IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MWENYEKITI wa Chama cha Democrat (DP), Mchungaji Christopher Mtikila, anashikiliwa na Jeshi la Polisi Kanda Maalumu Mkoa wa Dar es Salaam kwa tuhuma za kuandaa na kusambaza waraka unaodaiwa kumkashifu Rais Jakaya Kikwete.
Tanzania Daima ilipata taarifa kuwa maofisa wa polisi kutoka Makao Makuu pamoja na Kanda Maalum ya Dar es Salaam waliokuwa wakiongozwa na Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda ya Dar es Salaam (ZDCO), Charles Mkumbo, walizingira nyumba ya Mtikila iliyopo Mikocheni B.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, askari hao walianza kufanya upekuzi katika nyumba hiyo jana, majira ya saa moja na nusu asubuhi baada ya kusikia taarifa za waraka huo uliokuwa umehifadhiwa kwenye kompyuta ya Mtikila.
Wakati maofisa hao wa polisi wamezingira nyumba hiyo, Mtikila na mkewe, Georgia Mtikila walilipigia simu gazeti hili, kuliarifu tukio hilo ambalo lilifanyika bila purukushani zozote.
Mtikila alisema katika upekuzi huo, askari hao waliichukua kompyuta moja inayodaiwa kuhifadhi waraka huo, wakaondoka naye hadi Kituo Kikuu cha Polisi kwa mahojiano zaidi.
Alisema timu ya maofisa wa polisi ilianza kumhoji kwa njia ya mdomo kuanzia saa nne asubuhi hadi saa nane mchana yalipomalizika ambapo aliomba aruhusiwe kutoka nje ili amuagize mkewe akamfuate wakili wake.
Kiongozi huyo alisema alifanya hivyo ili wakili wake awepo wakati polisi wanaanza kuchukua maelezo yake kwa maandishi.
Mtikila alisema alielezwa kuwa jeshi hilo lilifikia hatua ya kumkamata kwa sababu anakabiliwa na tuhuma za uchochezi kutokana na hatua yake ya kuandika waraka wa kutetea Ukristo, wenye kurasa 24.
Alisema katika waraka huo, amewataka Wakristo waungane ili waweze kumchagua rais Mkristo kwenye uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba.
Mtikila alisema kama Wakristo wakifanya hivyo, watakuwa wameunusuru Ukristo ambao hivi sasa upo shakani kutokana na kukandamizwa na utawala uliopo, ambao kwa mujibu wake unapendelea Uislamu.
“Polisi walinikamata asubuhi nyumbani kwangu wakachukua kompyuta yangu…na katika mahojiano yetu sijaukana ule waraka nimekubali ule waraka ni wangu kwani ili kuukana ule waraka nitakuwa namkana Yesu Kristo na mwokozi wangu.
“Serikali ya awamu ya nne inayoongozwa na Kikwete imeutesa Ukristo kuliko kipindi chochote kile tangu Ukristo uje nchini… ndiyo maana ni kosa la jinai katika awamu ya nne kuutetea Ukristo, lakini ni halali kwa waumini wa dini ya Kiislamu kufanya mikakati yote kuuangamiza Ukristo,” alisema Mtikila na kuongeza kuwa waraka huo uko mbioni kuchapwa ili kiwe kitabu kamili.
Tanzania Daima liliwasiliana na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, ambaye alithibitisha kukamatwa kwa Mchungaji Mtikila.
Kamanda Kova alisema wanamshikilia kiongozi huyo kwa tuhuma za kuandaa waraka huo na kuusambaza kwa baadhi ya wachungaji wa dini, ukiwa na ujumbe unaoweza kuhatarisha amani nchini.
Alisema polisi walifikia hatua ya kumkamata baada ya kupata taarifa kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, kwamba Mtikila ameandaa waraka huo na ameshausambaza kwa baadhi ya wachungaji.
“Ni kweli tunamshikilia Mtikila na tumefikia hatua ya kumkamata baada ya jeshi letu kupata taarifa hizo kutoka Idara ya Usalama wa Taifa, na tumemkamatia nyumbani kwake na kutokana na ukubwa wa tukio hilo, siwezi kulizungumzia, kwani jambo hilo liko chini ya Makao Makuu ya Polisi nchini,” alisema.
Hata hivyo, habari ambazo tumezipata wakati tunakwenda mitamboni, Mtikila ameachiwa kwa dhamana ya polisi na ametakiwa kuripoti leo saa nane mchana.
Hii si mara ya kwanza Mtikila kukamatwa kwa tuhuma za uchochezi, kwani mwaka juzi alikamatwa na kufikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa kosa la kusambaza waraka wa kumkashifu Rais Kikwete kwa kumuita gaidi anayetaka kuleta Mahakama ya Kadhi nchini.
Mtikila alibainisha kuwa, katiba ya nchi inatamka bayana kuwa Tanzania si nchi ya kidini. Kesi hiyo inaanza kusilizwa Aprili 22, mwaka huu.
Vile vile, Mtikila alishawahi kufikishwa katika mahakama hiyo akikabiliwa na kesi ya kutoa maneno ya uchochezi wakati akihutubia katika mkutano wake katika Viwanja vya Jangwani kwa kumkashifu Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere.
Mchungaji huyo alishawahi kushinda kesi ya kutoa maneno ya uchochezi dhidi ya Rais wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa alipomwita rais wa Msumbiji anayeuza nchi kwa Wazungu.
You Are Here: Home - - Mtikila atunga kitabu cha kumshambulia Kikwete
0 comments