Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Msajili wa vyama vya ataka mpango wa mgombea binafsi uanze mwakani

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter

Msajili wa vyama vya siasa Tanzania, John Tendwa, anashauri mpango wa mgombea binafsi uanzishe haraka kupunguza migogoro ya uongozi.
Na Elizabeth Suleyman

MSAJILI wa vyama vya siasa nchini, John Tendwa ameitaka serikali na asasi zisizo za kiserikali kuanza mchakato wa kuwa na wagombea binafsi katika chaguzi ili kuwapa wananchi fursa ya kuchagua viongozi wanaowajibika na ambao hawafungamani na vyama vya siasa.

Akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Haki za Binadamu iliyoandaliwa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam jana, Tendwa alisema mchakato huo unafaa kuanza sasa ili ikiwezekana suala hilo lianze kutekelezwa mwakani.

Kwa mujibu wa Tendwa mgombea binafsi ana fursa nzuri zaidi kutekeleza majukumu yake bila fujo wala mikanganyiko katika ulingo wa siasa.

"Naamini pia kuwa suala la mgombea binafsi litaongeza uwajibikaji ndani ya vyama vya siasa na litatoa fursa kwa viongozi mbalimbali kuwajibika bila kushurutishwa," alisema Tendwa.

Alifafanua kuwa takwimu zimeonyesha kuwa Watanzania wengi si wafuasi wa vyama vya siasa, hivyo kumekuwa na joto la watu kutaka kujua namna raia hao wanavyoweza kupata fursa ya uongozi katika jamii.

"Suala la mgombea binafsi sio zawadi kwa raia bali ni haki ya msingi ya raia itakayowawezesha kushiriki katika vyombo vya kutoa maamuzi yanayowahusu," alisema Tendwa na kuongeza:

"Tuna mifano ya nchi jirani kama vile Malawi, Zimbabwe, Zambia na nyinginezo ambazo tayari zimesharuhusu wananchi wanaotaka kugombea bila vyama kufanya hivyo na wananchi kupata viongozi wanowataka bila kubanwa na chama cha siasa."

Kauli ya Tendwa imekuja wakati serikali imetoa notisi ya kukata rufaa baada ya kushindwa mahakamani katika kesi ya kikatiba ya kupinga kuzuiwa kwa mgombea binafsi.

Tayari serikali imeshashindwa mara mbili katika suala hilo.

Kauli hiyo ya Tendwa pia imekuja wakati kukiwa na misuguano kwenye vyama, hasa CCM ambayo wanachama wake wamekuwa wakieleza waziwazi kuwa na wasiwasi na uwezo wa mwenyekiti wao wa chama kuongoza nchi.

Wasiwasi huo pamoja na majibu dhidi ya wanaoeleza wasiwasi hadharani, umejenga hisia za uwezekano wa chama hicho kuparaganyika iwapo makada hao wa chama watashughulikiwa na vikao vya juu na kuamua kujitoa.

Tayari viongozi wa juu wa CCM wameshaeleza kuwa makada ambao wanamtaka Rais Jakaya Kikwete achukue maamuzi magumu dhidi ya mafisadi, ni wale walioshindwa kwenye uchaguzi uliopita na kwamba wana ajenda yao.

Katika hatua nyingine, Tendwa alipongeza hatua iliyofikiwa na Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar (SMZ), Amani Abeid Karume na katibu mkuu wa CUF, Seif Sharrif Hamad kuacha uhasama wao na kukutana kujadili hali ya amani visiwani Zanzibar.

Alisema hii ni changamoto kubwa kisiasa kwa kuwa inaonyesha ukomavu wa viongozi hao wawili kufanya jambo ambalo halijawahi kufanywa tangu kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi nchini 1992.

"Hivyo, Changamoto iliyoko mbele yetu ni kutengeneza mfumo ambao utaleta umoja wa kitaifa visiwani Zanzibar," alisema.

Tendwa aliendelea kusema sasa umefika wakati kwa wanasiasa kuunda serikali yenye sura ya kitaifa itakayojumuisha uwakilishi wa raia utakaozingatia uwiano wa kijografia na maslahi ya vyama kuweka mshikamano.

"Ni imani yangu kuwa itafika wakati viongozi wetu wa siasa wataukubali ukweli kuwa ufumbuzi wa tatizo la kisiasa Zanzibar ni kuunda serikali yenye sura ya kitaifa ili kuwe na mshikamano wa kudumu," alisema.

Katika maadhimisho hayo, LHRC wamezindua kitabu kinachohusu ripoti ya uchaguzi na mapungufu mbalimbali yaliyojitokeza katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliofanyika Oktoba mwaka huu.

Mwenyekiti wa mtandao huo, Judith Odunga alisema mtandao umedhamiria kusaidia kuzijengea uwezo wa kiutendaji taasisi zote wanachama ili ziweze kutoa msaada wa kisheria unaolingana na viwango vya kitaalamu na mahitaji halisi.

Akizungumza katika maadhimisho hayo, balozi wa Sweden nchini, Staffan Herrstrom aliipa serikali changamoto ya kutoa elimu ya kutosha kuhusu suala zima la uchaguzi kuwasaidia wananchi kuwa na uelewa wa kuchagua viongozi bora na wenye maadili.

Tags:

0 comments

Post a Comment