IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
SIKU moja baada ya Bunge kutangaza kuufunga rasmi mjadala wa kampuni tata ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond Development Company Limited LLC, wadau mbalimbali hapa nchini wamepinga hatua hiyo kwa madai inalea ufisadi pamoja na kuilinda serikali.
Mhadhiri mwandamizi wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Senkondo Mvungi, amesema mjadala huo ambao kwa muda wa miaka miwili umekuwa ukitikisa nchi hauwezi kufungwa kienyeji kama lilivyofanya Bunge.
Dk. Mvungi alisema Bunge halina ubavu wa kufunika au kuufunga mjadala wa Richmond wakati watuhumiwa hawajachukuliwa hatua za kinidhamu na kisheria kama maazimio ya Bunge yalivyokuwa yakitaka.
“Kuibuka upya kwa suala hili hakuzuiliki, mjadala wa Richmond ni hadi kieleweke. Anayesema tunavunja katiba atupeleke mahakamani kwani hili suala halikuwa mali ya Bunge bali ni haki ya Watanzania wote kulijadili na kuhoji pale ambapo mambo yanafichwa. Bunge lisijione kuwa lina mamlaka juu ya kila kitu,” alisema Dk. Mvungi.
Alisema kama kuna utapeli umefanywa na serikali kulimaliza suala hilo kabla ya uchaguzi mkuu wa mwaka huu, utagundulika.
“Kuna Mungu katika dunia hii, hakuna mtu katika nchi hii anayeweza kulifunga suala muhimu linalogusa maisha ya watu hivi hivi na likaisha. Na ijulikane kuwa binadamu hana uwezo wa kufunga kitu hapa duniani akakifunga na mbinguni, kwahiyo ukweli utajulikana tu,” aliongeza.
Dk. Mvungi ambaye ni mtaalamu wa masuala ya katiba, alisema kuwa hadi sasa haieleweki Bunge limehitimisha ripoti ipi kwa sababu hakuna uwazi tena kuanzia serikalini hadi bungeni.
Alisema serikali inatakiwa kuwaeleza Watanzania kama imetekeleza maazimio yapi, na ieleze maazimio yaliyopelekwa katika kamati za kisekta za Bunge ni yapi halafu takwimu zitumike kutoa maelezo.
Aidha, alisema ameshangazwa na kauli za Waziri Mkuu Mizengo Pinda, kuwataka waliojiuzulu nyadhifa zao kutokana na kashfa ya Richmond wasihofu ipo siku watarejea katika utumishi wa umma, inaonyesha kuwa serikali inalinda wanaofanya ufisadi na iliumia kwa mawaziri wake kuhusishwa na kashfa hiyo.
“Waziri Mkuu hajui anachokisema, hawa watu wametuhumiwa kwa rushwa, yeye anawaombea kwa Mungu warudi serikalini, Mungu siyo wa hivyo. Watu wanacheza na nafasi ya Mungu katika dunia,” alisema Dk. Mvungi.
Naye Mwenyekiti cha Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Freeman Mbowe alisema Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambacho ndicho kinashikilia dola na idadi kubwa ya wabunge hakina uwezo wa kuwajibishana.
Alisema kuwa CCM ni wadau wa ufisadi ambao hutumia fursa ya vyombo vya habari kuonyesha kuwa wanapambana na ufisadi wakati hawana dhamira ya kufanya hivyo.
“Richmond imezungumzwa kwa miaka mitatu, lakini serikali imefanya kila linalowezekana kuhakikisha suala hili linacheleweshwa ili watafutiane muda wasuhulishane ndani kwa ndani…tukisema CCM chama cha mafisadi sioni sababu ya watu kutoamini,” alisema Mbowe.
Alisema kuwa kilichofanyika bungeni wakati wa kufunga mjadala wa Richmond ni mchezo wa kuigiza kwani CCM pamoja na serikali wameonyesha wazi kuwa dhamira ya kupambana na ufisadi haipo.
