IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MAHARAMIA wa Kisomali wameiteka nyara meli ya mafuta karibu na Madagascar ikileta mafuta nchini na kuipeleka pwani ya Somalia, wamiliki wa meli hiyo wa Norway wameiambia Reuters.
Meli hiyo yenye jina la UBT Ocean, ilikuwa na mafuta kutoka Umoja wa Falme za Kiarabu kwenda Tanzania, Svenn Pedersen, wa kampuni inayomiliki meli hiyo, Brovigtank, alisema.
Uharamia umefanya eneo la bahari ya Hindi katika Pembe ya Afrika kuwa moja ya maeneo hatari zaidi duniani, licha ya kuwapo merikebu za majeshi ya kimataifa. Utekaji nyara huo huongezeka katika miezi ya Machi na Mei wakati ambao bahari huwa imetulia.
Pedersen alisema juzi kuwa wamiliki wa meli hiyo walipokea simu kutoka kwa nahodha akisema maharamia wamewavamia melini. "Baada ya taarifa hiyo mara moja tukapoteza mawasiliano na meli," Pedersen aliiambia AFP.
Meli hiyo ina usajili wa visiwa vya Marshall. Kutekwa nyara kwa meli hiyo kumetokea siku mbili tu baada ya maharamia kuiteka nyara meli nyingine ya mafuta ya Saudi Arabia na mabaharia wake katika Ghuba ya Aden na kuipeleka katika mji wa Garacad, Somalia.
Majeshi ya wanamaji ya kimataifa yanafanya doria katika eneo hilo la Ghuba na Bahari ya Hindi, lakini bado yameshindwa kuzuia uharamia huo unaofanywa na Wasomali.
Wiki moja iliyopita, wanamaji wa Marekani walifanikiwa kuinusuru meli yenye bendera ya Tanzania dhidi ya kutekwa nyara na maharamia wa Kisomali.
Helkopta SH-60B Seahawk kutoka manowari ya Jeshi hilo, USS Farragut, ilishambulia mashua iliyokuwa ikitumiwa na maharamia hao na kuweza kukamata wanane.
Kwa mujibu wa Ubalozi wa Marekani nchini, meli hiyo mv Barakaale 1, ilishambuliwa mara mbili na maharamia kabla ya timu ya wanajeshi hao kuwasili eneo la tukio. Somalia haina serikali imara tangu mwaka 1991
You Are Here: Home - - Wasomali wateka meli ikileta mafuta Dar
0 comments