Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Chadema yatembeza Sangara kwa helkopta za Ndesamburo

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo(CHADEMA), jana kimezindua kampeni ya Operesheni Sangara mkoani Tanga kwa mara ya kwaza kwa kutumia helkopta mpya ya mwenyekiti wa chama hicho mkoa wa Kilimanjaro , Phelemon Ndesamburo.

Helkopta hiyo, iliwasili katika Uwanja wa Tangamano majira ya saa 10:30 ikiwa na Mwenyekiti wa CHADEMA, Freeman Mbowe na viongozi wengine wa chama hicho, ambapo jana pia chama hicho, kilizindua kuanza kuchangia chama hicho kwa kupitia ujumbe wa simu za mikononi.

Akizungumza katika mkutano huo wa hadhara, alisema uzinduzi wa operesheni Sangara Tanga unalenga kuimarisha nguvu za vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu ujao.

"Naomba wanachama wa vyama vyote vya upinzani tushirikiane, hapa hatukuja kuvunja nguvu ya CUF bali tumekuja kushirikiana na wanaCUF katika vita ya mageuzi, hivyo sote tuwe kitu kimoja,"alisema Mbowe.

Mbowe pia alieleza Chadema kupinga kesi aliyofunguliwa mbunge wa CUF, Nuru Bafadhili kwa tuhuma za kumkashifu Rais Jakaya Kikwete kwa kusema amekuwa akichekacheka na mafisadi.

"Naomba mumpelekee ujumbe mkuu wa mkoa wa Tanga, kuwa hatuwezi kujadili mustakabali wa nchi hii bila kumtaja Kikwete na CCM yake kwani kutokumtaja Kikwete ni sawa na mchungaji au sheikh kuendesha mahubiri bila ya kumtaja Mtume Muhammad na Koran au Yesu Kristo na Biblia,"alisema Mbowe.

Katika mkutano huo, Mbowe alizindua uchangiaji chama hicho na jinsi ya kujiunga kwa kutumia simu ya mkononi kwa kutuma neno Chadema kwenda namba 15710.

Mpango huu una lengo la kukusanya fedha kwa ajili ya kuendesha chama na pia kupata wanachama wengi zaidi kwa njia ya kisasa na gharama ya kutuma ujumbe huo ni shillingi 350 tu.

Mkurugenzi wa Mambo ya Nje wa Chadema, John Mnyika akizungumza katika mkutano huo, aliwataka vijana wa mkoani Tanga kuingia katika siasa na kugombea nafasi mbalimbali ndani ya chadema kwani ndicho chama cha kizazi kipya.

Mnyika alisema umaskini uliokithiri mkoani Tanga umetokana na serikali kuutekeleza mkoa huo ambao awali ulikuwa ukisifika kwa kuwa na viwanda vingi, bandari ya kisasa na huduma nzuri za usafiri wa reli.

"Nafurahi hapa nimekuta watu wengi waliopo kwenye mkutano ni vijana hivyo naamini kabisa ninachosema mtakielewa kwani pia mimi nilizaliwa hapaĆ¢€¦hali ya maisha Tanga ni ngumu na lazima vijana tusimame na kubadili hali hii,"alisema Mnyika.

Naye Wilfred Rwakatare alisema ameamua kujiondoa CUF na kujiunga na Chadema, si kwa kufuata uongozi au ubunge bali ameamua kuungana na Chadema kwani kuna wapiganaji wa dhati wa vita ya kuwakomboa Watanzania.

"Mimi niliwahi kushika nyadhifa mbalimbali za kisiasa hapa nchini, lakini kimoja kilichonifurahisha na Chadema ni siku viongozi wake walipokutana katika viwanja vya Mwembechai na kutangaza orodha za mafisadi bila kificho na hizo ndizo siasa ninazozitaka mimi,"alisema Rwakatare.

Chadema imezindua mikutano ya Operesheni Sangara mkoani hapa na itafanyika katika kipindi cha siku 10 kutembelea zaidi ya kata168 na Wilaya zote za Mkoa wa Tanga.

Tags:

0 comments

Post a Comment