hata hivyo, Dk. Mahanga anaweza kupumua baada ya NEC kuligawa jimbo hilo katika majimbo mawili.
Wengine ni Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Adam Kighoma Malima (Mkuranga), Naibu Waziri wa Uvuvi na Ufugaji, Dk. James Wanyancha, (Serengeti), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Balozi Seif Ally Idd na Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk. Cyril Chami (Moshi Vijijini).
You Are Here: Home - - 'Nusu ya mawaziri wa JK hawachaguliki' • UTAFITI WAWATAJA, WAPONZWA NA KAULIMBIU YA ?MAISHA BORA?
0 comments