You Are Here: Home - - SIRI NZITO ZA KAWAWA
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Akiongea na Uwazi katika mahojiano maalum, Msaidizi wa karibu (Personal Assistant) wa mzee Kawawa, Venance Mkude, alisema siku Rais Kikwete alipomtembelea marehemu Hospitali ya Muhimbili alitokwa na machozi baada ya kumuona akiwa katika hali mbaya na kuusiwa maneno mazito.
Mzee Kawawa alimwambia Mhe. Rais kuwa amefarijika na ujio wake na kumtaka adumishe umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania na ndiyo ilikuwa kauli yake ya mwisho kwa Rais.
“Nimefarijika na ujio wako nakuomba udumishe umoja na mshikamano miongoni mwa Watanzania,” alisema Kawawa na kumfanya Rais abubujikwe na machozi.
Watafiti wa mambo wamebainisha kuwa kauli hiyo ni siri nzito iliyo moyoni mwa Rais ambayo atatakiwa kuizingatia na kuitekeleza kwa vitendo ili kulinda heshima na usia wa marehemu.
Rais Kikwete baada ya kumpa pole mzee Kawawa aliondoka na kumwacha akihudumiwa na madaktari sita. Kesho yake, Desemba 31 asubuhi, hali yake ilibadilika na Rais Kikwete aliarifiwa hivyo kulazimika kurejea tena hospitali, lakini alimkuta marehemu yu mahututi na hivyo kushindwa kuongea naye hata alipomsemesha.
“Hali hiyo ilimfanya Rais aondoke na kwenda kupumzika katika chumba maalum (VIP) na baada ya dakika chache akaletewa taarifa rasmi kuwa mzee Kawawa kaaga dunia na akahuzunika sana na alionesha mshituko, akaondoka kuelekea Ikulu na baada ya nusu saa maiti ikachukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Lugalo,” alisema Mkude.
Alisema kabla ya mauti, mzee Kawawa alikuwa akijiandaa kwenda Dodoma kwa mapumziko lakini kutokana na kuugua ghafla, aliahirisha safari.
Akizungumza na mwandishi wetu, msaidizi mwingine wa karibu wa mzee Kawawa ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Kata ya Mwananyamala, Rajab Mwilima (pichani ukurasa wa kwanza aliyekaa na marehemu kwenye kitanda), alisema kiongozi huyo aliitaka familia yake kuishi kwa upendo na kupiga vita rushwa.
(Picha zingine katika ukurasa huo, mzee Kawawa anaonekana akielekezwa jinsi ya kutumia laptop na akisaidiwa kunyanyuka na mkewe pamoja na Mwilima).
Aidha, Mwilima alisema kuwa hayati Kawawa siku chache kabla ya kifo chake aliweza kuzungumzia mambo mbalimbali likiwemo suala la upendo ndani ya familia na alikuwa na tabia ya kuiweka pamoja familia yake na kupanga maamuzi ya maendeleo kwa pamoja.
Hivi karibuni kabla ya mauti kumfika, mzee Kawawa aliitaka familia yake kuendelea kuishi kwa upendo, kutokuwa wabinafsi, kutatua matatizo ndani ya jamii bila kujali udini, ubaguzi ama itikadi za kisiasa, na aliwataka kupiga vita rushwa nchini kwa nguvu zote kama alivyokuwa akifanya yeye. Pia alikuwa akiwashauri wawe wavumilivu na wepesi wa kuomba msamaha pale wanapokosea.
Bw. Mwilima alitoa siri nyingine ya hayati huyo kuwa alikuwa akimueleza kuwa katika familia mwanaume anatakiwa awe na msimamo ili waishi kwa amani na upendo bila kubaguana na pale (mwanaume huyo) alipokuwa anataka kufanya maamuzi ya jambo la kimaendeleo ni lazima aishirikishe familia nzima.
KUHUSU CCM
Msaidizi wake huyo alisema kwamba Hayati Kawawa alikuwa akikerwa sana na baadhi ya wanachama kubaguana bila kufuata kanuni za chama na aliwataka watu hao kutatua migogoro kwa kujadiliwa na kamati ya maadili kwani hakupenda siri za CCM zitoke nje.
