Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Wazee wa Kigoma wamzuia Zitto kugombea nje

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
WAZEE wa mkoa wa Kigoma wamemtaka Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe agombee katika moja ya majimbo mawili mkoani humo na si vinginevyo.

Uamuzi huo ulifikiwa jana mara baada ya kumalizika kwa kikao baina ya wazee hao na mbunge huyo.

Zitto anakumbana na maamuzi hayo kufuatia kutangaza kuwa anaweza kugombea katika moja ya majimbo matano ambayo ni Kinondoni (Dar es Salaam), Geita (Mwanza), Kahama (Shinyanga), Kigoma Mjini na Kigoma Kaskazini.

Akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu, mara baada kumalizika kwa kikao, mwenyekiti wa wazee mkoani humo Bakari Menge alisema wamemkataza Zitto asigombee nje ya Mkoa wa Kigoma.

"Hata sisi tulishangazwa na taarifa ya kuwa Zitto anatafakari mahala pa kwenda kugombea, kutokana na hilo sisi wazee wa Kigoma tumemuita ili atueleze kwa kina kwa nini anataka kwenda kugombea nje ya mkoa huu.

"Pamoja na kumsikiliza yote aliyozungumza, uamuzi tuliofikia sisi wazee ni kwamba, Zitto lazima agombea Kigoma kati ya Jimbo la Kigoma Mjini au la Kaskazini na si vinginevyo," alisema Menge.

Menge alifafanua kwamba, pamoja na mambo mengine wamefikia maamuzi hayo kwa mustakabali wa baadaye wa kisiasa wa Zitto.

"Zitto hakuwa na sababu za msingi za kutokugombea mkoani hapa. Na sio kwamba tumemlazimisha ili agombee hapa nyumbani Kigoma, lakini tumemwambia ni kwa mustakabali wake wa baadaye katika siasa," alisema Menge na kuongeza:

"Licha ya kumpa muda akalifikirie hilo, kwa jinsi tulivyomuona ni lazima atakubaliana na ushauri wetu."

Akizungumza jana na gazeti hili, Zitto alisema amepokea ushauri wa wazee hao na kwamba uamuzi wake atautoa mwanzoni mwa mwezi Aprili mara baada ya kumaliza vikao vyake vya chama na wananchi.

"Ushauri wa wazee wangu wa Kigoma nimeupokea kwa umakini, lakini uamuzi wangu nitautoa wiki moja baada ya Machi 28, mwaka huu nitakapokuwa nimemaliza vikao vya chama na vya wananchi," alisema Zitto.

Mbali na wazee wa Mkoa wa Kigoma, Zitto ambaye ni Naibu Katibu Mkuu wa Chadema anatarajiwa kubanwa na chama hicho katika kikao cha Kamati Kuu kinachotarajiwa kufanyika Machi 27, mjini Dodoma huku wanachama wa Jimbo la Geita nao wakitarajia kukutana naye Machi 28.

Katika kikao cha kamati kuu, Zitto atajadiliwa na baadaye mapendekezo kutolewa juu ya jimbo ambalo atagombea ubunge kwenye uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba 25.

Juzi Zitto, aliliambia gazeti hili kuwa baada ya kikao cha kamati kuu atalazimika kwenda Geita kukutana na wananchi wa jimbo hilo.

''Machi 28, nitafanya mkutano na wananchi wa jimbo la Geita. Hii ni kutokana wananchi hao kunitaka niende nikazungumze nao,'' alisema Zitto

Akinukuliwa na gazeti hili hivi karibuni, Zitto alisema hadi sasa hajafanya uamuzi rasmi wa jimbo gani kati ya hayo, lakini uamuzi wa kugombea moja kati ya majimbo hayo utategemeana na utafiti ambao ameshaanza kuufanya kwa kutumia watu wake maalumu pamoja na ushauri kutoka kwa viongozi wa chama chake, ndugu, jamaa na marafiki zake.

"Siwezi kukurupuka na kutangaza tu kuwa nitagombea jimbo hili. Kwanza nimeshaanza kufanya utafiti wa kina katika hayo majimbo, pia uamuzi wangu utategemeana na ushauri kutoka kwa viongozi wangu wa Chadema, ndugu, marafiki na jamaa zangu," alisema Zitto.

Lakini alisema kuwa itakuwa vigumu kuwaacha wananchi wa Jimbo la Kigoma Mjini na la Kaskazini kwa vile ndiko alikozaliwa.

"Jimbo la Kigoma Mjini na la Kaskazini, yananiumiza kichwa kwa sababu yote yapo nyumbani nilipozaliwa. Lakini natumaini uamuzi wangu nitakaoutoa utazingatia mambo muhimu na wananchi watauheshimu na kukubaliana nami."

Tayari uongozi wa Mkoa wa Kigoma, umemega eneo la Mwandiga la Kigoma Kaskazini ambalo Zitto anakubalika na kulipeleka Kigoma Mjini. Eneo hilo lililomegwa linadaiwa kuwa ngome kuu ya Zitto na kwamba hatua hiyo inaweza kuchukuliwa kama sababu ya kuhamia Dar es Salaam.
Tags:

0 comments

Post a Comment