IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SIKU moja baada ya Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, kudai Rais Jakaya Kikwete amepotoshwa kuhusu sheria ya gharama za uchaguzi, serikali imesema itaomba radhi na kurejesha muswada huo bungeni.
Akizungumza na Tanzania Daima jana, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Jaji Frederick Werema alisema:
“Kama kweli ikithibitika, tuko tayari kuomba msamaha na kurudisha bungeni suala hili ili lifanyiwe marekebisho… namhakikishia Dk. Slaa kuwa tutarudisha bungeni ili makosa hayo yaondolewe.
“Siamini na si dhani kama ni kweli, kwa sababu eneo hilo nakumbuka lilijadiliwa kwa kina mno, tena Dk. Slaa na John Cheyo (Mbunge wa Bariadi Mashariki) walitoa mchango mzuri uliozua mjadala mrefu na hatimaye tukafikia mwafaka.”
Dk. Slaa alidai Rais Kikwete amepotoshwa katika baadhi ya vipengele, kikiwamo kipengele kinachohusu uthitibishwaji wa wajumbe wanaounda timu za kampeni kwa ajili ya wagombea urais, wabunge na udiwani.
Alisema Bunge halikukubaliana kuhusu kipengele hicho, wala hakimo katika kumbukumbu za Bunge; na kwamba kiliongezwa baadaye, kabla ya Rais Kikwete kusaini muswada huo kuwa sheria.
Hata hivyo, Jaji Werema alishtushwa na kauli ya Dk. Slaa, na kudokeza kwamba inawezekana hata mwanasiasa huyo hakukielewa vema kipengele hicho.
“Nimeshutushwa na kauli ya Dk. Slaa… wasaidizi wangu wameniambia haya mambo, saa sijui tatizo liko wapi… nafikiri anapaswa kuelimishwa tu.
“Tunajua sasa zipo kampeni, hivyo kila mtu anataka kufanya au kufuatilia kwa makini sheria hii, sasa namshauri Dk. Slaa aisome kwa makini,” alisema Jaji Werema.
Alisema kumbukumbu zinaonyesha kuwa wakati wa kujadili muswada huo kila kipengele kilipitiwa kwa umakini wa hali ya juu na kuridhiwa na wabunge.
“Nakumbuka katika kumbukumbu zangu wakati tunajadili muswada huu tulipitia kipengele kwa kipengele; sasa haya mengine yatakuwa yametoka wapi?” alihoji Jaji Werema.
Alisema kama kweli kutakuwa na baadhi ya vipengele ambavyo vitakuwa vimechomekwa kwenye sheria hiyo kinyemela, sheria hiyo inaweza kurudishwa bungeni kwa ajili ya kufanyiwa marekebisho haraka.
Akizungumzia sheria hiyo, juzi Dk. Slaa alisema anashangazwa na kilichotokea Ikulu siku Rais Kikwete aliposaini sheria hiyo.
Dk. Slaa alisema atamchukulia hatua mtu aliyehusika kuongeza kipengele hicho bila idhini ya Bunge.
Katika kushangaa huko, Dk. Slaa alionyesha kitabu cha kumbukumbu za Bunge (Hansard), ambacho hakionyeshi viongozi wanaopaswa kufanya uhakiki wa timu za kampeni za wagombea.
“Katika sheria aliyosaini rais kuna kifungu cha 7 (3), ambacho hakikuwepo kabisa kwenye muswada uliojadiliwa na kupitishwa bungeni, kwa kweli nimeshangazwa sana, kwa sababu rais amedanganywa,” alisema Dk. Slaa.
Kabla ya kuzungumza na Jaji Werema, gazeti hili liliwasiliana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Salvatory Rweyemamu, ili atoe msimamo wa Ikulu.
Alisema hana jibu, akamshauri mwandishi wa habari hizi kuwasiliana na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, kwa kuwa ndiyo inayohusika zaidi na suala hilo.
“Sina cha kujibu katika hili, nakuomba uwatafute watu wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu, hawa ndio wako kwenye nafasi ya kuzungumzia suala hili kwa kina,” alisema Rweyemamu.
You Are Here: Home - - Serikali yakiri hoja ya Dk. Slaa nzito. • MWANASHERIA MKUU AJIANDAA KUOMBA RADHI
0 comments