MBUNGE wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe ameibuka tena na kusisitiza uamuzi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, (Takukuru) kuhoji wabunge ni mkono wa mafisadi.
Madai ya Dk Mwakyembe yanakuja wakati mjadala wa kutaka wabunge wa Jamhuri kuhojiwa kwa madai ya kupokea posho mbili ukiwa umeanza kupoa.
Dk Mwakyembe alitoa tuhuma hizo kwenye Kongamano la Maadili lililofanyika katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam jana.
Alisema kuwa mpango huo unafadhiliwa na mafisadi ambao wanataka kuwavuruga wabunge ili wasiwe na umoja wa kuwabana kutokana na tuhuma mbalimbali za kupora mali za nchi zinazowakabili.
"Kitendo hicho hakipo katika nchi yoyote ile duniani, huo ni mpango wa kifisadi wenye lengo la kudhoofisha mapambano ya ufisadi," alisema Mwakyembe ambaye ni mmoja wa wabunge waliopo mstari wa mbele kupambana na ufisadi nchini.
Aliongeza kuwa katika taaluma yake ya sheria aliyosoma kwa msaada wa fedha za walipa kodi, hajawahi kuona wabunge wakihojiwa kwa kuchukua posho mbili.
"Mimi ni mwanasheria niliyebobea na niliyefundishwa kwa fedha za wananchi wa Tanzania enzi za Mwalimu Julius Nyerere, sijawahi kuona wabunge wakihojiwa kwa kuchukua posho mbili," alisisitiza mbunge huyo.
Akihojiwa na kituo cha Televisheni cha TBC, baada ya kongamano hilo kama Takukuru imesha mhoji kwa madai hayo ya kupokea posho mara mbili, Dk Mwakyemba hakukubali wala kukataa badala yake alisema anayetaka kujua awaulize Takukuru wenyewe.
"Kuhojiwa wala si 'issue' kubwa, kama mtu anataka majibu sahihi yako Takukuru kwenyewe,"alisema.
Mwakyembe ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kamati ya Bunge ambayo ilichunguza kashfa ya Richmond, na kumsababisha waziri mkuu , Edward Lowassa na mawaziri wengine wawili kujiuzulu, alishawahi kuweka wazi msimamo wake kuwa hayuko tayari kuhojiwa na taasisi hiyo kuhusiana suala hilo.
Mbunge huyo pamoja na wabunge kadhaa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wakiwamo, Mbunge wa Same mashariki, Anne Kilango, Mbunge wa Vunjo, Aloyce Kimaro, Mbunge wa Kishapu, Fred Mpendazoe, Mbunge wa Nzega, Lucas Selelii na Mbunge wa Kahama , James Lembeli wamejitoa mhanga kupambana na vitendo vya ufisadi.
Hata hivyo, mara kwa mara wamekuwa wakilalamika kuwa kuna njama za kuwahujumu katika majimbo yao ili wasirejee katika uchaguzi mkuu ujao.
Habari hii imeandaliwa na sadick Mtulya na Claud Mshana
0 comments