Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Pinda ataka majina ya viongozi wanaojishughulisha na siasa

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WAZIRI Mkuu, Mizengo Pinda, ametaka kupelekewa majina ya viongozi wanaojihusisha na siasa, ili waweze kuchukuliwa hatua zaidi kama ilivyofanywa kwa Profesa Baregu.
Pinda alitoa kauli hiyo jana bungeni wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu, Susan Lyimo (CHADEMA), aliyetaka kujua kama viongozi wa siasa wanaruhusiwa kuwa viongozi wa umma.
Susan alitaka kujua hatua ya serikali kuwa na kauli mbili za kukinzana zilizotolewa na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Profesa Jumanne Maghembe, na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Hawa Gasia, kuhusu kusitishwa kwa ajira ya Profesa Baregu.
Katika kauli yake Maghembe alisema Profesa Baregu hakuondolewa kwa sababu ya kuwa kiongozi wa CHADEMA, kwani wapo viongozi wengine walioko katika vyama wakati huohuo ni watumishi wa umma wakati Ghasia alisema Baregu aliondolewa kwa sababu za kujihusisha na siasa.
Pinda alisema maamuzi yaliyofanywa na mwajiri kusitisha ajira ya Profesa Baregu ni sahihi, kwani unazingatia waraka wa utumishi wa umma.
“Sidhani kama Mheshimiwa Susan uliusoma waraka wa utumishi wa umma… yapo mambo mawili mojawapo ni mamlaka ya mwajiri kumwondoa mtu aliye kazini kwa mkataba na jambo jingine ni ukiwa mtumishi wa umma hutakiwi kujihusisha na masuala ya kisiasa eneo hili la pili linagusa pia mtumishi yeyote.
“Kwa Baregu kwa upande mmoja yuko katika mkataba tena alikuwa nao akaongeza,” alisema Pinda.
Aliongeza hata kama asingekuwa si mtumishi wa mkataba naye pia angechukuliwa hatua ya namna hiyo kama tungekuwa na ushahidi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema hakuna utata ndani ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi kuhusu ufutwaji wa ada za mitihani kwa kidato cha pili, nne na sita.
Pinda alisema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa, aliyetaka kujua ukweli kuhusu ufutwaji wa ada hizo za mitihani, kwani baada ya Waziri Maghembe kutangaza kauli hiyo siku chache baadaye Ofisa Habari wa Wizara ya Elimu alitangaza kuwa ada kwa wanafunzi hao ziko pale pale.
Akijibu swali hilo Waziri Mkuu, alichosema Profesa Maghembe ni kwamba utaratibu huo wa wanafunzi kufutiwa ada za mitihani utaanza kutumika katika bajeti ya mwaka 2010/2011.
Alisema utaratibu mzima wa malipo kuhusu fedha za mitihani utaingizwa katika fedha ambazo zitalipwa na serikali katika bajeti inayokuja.
Alisema hata hivyo suala hilo linaweza kutazamwa kwa kesi nyingine hasa kwa wanafunzi ambao wazazi wao hawana uwezo.
Kuhusu swali la nyongeza la Dk. Slaa aliuliza kwamba lini serikali itatoa waraka kwa halmashauri zote ili kujiandaa na zoezi hilo Pinda alimtaka Slaa kuvuta subira.
‘Mheshimiwa Naibu Spika mi’ naona mwenzangu mheshimiwa Slaa ana haraka na hilo sidhani kama kuna utata kuhusu suala hilo, alichosema Waziri Maghembe ni kwamba utaratibu huu utaanza kutumika katika bajeti ijayo inayokuja,” alisema Pinda.
Tags:

0 comments

Post a Comment