“Alikuwa akisema ugomvi wa watu wachache ndani ya chama kunawafanya watu wengine waamini kuwa hakuna maelewano ndani ya chama hicho wakati kuna mshikamano wa hali ya juu akitoa mfano wa jinsi CCM inavyoshinda kwa asilimia kubwa katika chaguzi mbalimbali nchini ,” alisema Mwilima.
Aliongeza kuwa Mzee Kawawa alikuwa akiwaasa viongozi wa chama na serikali kila anapokutana nao kwa kuwaambia kuwa mtu ukiwa na nafasi ya juu kimadaraka lazima ukutane na misukosuko na kinachotakiwa ni kuwa mwepesi wa kusamehe pia kuondokana na majivuno ama kulipa kisasi kutokana na wadhifa uliokuwa nao.
VYAMA VYA UPINZANI
Mwilima alisema siri nyingine ni kuwa Hayati Kawawa hakupenda vyama vingine vya kisiasa nchini vibaguliwe ama kunyanyaswa bali alitaka upendo udumishwe na maamuzi ya pamoja ya mambo mbalimbali ya kitaifa yafanyike, na alipenda kuona migogoro inamalizwa kwa njia ya mazungumzo na siyo kwa kumwaga damu.
Aidha, alimnukuu hayati Kawawa akisema, “Kusiwe na uongozi wa chuki bali upendo utawale ili nchi iendelee katika misingi ya utawala bora,” alisema kauli hiyo alikuwa akiitoa mara kwa mara anapokutana na viongozi na kuwataka kutohodhi mali huku wananchi wakiwa katika umasikini mkubwa.
Bw. Mwilima alisema hayati Kawawa ambaye pia alijulikana kwa jina la Simba wa Vita alikuwa na tabia ya kuwataka wazee kuwa na tabia ya kung’atuka katika uongozi kwa hiari yao na kuwaachia vijana na siyo kungoja kung’olewa madarakani kwa nguvu, badala yake alitaka wazee wawe ni walezi na mhimili wa kupambana na rushwa kwa maelezo kuwa wanaotoa na kupokea mlungula wote ni watuhumiwa.
WASIA KWA VITA KAWAWA
Naye mtoto wa pili wa hayati Kawawa, Vita Kawawa, alipozungumza na gazeti hili siku ya mazishi ya baba yake alisema kuwa mzazi wake alimuachia maneno mazito kabla ya kifo chake.
Vita ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Namtumbo, Songea, alisema kuwa kabla ya baba yake kufariki dunia alimuasa kwamba ahakikishe anaendelea kuishi katika maadili mema na kuiongoza familia yake ili afike mbali katika harakati zake za kisiasa.
“Mara nyingi baba alikuwa akinisisitiza kwamba nihakikishe naitumikia nchi yangu vyema bila upendeleo wowote na niishi katika maadili mema ili kufanikisha harakati zangu za kisiasa.
“Hata kabla ya kifo chake, nilikuwa sijui kwamba Mungu atamchukua mapema, alinisisitiza mno kulinda heshima aliyoiacha yeye katika jamii na kuhakikisha kwamba akifariki hakuna mgogoro wowote utakaotokea katika familia yetu,” alisema Vita.
Aidha, Vita alisema kuwa kutokana na wasia huo mzito wa baba yake katika kipindi chake chote cha kisiasa atahakikisha kwamba anafuata nyayo za mzazi wake kulitumikia taifa na wananchi waliomchagua kuwa Mbunge wao kwa ajili ya kulinda heshima yake.
“Kwa kweli baba alikuwa na heshima kubwa katika jamii na iwapo mimi nitashindwa kuliendeleza hili litakuwa jambo baya kwangu, hivyo siwezi kwenda kinyume na maagizo ya baba,” alisema Vita.
Mzee Kawawa ambaye alikuwa mmoja wa wapigania uhuru wa nchi hii kwa kushirikiana na Baba wa Taifa, Mwl. Julius Nyerere na wazee wengine, alifariki dunia Desemba 31, mwaka jana katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa ugonjwa wa kisukari na figo na kuzikwa Januari mbili kijijini Madale, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.
0 comments