IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, Mwandishi wa habari za uchunguzi na Mtangazaji wa Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC 1), Jerry Muro amekoswakoswa kupigwa na kitu kinachoaminiwa kuwa ni risasi nje ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu alikokwenda kusikiliza kesi yake Ijumaa iliyopita...
Jerry ambaye alikuwa mahakamani hapo katika kesi yake anayotuhimiwa kuomba rushwa na watuhimiwa wengine wawili, alinusurika kupigwa na kitu hicho kinachoaminika kuwa ni risasi na badala yake ikampata mtu aliyekuwa naye mahakamani hapo.
Mtu huyo alifahamika kwa jina la Dk. Paul Andrew ambaye ni mtaalamu wa tiba za binadamu na ilielezwa kuwa alikuwa amekuja mahakamani hapo kumsindikiza Jerry kwa maelezo kwamba ni ndugu yake.
“Sisi tunaamini aliyekusudiwa ni Jerry Muro kwa sababu Dk. Paul alikuja kwa bahati mbaya tu na hatufikirii kama waliorusha risasi walikuwa wakijua kuwa mtu huyo atakuja mahakamani lakini tunaamini waliofanya kitendo kile walijua kuwa Muro atakuwepo kortini na inawezekana walikuwa wakimngoja nje ndipo akapigwa mtu wake mguuni.” Kilisema chanzo hicho.
Habari zinasema, Dk. Paul baada ya kujeruhiwa akitokwa na damu nyingi, kitu kilichowashitua watu wengi walioshuhudia tukio hilo.
Mtoa habari huyo aliongeza kuwa walishuhudia gari moja dogo lenye ‘tinted’ ambalo hawakuweza kujua namba zake likitoka eneo hilo kwa kasi, kitu kilichowafanya waamini kwamba watu waliotenda kitendo hicho cha kurusha kitu kilichomjeruhi daktari huyo, walikuwa humo.
Chanzo hicho kilizidi kupasha kuwa baada ya watu, akiwemo Jerry kuona daktari huyo akivuja damu kupita kiasi mguuni huku akiwa ameanguka chini, waliamua kumkimbiza Hospitali ya Marie Stopes Mwenge ambako anafanyia kazi.
Habari zinasema alipofikishwa hospitalini hapo aliingizwa moja kwa moja chumba cha upasuaji ambako jeraha hilo lilishonwa.
Mwandishi wetu alimpigia simu juzi Jumapili Jerry na kumuuliza tukio la kurushiwa risasi iliyompata Dk. Paul lakini awali alikataa kusema chochote, hata hivyo, baada ya kubanwa sana akathibitisha kutokea tukio hilo.
“Ni kweli Dk. Paul nilikuwa naye mahakamani alinisindikiza na alijeruhiwa vibaya mguuni na watu wasiojulikana na akakimbizwa Hospitali ya Marie Stopes, lakini sitaeleza chochote zaidi ya hayo. Mtafuteni yeye awaelezee zaidi,” alisema Jerry.
Dk. Paul alipopigiwa simu alithibitisha kuumizwa mguuni na kitu anachoamini kuwa ni risasi na watu ambao hawajui.
Akisimulia mkasa huo, Dk. Paul alisema alikwenda katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kumsindikiza Jerry anayekabiliwa na kesi ya kuomba rushwa na mara baada ya shauri kuahirishwa walitoka nje ya Mahakama.
“Tulitoka nje ya mahakama na nikiwa karibu na barabara ya lami gari moja lenye tinted rangi ya silver (fedha) lilipita kwa kasi na nikashitukia mlio wa chini pyuu, nikasikia mguu una ganzi na nilipoangalia nikakuta unavuja damu,” alisema Dk. Paul.
Alisema anaamini kitu hicho kilichomuumiza ni risasi kwa sababu kilitoboa hadi kiatu chake na kumjeruhi vibaya mguu wake, hali iliyosababisha avuje damu nyingi.
“Nilipata mshituko mkubwa ndipo ndugu na jamaa zangu wakanisaidia kunikimbiza Hospitali ya Marie Stopes ambako nilishonwa jeraha,” alisema Dk. Paul.
Hata hivyo, alipodadisiwa zaidi alisema ana mashaka na baadhi ya wafanyakazi wa taasisi moja (jina tunahifadhi) kuhusika na njama hiyo ya kutaka kummaliza kutokana na kuhitilafiana, japokuwa inawezekana pia Jerry ikawa alikusudiwa.
Alisema tukio hilo alikuwa hajaliripoti polisi kutokana na hofu kubwa aliyoipata iliyomfanya achanganyikiwe lakini akasema alikuwa akimsubiri Jerry ili washauriane.
You Are Here: Home - - Jerry Muro akoswakoswa kuchapwa risasi
0 comments