|
WAKATI Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi ikitarajiwa kupokea, Jumatano ijayo, taarifa ya Kamati ya Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi inayotafuta njia ya kumaliza msuguano ndani ya chama hicho, mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa chama hicho, Pius Msekwa, ameelezwa kutaka Spika wa Bunge Samuel Sitta achukuliwe hatua, Raia Mwema limefahamishwa.
Habari za ndani ya CCM zimeeleza kwamba Msekwa, ambaye alipoteza nafasi yake ya Uspika baada ya kushindwa na Sitta, amekuwa akionyesha waziwazi kutaka hatua zichukuliwe dhidi ya Sitta na wabunge wanaomuunga mkono katika vita dhidi ya ufisadi.
Hata hivyo, Msekwa amekuwa akipata pingamizi kutoka kwa wajumbe wenzake, akiwamo Mzee Mwinyi, na Spika wa kwanza wa Baraza la Kutunga Sheria la Jumuiya ya Afrika Mashariki, Abdurahaman Kinana.
Wakati Kinana ameelezwa kuwa na msimamo mkali zaidi akitaka pande zote husika zichukuliwe hatua kulingana na uzito wa tuhuma, kwa watuhumiwa wa ufisadi kushughulikiwa kukisafisha chama na Sitta na wenzake kukemewa, Mzee Mwinyi amekuwa akielezwa kutumia busara zaidi kutoa maoni yake.
“Msekwa alisema wazi kwamba matatizo ya sasa yasingekuwapo kama Sitta angechukuliwa hatua na vikao vya CCM vilivyoandaliwa mahususi kumshughulikia, lakini Mzee Mwinyi akamwambia chama hicho tawala hakiendeshwi kwa jazba,” anasema mtoa habari wetu ndani ya CCM.
Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa
Kutokana na msimamo mkali wa Msekwa, imeelezwa kwamba katika kikao kijacho cha NEC kamati hiyo itawasilisha taarifa yake lakini wajumbe wake watakua na nafasi ya kuongeza mambo kwa kuchangia, huku baadhi ya maoni yao yakielezwa kuwa mazito zaidi na yatakayozingatiwa na kuongoza mjadala.
Imeelezwa kwamba kikao kilichoandaliwa mahususi kumng’oa Sitta kiliongozwa na mashambulizi dhidi ya Spika huyo aliyejijengea heshima kubwa kwa jamii kutokana na msimamo wake, lakini yalizimwa na Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ambaye aliwazuia baadhi ya wajumbe kutoa michango iliyoshambulia bila kuwa na hoja za msingi.
Imeelezwa kwamba hata uanzishwaji wa Chama cha Jamii (CCJ) ulitokana na matokeo ya kikao hicho kilichoonyesha kusudio la wazi la kushusha hadhi ya Spika na wabunge waliojitokeza kupambana na ufisadi, kabla ya uongozi wa juu wa CCM na serikali kutuliza hasira za kundi hilo kwa kuonyesha wazi kuliunga mkono.
“Si uliona hata Katibu Mkuu wa CCM, Yussuf Makamba, katika hali ya mshangao alikwenda Urambo nyumbani kwa kina Sitta na kuonyesha kumuunga mkono. Ile ilikuwa ni moja ya hatua za makusudi za kupooza hasira za Sitta na wanaomuunga mkono,” anasema mtoa habari wetu ndani ya CCM..
Habari zinaeleza kwamba tayari kumekuwapo na wasiwasi mkubwa ndani ya kundi la watuhumiwa wa ufisadi, baada ya kubaini kuwapo kwa mabadiliko katika nyendo za baadhi ya viongozi na watendaji wa serikali dhidi yao, tofauti na ilivyokuwa awali.
“Kwa sasa mafisadi wamechanganyikiwa na wamekuwa wakihaha kutafuta mbinu za kujihami na kuvuruga mambo. Kuna wakati wanaelekea kama wanafanikiwa lakini hali si shwari kabisa kwa upande wao. Wanalishwa chambo, wakinasa wamekwisha,” anasema Ofisa mmoja mwandamizi wa serikali aliye karibu na mifumo ya kisiasa.
Hayo yakijiri, CCM bado imekuwa na kiwewe cha kuanzishwa kwa CCJ huku matokeo ya kikao kijacho cha NEC yanaelezwa kuwa msingi mkuu wa kuimarika ama kufa kwa chama hicho kipya kinachohusishwa na vigogo ndani ya CCM.
Samuel Sitta, Spika wa Bunge
Pamoja na kuwapo makundi mengi ndani ya CCM, makundi mawili ndiyo yanayotajwa kuwa chachu ya misuguano ndani ya chama hicho, yakiongozwa na wanasiasa wawili wazito, Sitta na Waziri Mkuu aliyejiuzulu kwa kashfa Edward Lowassa, wanasiasa ambao kwa sasa ndio wanaokiyumbisha chama hicho tawala.
Tayari kulikuwa na maelekezo kutoka kwa Mwenyekiti wa CCM, Rais Kikwete, alishauri kuwapo maridhiano kati ya kundi la Lowassa na Sitta, pendekezo ambalo limekwama kutokana na kila upande kuuamini liko sahihi.
Habari za karibu na Kamati ya Mwinyi zinasema kwamba baada ya kukutana na wahusika wa pande zote mbili, kundi la Lowassa lilielezwa kukubali maridhiano lakini kwa sharti la kuombwa radhi hadharani ikiwamo ndani ya Bunge, pendekezo ambalo lilipingwa vikali na Sitta akibainisha kwamba hakuna “ugomvi binafsi” kati yao bali masuala yanayowagusa Watanzania wote ambao hawajahojiwa na kamati hiyo.
Kiongozi mmoja wa CCM ameliambia Raia Mwema kwamba hoja ya kukisafisha chama imekuwa ikisubiriwa kwa hamu na wajumbe wengi wa NEC ambao wamepokea maoni ya wananchi katika maeneo yao ambao wameelezwa kuchoshwa na matusi kutoka kwa wapinzani kwamba chama chao ni cha mafisadi.
“Nashangaa watu wanashangilia eti mafisadi kutochukuliwa hatua. Hakuna mtu aliyetaja fisadi ni nani na kwamba kama kuna mtu anashangilia wahalifu kutochukuliwa hatua basi huyo hana akili timamu ama amepumbazwa na ufisadi. Ndio maana Dk. Harrison Mwakyembe (Mbunge wa Kyela) alisema kuna ujasiri wa kisiasa,” anasema mjumbe mmoja wa NEC kutoka kanda ya ziwa.
0 comments