MARIDHIANO ya Rais Amani Karume na Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF), Seif Shariff Hamad yamewachanganya wana Chama Cha Mapinduzi (CCM), na hasa wa Zanzibar, wanaoona kuwa ni mbinu ama ya kuendeleza utawala wa Karume au kumlinda kama ikilazimu Seif ndiye akawa mkuu wa nchi, Raia Mwema imeambiwa.
Tayari vigogo kadhaa wa CCM Zanzibar wameanza kuamini kuwa maridhiano hayo yanaweza kuhitimishwa kwa Rais Karume, kuwania tena urais wa Zanzibar, baada ya Katiba ya Visiwa hivyo kufanyiwa mabadiliko mahsusi.
Aidha, vigogo hao ambao wengine wangetamani kumrithi Karume, wanayatazama maridhiano hayo kwa hadhari kubwa, wakiamini kuwa yanakwenda kinyume cha maelekezo ya mkutano wa Halmashauri Kuu (NEC) iliyokutana kijijini Butiama, mwishoni mwa mwaka jana.
Katika kikao hicho cha NEC iliazimiwa kuwa Serikali ya mseto iundwe baada ya kufanyika kwa kura ya maoni Zanzibar (referendum), ambayo yatakuwa chanzo cha mabadiliko ya Katiba ya Zanzibar.
Hata hivyo, baada ya kikao hicho CUF walipinga wakisema hapakuwa na haja ya kura za maoni na kwamba mabadiliko ya Katiba yamekuwa yakifanyika kila inapobidi kwa kuzingatia hali halisi na mahitaji ya nchi kwa wakati husika.
Kutokana na msuguano huo, CUF walikataa kuendelea na mazungumzo ya muafaka wakitaka utekelezaji lakini CCM, akiwamo Rais Jakaya Kikwete walitoa wito wakitaka warejee kwenye meza ya mazungumzo.
Lakini upepo umegeuka wiki kadhaa zilizopita, baada ya Rais Karume na Seif kukutana katika kikao kisicho rasmi lakini kilichoonekana kuwa na nguvu kuliko hata vikao vilivyokuwa na nguvu za kisheria.
Katika kikao hicho kulifikiwa maridhiano ambayo matokeo yake ni pamoja na CUF kutambua urais wa Karume, na yeye kuwateua baadhi ya viongozi wa CUF kuwa wajumbe wa Baraza la Wawakilishi, akiwamo Juma Duni Haji.
Wakati hayo yote yakitokea mtafaruku umeibuka CCM Zanzibar, Karume na Seif wakitajwa kuwa na ajenda zenye malengo ya kuwanufaisha kama timu mpya ya watu wawili, iliyolenga kubeba siasa za Visiwa hivyo.
Wao wenyewe wamekuwa wakinukuliwa kusema kwamba kwa hali ya siasa zilivyo tete Zanzibar wanaona kwamba bila hatua kama hii uchaguzi wa mwakani unaweza kuzua machafuko makubwa ambayo yataweza kusababisha hata damu kumwagika.
Kwa hali hiyo wamedai kwamba wao kama viongozi hawawezi kuruhusu hayo yatokee na hivyo wameingia katika maridhiano kuepuka wao kama watu binafsi kushitakiwa baadaye katika Mahakama ya Kimataifa ya The Hague, Uholanzi kwa kusababisha maafa.
0 comments