“Serikali ni dhaifu, rais ni dhaifu. Selelii, Sitta, Mwakyembe lao moja, hakuna kitu pale bungeni, ni ‘Talk Show’… na sasa Watanzania wanapaswa kuamka wasitegemee mabadiliko kutoka CCM, wafute mawazo yao, huko ni kupoteza muda, CCM haiwezi kuwasaidia… sasa hivi tunapokwenda kwenye uchaguzi sidhani kama kuna wabunge wa CCM watakaopambana na ufisadi mpaka tone la damu.
“La msingi hapa tunataka wabunge wengi wa upinzani bungeni, hapo tutaona tunapambana na ufisadi kuliko ilivyo hivi sasa ambapo wabunge wengi ni wa CCM, hivyo si rahisi kufichua ufisadi wao,” alisema Mbowe.
Aidha alisisitiza kuwa ufisadi ambao vyama vya upinzani vimekuwa vikiupinga si Richmond peke yake.
“…Kuna Kiwira, kwenye halmashauri na mambo mengine ambayo serikali haijaonyesha dhamira ya dhati ya kupambana na ufisadi huo,” alisema.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba, alisema uamuzi huo wa Bunge ni wa kushangaza na usiopaswa kuzungumzwa mbele ya wapenda maendeleo.
Lipumba alisema amebaki njia panda hasa kwa kutojua maamuzi yaliyofikiwa na chombo hicho cha kutunga sera na sheria licha ya Spika wa Bunge, Samuel Sitta juzi kutangaza kwamba mjadala huo umefungwa.
“Nashindwa kujua mjadala wa Richmond umefungwa vipi wala maamuzi yaliyochukuliwa dhidi yake. Nchi ilipata hasara kubwa sana,” mwanasiasa huyo aliliambia gazeti hili.
Aliongeza kwamba kinachosikitisha zaidi ni kwamba hata pamoja na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) kuisafisha Richmond, hakuna hatua zilizochukuliwa hadi sasa, jambo linaloongeza shaka kwa hatua ya Spika Sitta kulitangazia Bunge kuwa mjadala huo umefungwa.
Profesa Lipumba alisema hoja ya Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz ya kutaka taratibu za kisheria zitumike kuchunguza sakata hilo la Richmond bora ungezingatiwa walau kuona iwapo mchakato huo ulihusiana na makosa ya jinai.
Mwenyekiti wa Chama cha Tanzania Labour (TLP), Augustine Mrema, alisema yeye amefurahishwa na hatua ambayo Bunge limefikia ya kuamua kuachana na suala la Richmond na kulifunga kwani lilikuwa linapoteza muda.
Mrema ambaye siku za hivi karibuni ametangaza kugombea ubunge na kuachana na kugombea urais, alisema suala hilo lilichukua karibia miaka mitatu huku likiteka masikio na akili za watu wakati kuna mambo mengi ya msingi ambayo wabunge wanapaswa kuyajadili kwa ajili ya maslahi ya nchi.
“Nimefurahia sana na hatua iliyofikiwa, wabunge wamezingatia maslahi ya taifa. Jambo moja la Richmond liliteka akili za Watanzania kwa zaidi ya miaka mitatu, tuna mambo mengi ya kujadiliana juu ya mustakabali wa nchi yetu, hasa kwa kipindi hiki, ” alisema Mrema.
Sakata la Richmond lilianza baada ya kuundwa kwa kamati teule ya Bunge kuchunguza na kubaini kama kulikuwepo na mianya ya rushwa ambapo baadaye ilithibika kuwa viongozi wa serikali wakiwemo mawaziri na viongozi waandamizi walihusika.
Februari mwaka juzi kamati hiyo chini ya Mbunge wa Kyela, Dk. Harison Mwakyembe (CCM), iliwasilisha ripoti bungeni na kusababisha kujiuzulu kwa aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa na waliokuwa mawaziri wa Nishati na Madini kwa nyakati tofauti, Nazir Karamagi, na Dk. Ibrahim Msabaha.
You Are Here: Home - - Mhadhiri mwandamizi wa Kitivo cha Sheria Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk. Senkondo Mvungi atikisa Bunge. Baregu cha mtoto
0 comments