IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
MIKOA ya Kanda ya Kaskazini bado inaandamwa na ajali mbaya za barabarani baada ya watu 24, akiwamo dereva wa basi, kufariki dunia papo hapo na wengine zaidi ya 30 kujeruhiwa baada ya mabasi mawili kugongana uso kwa uso katika barabara ya Segera - Chalinze.
Ajali hiyo ilitokea majira ya saa 8:50 mchana katika Kijiji cha Kitumbi kilicho wilayani hapa ikihusisha mabasi ya kampuni ya Mzuri Transport, ambalo lilikuwa likitokea Dar es salaam kuelekea Lushoto na Chatco lililokuwa likitokea Arusha kuelekea Dar es salaam, kwa mujibu wa maofisa wa polisi.
Ajali hiyo ni ya tatu kubwa kwenye barabara hiyo baada ya ajali iliyotokea Same mkoani Kilimanjaro kuua zaidi ya watu 19, ikiwa ni miezi michache baada ya ajali nyingine mbaya kutokea Korogwe ambako watu 28 walipoteza maisha.
Ofisi ya kamanda wa polisi mkoani Tanga ilisema kuwa taarifa kamili ya ajali hiyo ingetolewa baada ya kaimu kamanda wa mkoa, Simon Mgawe mara baada ya kurejea kutoka eneo la ajali.
"Hatujapata taarifa kamili za waliokufa na hata majeruhi kwa kuwa shughuli za kuokoa watu bado zinaendelea, lakini maiti na majeruhi wameshaanza kupelekwa Hospitali ya Wilaya ya Korogwe ya Magunga," alisema mmoja wa polisi ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini kwa kuwa si msemaji.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana baadaye zilieleza kuwa majeruhi walikimbiziwa Hospitali ya Bombo wakiwa wamebebwa pamoja na maiti kwenye lori.
Watu walioshuhudia tukio hilo walisema kuwa chanzo cha ajali hiyo ni dereva wa basi la Chatco ambaye alikuwa akitaka kulipita gari lililokuwa mbele yake na ghafla alikutana uso kwa uso na basi la Mzuri ambalo dereva wake alikufa papo hapo.
Walisema magari yote yalikuwa katika mwendo wa kasi.
"Ni ajali mbaya sana... Chatco lilikuwa linaipita gari iliyokuwa mbele yake, lakini ghalfa ikakutana uso kwa uso na basi la Mzuri ambalo nalo lilikuwa kwenye mwendo kasi katika eneo ambalo lina kona,"alisema Khalid Juma ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Kitumbi.
Ajali hiyo imetokea eneo la umbali wa kilomita tatu kutoka kizuizi cha polisi cha Kitumbi ambacho kipo kitongoji cha Kwangau Pakeni ambako basi basi la Chatco lilikuwa limekaguliwa na polisi.
Naye Hussein Semdoe anaripoti kwamba Mkuu wa wilaya hiyo Seif Mpembenwe alithbitisha kutokea kwa ajali hiyo na kusema kuwa majeruhi wa ajali hiyo walikimbizwa katika Hospitali ya Magunga Korogwe na maiti zimehifadhiwa katika Hospitali ya Teule wilayani Muheza.
Kapteni Mpembenwe alisema kuwa Chatco ilikuwa ikilipita roli lililokuwa limesimama ndipo likagongana na jingine. Sindo Abdallah Sindo 48 aliyekuwa akiendesha gari ya Mzuri alijeruhiwa vibaya miguuni, huku dereva wa Chatco Mambo Mnyamwani 38 kapa jeraha madogo.
Taarifa zaidi zinasema kuwa gari ya Mzuri lilikuwa limeba abiria wengi waliokuwa wakitoka kwenye sherehe ya harusi.
You Are Here: Home - - Ajali mbaya yaua tena watu 24 Tanga, mabasi yagongana uso kwa uso
0 comments