Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, John Tendwa akiteta jambo na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa ya Serikali za Mitaa ( TAMISEMI) , Celina Kombani baada ya kuwasili katika ukumbi wa Bunge Dodoma jana |
Vilevile, uongozi wa CCJ umeweka bayana kwamba umeamua kujitoa mhanga kuhakikisha unasimama mstari wa mbele ili kuwakaribisha Watanzania wenye uwezo wagombee nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwemo ya urais.
"Hatutaki madaraka, kazi yetu kubwa ni kupiga debe watu makini wajitokeze na kujiunga nasi ili tushiriki pamoja katika mpango wetu wa kuleta ustawi wa jamii nchini," alisema katibu mkuu wa CCJ, Renutus Muabhi.
Awali taarifa za kuanzishwa kwa CCJ ziligonga vichwa vya habari vya magazeti mengi, hasa baada ya chama hicho kuhusishwa na baadhi ya vigogo na wabunge wa CCM, ambayo katika kipindi hiki ina migogoro mikubwa Bara na Visiwani.
Lakini Muabhi aliiambia Mwananchi katika mahojianp juzi kuwa lengo la CCJ si kuchochea vurugu wala kuingiza msuguano ndani ya CCM au nchini, bali kufanya mageuzi ya mfumo wa uongozi.
"Kuna kitu kimoja kinatusikitisha sana, ndiyo maana tumeamua kutozungumza na vyombo vya habari... mwisho leo (juzi). Baadhi ya waandishi wanapotosha dhamira yetu," alifafanua.
"Jinsi baadhi wanavyoiandika CCJ utadhani ni chama ambacho kimelenga kuleta vurugu kwa kuichafua CCM... ndiyo lengo ni kumng'oa hadi yeye Rais Kikwete, lakini isiwe kama vile usajili wetu mzima una lengo hilo moja. (Kikwete) anaweza kudhani sisi tumekuwa tukimlenga yeye tu, si vizuri."
Katibu huyo aliongeza kusema:"Hatumlengi mtu fulani, bali tumekuja kutetea maslahi ya taifa na kuomba ridhaa ya umma; CCJ ni chama makini, kinaundwa na watu makini ambao mwisho wa siku Watanzania watashangaa."
Alipoulizwa kuhusu taarifa kuwa mafisadi wanaweza kujipenyeza, alijibu:" Loo! Hiyo itakuwa ni ajabu kweli, hivi sisi tunaweza kukaa na mafisadi kweli?"
Muabhi alifafanua kwamba kamwe mafisadi hawewezi kupata nafasi hata ya kukaribia chama hicho kwa kuwa ni miongoni mwa watu ambao wamekuwa wakisababisha umasikini na uporaji wa rasilimali za taifa.
"Sisi tumekuja kwa ajili ya ustawi wa jamii, tena tuwaruhusu mafisadi, itakuwa jambo la ajabu sana. Watu wanaoruhusiwa kuingia CCJ ni wale ambao ni waadilifu tu, yeyote mwadilifu tutamkaribisha," alisisitiza.
Alisema kuruhusu watu wachafu kujiunga na CCJ ni hatari kwa ustawi wa maisha ya jamii kwa kuwa wamekuwa wakipora utajiri wa Watanzania wakati wengine wako vijijini wanalalia vitanda vya kamba.
"Inasikitisha sana kuona watu wachache wamekuwa matajiri wa kutisha katikati ya umasikini," alisema.
Tayari Msajili wa Vyama vya Siasa, John Tendwa ameshaeleza kuwa uwezekano wa CCJ kushiriki uchaguzi mkuu uliopangwa kufanyika Oktoba 25 ni mdogo kwa kuwa taratibu za usajili wa kudumu zitachukua muda mrefu na hivyo chama hicho kuwa nje ya muda.
Lakini katibu huyo alisema hategemei kuwa CCJ inaweza kuchelewa uchaguzi mkuu.
"Siamini kama Tendwa atafanya hivyo kwa kuwa ni mtu ambaye tunamheshimu sana na tunajua ni mwadilifu," alisema.
"Kama akikataa kukisajili atakuwa amewanyima Watanzania haki yao ya msingi kupata chama mbadala wakati wa uchaguzi, ndiyo maana nasema siamini kama Tendwa anaweza kufanya hivyo, namuamini sana sijui labda abadalike."
Kwa mujibu wa taratibu za usajili wa vyama vya siasa, CCJ sasa itasubiri kupewa usajili wa muda ambao katika kipindi cha miezi sita ijayo utakipa nafasi ya kutafuta wanachama 200 kutoka mikoa 10 au zaidi na baadaye kitaomba usajili wa kudumu.
Wakati kikisubiri usajili wa kudumu, Tendwa na timu yake watalazimika kufanya uhakiki kabla ya kukiruhusu kuingia kwenye ulingo wa kisiasa, ikiwa ni pamoja na kushiriki chaguzi, kitu ambacho msajili alisema hakitawezekana kufanywa katika muda mfupi uliobaki kulingana na kalenda ya uchaguzi mkuu.
Alipoulizwa kuhusu ofisi zao, Muabhi alisema ni vigumu kutaja zilipo ofisi kwa sasa kwani wanasubiri taratibu za kisheria kutoka kwa msajili wa vyama.
Kuhusishwa kwa CCJ na baadhi ya vigogo wa CCM na wabunge wake kumesababisha wadadisi kuhisi kuwa utabiri wa baba wa taifa, Mwalimu Julius Nyerere kuwa upinzani wa kweli utatoka ndani ya CCM, unakaribia kutimia.
Vita dhidi ya ufisadi imekuwa ikionekana kugombanisha wanachama wa CCM na hasa viongozi na wabunge na ilipamba moto baada ya kuibuliwa kwa kashfa ya Richmond iliyosababisha Edward Lowassa kujiuzulu.
Tangu hapo, vikao vya Bunge vimekuwa vikitawaliwa na kurushiana makombora na mwaka jana vita hiyo iliingia ndani ya CCM, ambako watuhumiwa walijibu mapigo kiasi cha kuifanya halmashauri kuu kuunda kamati ya watu wenye busara kutafuta chanzo cha migongano hiyo.
Hata hivyo, mikutano ya kamati hiyo na wabunge iliwasha moto mpya baada ya wanachama kurushiana maneno makali zaidi, kitu ambacho kinafanya wadadisi waone kuwa kundi kundi linaweza kuwa linatafuta mwanya wa kupumulia kuepuka hali mbaya ya hewa iliyo ndani ya CCM.
0 comments