MWENYEKITI wa Chama Cha Wananchi (CUF) Prof Ibrahim Lipumba amesema atatangaza iwapo atagombea nafasi ya urais au la wakati utakapofika.
Lipumba alitoa kauli hiyo juzi alipohojiwa na kituo cha Televisheni ya Taifa (TBC 1) kuhusiana na uchaguzi mkuu wa Rais, Wabunge na Madiwani, unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
"Chama kama chama kitatoa mgombea wake, lakini kwa sasa siwezi kusema ni nani atakuwa mgombea kupitia CUF, kwa sababu bado wanachama hawajajitokeza kuchukua fomu," alisema Lipumba.
Lipumba alisema kwa sasa CUF inaruhusu kila mwenye nia ya kugombea nafasi hiyo kuchukua fomu ya kugombea nafasi hiyo.
"Muda wa kuchukua fomu ndio huu, kila anayejisika na kuona anafaa kugombea nafasi ya urais anaruhusiwa, lakini iwapo ametimiza miaka 40 na kuendelea,"aliongeza Lipumba.
Akijibu swali lililotaka kujua uhusiano wa CUF na chama tawala(CCM), Lipumba alisema kuwa uhusiano kati chama chake na CCM utaendelea kuimarika kutokana na mshikamano ulipo sasa kwa sababu hata rais Kikwete ameukubali.
Katika miezi ya mwishoni mwa mwaka 2009, Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Abeid Amani Karume amekuwa na mazungumzo na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad wakiwa na lengo la kutafuta maridhiano ya kisiasa ambapo tayari ameteua wanaCUF wawili kuwa wajumbe katika baraza la wawakilishi.
0 comments