Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Mpango wa CCJ kumtumia Nyerere wakwama

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter CHAMA cha siasa chenye usajili wa muda cha CCJ (Chama Cha Jamii), kimeondokana na mpango wa kutumia picha ya Baba wa Taifa Mwalimu Nyerere kwenye kadi zake za uanachama.

Hatua hiyo imesababisha chama hicho kichapishe kadi mpya tofauti na za awali zilizokuwa na picha ya Rais wa Kwanza wa Tanganyika na Tanzania.

Awali kadi hizo zenye rangi ya njano, zilikuwa na picha ya Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, mistari miwili ya rangi ya kijani na bluu pamoja na michoro ya familia ya baba, mama na mtoto.

Akizungumzia hatua hiyo jana, Katibu Mkuu wa CCM, Renatus Muabhi alikiri awali kuwa na picha ya Mwalimu, lakini iliondolewa baadaye kutokana na ushauri wa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa.

“Ni kweli tulikuwa na picha hiyo kwenye kadi zetu za uanachama kwa maana ya kumuenzi na kuunga mkono juhudi za Baba wa Taifa kulikomboa Taifa hili, lakini kabla ya kupata usajili wa muda, Msajili alituita na kutwambia tuiondoe,” alisema Muabhi.

Hata hivyo alilalamikia kitendo cha Msajili kuwataka waiondoe sura ya Baba wa Taifa kwenye kadi hizo, akishangaa kuwa awali wakati wanawasilisha maombi ya usajili ofisini kwake, Tendwa aliiona na kuwakubalia.

“Wakati tunawasilisha maombi yetu, tulimpelekea na sampuli ya kadi lakini hakuwa na kipingamizi, lakini muda mfupi kabla ya kutupa usajili wa muda, alituita tena bila barua na kutushauri kuiondoa picha hiyo.

“Alitwambia kuwa eti CCM wanalalamika kuwa Mwalimu alikuwa mwanachama wao, hivyo isingekuwa vizuri sisi kuitumia picha yake katika kadi zetu za uanachama,” aliongeza.

Pamoja na hatua hiyo, alisema kadi mpya zisizo na picha ya Mwalimu ziko tayari na kuwataka wanaopenda kujiunga na chama hicho waende katika ofisi za makao makuu yaliyoko Mwananyamala karibu na hospitali ya Wilaya Kinondoni, wakakate kadi za uanachama.

“Hatukati tamaa na tumeshachapisha zingine na yeyote anayehitaji aje na tunaziuza kwa Sh 500, lakini kwa wasio na uwezo, tunaweza kuwapa hata bure ili wajiunge na chama hiki,” alisema.

Si kawaida kwa kadi ya chama cha siasa kuwa na picha ya mtu au kiongozi wa chama chenyewe na pengine ndiyo sababu Msajili akawazuia kutumia kadi kama hizo, ingawa pia hatua hiyo ingeweza kuleta mtafaruku baina ya wafuasi wa CCM na CCJ.

Alipoulizwa sababu hasa za kutumia picha hiyo kwenye kadi ya uanachama, Mwenyekiti wa CCJ, Richard Kiyabo, alisema ufafanuzi kuhusu hilo, utatolewa kabla ya Machi 14 mwaka huu, ingawa hakutaka kusema ni lini hasa utatolewa.

Hata hivyo, alifafanua kuhusu rangi katika kadi yao kuwa njano inamaanisha utajiri wa nchi hususan wa madini, kijani ni uoto wa asili, bluu ni maji na familia ni Watanzania.

CCJ ilipata usajili wa muda hivi karibuni baada ya kusababisha mtafaruku miongoni mwa wanasiasa nchini, kikidhaniwa kuwa ni chama kitakachoigawa CCM kwa kuchukua vigogo ambao hawakubaliani na mwenendo wa chama hicho tawala.

Hata hivyo, uongozi wa chama hicho kipya umekuwa ukishikilia kuwa hakina uhusiano wowote na vigogo wa CCM wala mpango wa kuwachukua na kinajiandaa kushiriki uchaguzi mkuu mwaka huu.

Juhudi za kumpata Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Tendwa, kuzungumzia suala la picha ya Mwalimu kwenye kadi za uanachama, zilishindikana jana kutokana na simu yake kutopatikana.
Tags:

0 comments

Post a Comment