MWANASIASA mkongwe na mbunge wa kuteuliwa na rais, Kingunge Ngombale Mwiru, amekana familia yake kuhusishwa na umiliki wa Kampuni ya Smart Holdings, inayolalamikiwa kupewa zabuni za ukusanyaji mapato katika mazingira ya rushwa na upendeleo.
Kingunge amevunja ukimya juu ya suala hilo jana, ikiwa ni takribani miezi tisa imepita tangu kampuni hiyo inayotajwa kumilikiwa na familia yake ilalamikiwe kupewa kandarasi ya kukusanya mapato katika Kituo Kikuu cha Mabasi Ubungo (UBT), kwa mkataba mbovu ulioonekana kuinufaisha zaidi kampuni hiyo kuliko Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam.
Ikiwa na zabuni hiyo ya miaka mitano, kampuni hiyo ilidaiwa kuwa ilikusanya sh milioni 1.5 kwa siku, hali iliyosababisha hasara kwa Halmashauri ya Jiji.
Kiwango hicho kilielezwa kuwa kilimsukuma Waziri Mkuu Mizengo Pinda kuingilia kati na kuamua kurejesha jukumu la ukusanyaji wa ushuru mikononi mwa Jiji la Dar es Salaam baada ya mkataba wa kampuni hiyo kumalizika Oktoba, mwaka huu.
Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam iliyoanza rasmi kukusanya mapato kituoni hapo Novemba mosi mwaka huu, ilitangaza kupata mapato ya sh milioni nne kwa siku, tofauti na sh milioni 1.5 iliyokuwa ikiwasilishwa na Smart Holdings kabla ya kumaliza mkataba wake.
Mara baada ya kumaliza mkataba wake UBT, kampuni hiyo ilishinda zabuni nyingine ya kukusanya ushuru katika jengo jipya la wafanyabiashara ndogondogo ‘Machinga Complex’, jambo lililoleta mvutano mkali kutoka kwa wafanyabishara hao waliotangaza kuikataa na kuagiza mchakato wa zabuni urudiwe kwa sababu ya kile walichokielezea kuwa kampuni hiyo ni ya kifisadi na haikustahili kushinda.
Kingunge alipotakiwa na gazeti hili jana kutoa msimamo wake kama mkuu wa familia inayohusishwa na kampuni hiyo, alisema si kweli kuwa yeye na familia yake ni wamiliki.
“Hayo maneno yamesemwa sana na yanaandikwa na waandishi wa habari wasiofanya research (utafiti). Wamesema weee mimi nimenyamaza tu, nimewaacha waseme. Maana wana matatizo na Kingunge.
“Siyo kweli, ukienda BRELA utaona mwenyewe hakuna kampuni ya Kingunge wala ya mwanafamilia wake. Jina la hiyo kampuni linafahamika na wanahisa wake wako, hakuna akina Kingunge kule,” alisema.
Alisisitiza kuwa wote wanaomhusisha na kampuni hiyo ni watu wasio wa kweli bali wanaoeneza maneno hayo kwa malengo na chuki zao za kisiasa.
“Vijana nyie msikubali kutumiwa eeeh... mnatumiwa tu na watu wenye malengo na chuki zao za kisiasa. Waandishi msikubali kutumiwa... umenisikia. Mimi nanyamaza tu,” Kingunge alitoa rai hiyo kwa wanahabari.
0 comments