IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
HATIMAYE Chama Cha Mapinduzi kimefuata nyayo za Chama cha Demokrasia (CHADEMA) kwa kuanzisha mfumo wa wanachama wake kukichangua kwa njia ya simu za mikononi kwa kukwepa fedha haramu.
Mwaka jana, CHADEMA kilizindua mpango huo wa kuwawezesha wanachama na watu wenye nia nzuri kukichangia fedha na kujisajili kwa kutumia simu zao za viganjani.
Pamoja na njia hiyo ya kisasa, CCM itaandaa harambee ili kuwafanya wanachama wake na watu wenye mapenzi na chama hicho kikongwe barani Afrika kukichangia, lengo likiwa ni kuepuka fedha haramu kwa kuwa zitakiangamiza chama.
Akihutubia katika kilele cha maadhimisho ya miaka 33 ya CCM tangu kuzaliwa kwake katika Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam, jana, Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Jakaya Kikwete, alisema ili kukiepusha chama hicho kuingia katika kesi zinazohusu fedha chafu hasa baada ya uchaguzi, ni lazima michango ifanywe kwa njia ya wazi.
Kauli ya Kikwete inakuja wakati vyama vya upinzani, hususan CHADEMA na CUF, vinakituhumu chama hicho tawala kuwa ushindi kilichoupata mwaka 2005 ulitokana na fedha chafu hasa zile za akaunti ya madeni (EPA).
“Tujiepushe kutafuta fedha kwa gharama yoyote ile, fedha chafu zitatuangamiza. Zitatuletea matatizo baada ya uchaguzi.
“Tumebuni njia ya kisasa ya kukusanya fedha; ni kwa njia ya simu. Wenye mapenzi mema na chama pamoja na wanachama wanaweza kutumia njia hii kukichangia chama,” aliwaambia wanachama waliofurika katika viwanja hivyo.
Kuhusu kuchangisha kwa njia hiyo ya mtandao, alisema maandalizi ya kuanza zoezi hilo yanakaribia kukamilika na kuwataka wanachama wa CCM na wale wanaokitakia mema chama hicho kutumia fursa hiyo ikiwa ni pamoja na kushiriki harambee zinazoandaliwa na chama.
Mbali na hilo, mwenyekiti huyo alimtaka Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makmba, kuwa macho na wanachama ambao wanajitokeza wakati huu taifa linaingia kwenye uchaguzi mkuu hapo Oktoba kwani huenda wana lao jambo.
Alisema misaada hiyo ni haramu na huenda ikakiingiza chama matatani na kupendekeza njia anuai ya kukisaidia chama ni kuanzisha mifuko imara itakayoweza kukifanya kiwe thabiti na kuepuka watu wenye maslahi yao katika kukisaidia chama.
Huku akisisitiza ushindi mwaka huu ni lazima, Kikwete alibainisha kuwa CCM haitaacha mbinu yake ya kutumia mbinu ya ‘nyumba kwa nyumba’, ‘mtu kwa mtu’ hata ikiwezekana ‘chumba kwa chumba’ hata ikiwezekana usiku na mchana ili kuhakikisha kinawashawishi wapiga kura wakichague mwaka huu.
Alisema mbinu nyingine ni kuwapatia mafunzo viongozi wake hasa wa ngazi ya chini ili kuendana na mipango hiyo ya maandalizi pamoja na kuwaorodhesha wananchama wake katika daftari na kuepuka usaliti wakati wa uchaguzi.
Akizungumzia uwiano sawa kati ya wanawake na wanaume bungeni (asilimia 50-50), Kikwete alipendekeza kuwa mwakani kuwepo mjadala wa iwapo kuna uwezekano wa kubadili mfumo kwa kuchagua mgombea wa urais na vyama vyao na si wabunge.
Kikwete aliyeambatana na mkewe, Salma alisema njia hiyo itakifanya chama kipewe fursa ya kuteua wabunge kutokana na wingi wa kura kilichopata za urais na utaratibu ukikibana kitoe jina la mwanaume na wanawake, mfumo unaotumiwa Afrika Kusini.
Aliongeza njia nyingine ni ile ya sasa ambayo Katiba ya nchi inataka idadi ya wabunge wanawake isipungue asilimia 32 bungeni na kuongeza iwapo wanawake wakipata nafasi ya kugombea zaidi majimboni, wanahitaji viti 18 tu ili kutumiza uwiano huo.
Aliponda nyadhifa za viti maalumu kwa kusema kuwa wakati mwingine vinaonekana kuiminya demokrasia kwa kuwanyima watu uhuru wa kuchagua.
Naye Makamba aliendelea kuwadhihaki wale wote walioonyesha kutoridhishwa na utendaji wa Kikwete kwa kusisitiza kuwa ni wehu kutokana na ushauri wao wa kutaka Kikwete atoswe asigombee mwaka huu.
Alisema kura za maoni ya kitaalamu zinaonyesha Kikwete anakubalika kwa asilimia 86 na kukifanya chama hicho kimchukulie kama mtaji mkubwa katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dar es salaam, John Guninita, alisema Kikwete kupitia serikali yake ameweza kutimiza ahadi zake mwaka 2005 na katika maeneo mengine utekelezaji wake umefikia asilimia 500 kama shule na huduma ya afya.
“Halmashauri Kuu ya CCM mkoa tunakutangaza rasmi kwamba wewe ni mgombea pekee wa uchaguzi mwaka huu, 2010. Juhudi zake zinaonekana kwa kushughulikia suala la EPA na Richmond,” Guninita alitangaza na kuungwa mkono na wanachama waliofika katika sherehe hizo.
You Are Here: Home - - Kikwete: Fedha haramu zitaiua CCM
0 comments