Samaki wa Magufuli wageuka kitoweo cha Krismasi Dar |
Na Festo Polea BAADA ya kutokea kwa mapingamizi mbalimbali za kuzuia tani 296.32 za samaki waliokamatwa kutokana na kuvuliwa kwa njia haramu katika fukwe za bahari eneo la Tanzania maarufu kama ‘Samaki wa Magufuli’ leo zimegeuka kuwa kitoweo cha sikukuu ya Christmas baada ya kugaiwa jana kwa baadhi ya taasisi ambazo hata hivyo zilionekana kususua kuchukua samaki hao kutokana na kukosa vifaa vya kubebea. Zoezi la ugawaji wa kitoweo hicho lililoanza kwa kusuasua huku walengwa wakionekana kutokujua kilichokuwa kikiendelea eneo la ugawaji kjwani walionekana wakirandaranda huku na huko bila kuwa na magari ya kubebea samaki hao. Zoezi hilo lilianza jana mchana katika kiwanda cha kuhifadhia samaki cha Bahari Foods kilichopo Mwenge jijini Dar es salaam ambapo Tani 26 ndizo zilitarajiwa kugaiwa na wawakilishi wa vituo vya kulelea watoto yatima ndiyo walioonekana kuchangamkia kwa haraka haraka kuchukua samaki hao huku wengine wakiwemo jeshi la polisi wakibaki kutafuta magari na vifaa vya kubebea samaki hao. Ugawaji wa samaki hao ulipangwa kwa Jeshi la Wananchi Tanzania kupata tani 10, Jeshi la Magereza kupata tani tatu, Tani mbili kwa Jeshi la Polisi na tani moja kwa Chuo cha Uvuvi Mbegani. Taasisi nyingine zilizopangwa kupata samaki hao jana ni Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH) ambayo ilitakiwa kupata tani tatu, Vituo vya kulelea watoto yatima tani sita, Chuo Kikuu cha Dar es salaam tani moja na nusu tani kwa Chuo cha Utalii, ambapo hata hivyo baadhi ya taasisi ziliomba hudhuru ya kutochukua samaki hao jana hadi kesho kwa kuwa hawakuwa na vifaa vya kubebea samaki hao. Kabla ya ugawaji huo wa jana taasisi mbalimbali za uma na serikali 115 zilizopita katika mchujo wa kuomba samaki hao baada ya Serikali kuamua kuwagawa bure samaki hao kutokana na agizo la mahakama la Oktoba 5 mwaka huu na la Oktoba 20, iliyoitaka serikali kuwauza samaki hao au kugawa kwa wananchi wake bure kwa zilikwama kutokana na kutokea kwa vipingamizi vingine vilivyozua sababu mbalimbali zikiwemo za kutokuwa na vifaa. Akizungumza na waandishi wa habari jana kabla ya zoezi la ugawaji wa samaki hao kufanyika, Waziri wa Uvuvi na Maendeleo ya Mifugo, John Magufuli alisema samaki hao wapo katika hali nzuri ya kuliwa kama wananchi watazingatia hali ya afya katika kuwabeba kwenda kwenye maeneo yao. Magufuli alisema thibitisho la ubora wa samaki hao limetolewa na wataalamu kutoka maabara ya Nyegezi na pia Mkemia Mkuu alishirikishwa katika kuwapima samaki hao naye ametoa taarifa kuwa wanafaa kuliwa kwa afya za wanadamu bila madhara yoyote. “Samaki hao tunaoanza kuwagawa leo (jana) wamethibitishwa kuwa na ubora kwa afya za walaji kutoka kwa mkemia mkuu na ripoti kutoka maabara yetu ya Nyegezi, pia wamehifadhiwa kwa ubora wa hali ya juu na kiwango cha kimataifa cha nyuzi joto (-20). Katika hatua nyingine Magufuli alisema samaki hao huhifadhi wa samaki hao hadi jana Sh 1.2 bilioni ndizo zimetumika kwa ajili ya uhifadhi wa samaki hao na kufafanua kuwa kwa siku hutumika Sh 3.5milioni, fedha ambazo hata hivyo alisema hazijalipwa zote kwa wamiliki wa kiwanda hicho. “Serikali imegharamia kiasi hicho cha fedha hadi sasa na bado fedha hizo hatujalipa zote, zimelipwa nusu na zilizobaki zitalipwa baada ya zoezi la ugawaji wa samaki hao kukamilika,’’ alisema Magufuli huku akidai kutojali muda wa kumaliza zoezi hilo kwa kuwa kinachotakiwa ni kufanikiwa kwa zoezi hilo. Akizungumzia wizi uliokuwa ukifanyika katika bahari ya hindi kwa muda wa miaka 48 waziri Magufuli alisema ulitokana na kutokuwa na sheria za kuwabana wavuvi haramu hivyo kwa kupitia sheria mpya ya uvuvi ya namba ya namba 17 ya mwaka 2007 ambayo regulation yake ni ya mwaka 2009 zitasaidia kukomesha kabisa uvuvi haramu na kuifanya nchi kunufaika na eneo lake la bahari. “Kwa miaka 48 tumeibiwa samaki wetu na hivi karibuni ndiyo tumeshika maujizi ya samaki wetu, hapo awali kwa miaka hiyo yote tumeibiwa zaidia ya trilioni kadhaa lakini leo tumewashika tumetumia 1.2bilioni za uhifadhi kwetu siyo hasara ni jambo la kujipongeza kwa kuwa tutanufaika nalo baadae,’’ alisema Magufuli kwa msisistizo. Hata hivyo Magufuli aliongeza kuwa kitendo cha serikali kuwashikilia samaki hao kimeipa Tanzania heshima mbele ya mataifa mengine makubwa na januari serikali inatarajia kusaini mikataba ya uvuvi salama katika bahari ya hindi eneo la Tanzania ambapo nchi itaanza kunufaika na bahari hiyo. Pia Magufuli aliwataka wananchi wote kuwa walinzi kwa wale watakaogeuza samaki hao kuwa biashara kwa kutao taarifa zao ili waweze kushitakiwa mahakamani kwa kukiuka sheria. Wakati taasisi mbalimbali zikinufaika na samaki hao leo katika sherehe ya Christmas raia 37 ambao ni wa mataifa ya China, Vietnam, Indonesia, Filipino na Kenya waliokamatwa wakivua samaki hao kinyume na utaratibu hadi sasa wako rumande wakisubiri hatma ya kesi yao baada ya kunyimwa dhamana. |
You Are Here: Home - - Samaki wa magufulu waliwa siku ya Christmas
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments