Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Baada ya kutaka kuzuia Helikopta ya Mbowe Isiruke, Dk. Slaa ashusha bonge la Skendo ndani ya CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Dk. Slaa ailipua CCM Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dk. Willbrod Slaa
• Serikali mkoani Tanga yahaha kuizuia helikopta ya Mbowe isiruke KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willbrod Slaa, jana alifichua ufisadi mkubwa uliofanywa na Chama Cha Mapinduzi (CCM) wa kuingiza magari 200 aina ya Land Cruiser ‘mkonga’ bila ya kulipia sh milioni 600 za ushuru wa forodha kwa Mamlaka ya Mapato nchini (TRA)...
Dk. Slaa aliyasema hayo jana katika mkutano mkubwa wa hadhara wa muendelezo wa Operesheni Sangara uliofanyika katika Kijiji cha Kilole wilayani Korogwe. Alisema amepokea taarifa hiyo jana kutoka kwa msiri wake ndani ya TRA. Alisema hana ugomvi na CCM kuingiza magari 200 kwa ajili ya kupata ushindi mwaka 2010, lakini ugomvi wake mkubwa ni chama hicho kutoyalipia magari hayo ushuru wa sh milioni 600 ambazo zingewasaidia Watanzania katika kujenga nchi kwenye masuala mbalimbali ya maendeleo. Akizungumza kwa kujiamini, alisema suala hilo lina ukweli usiokanushika. Alimtaka na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, kama anaweza akanushe. “Taarifa hii nimeipata leo, na ina ukweli ndani yake. Hivi ninavyoongea yanaweza kutolewa muda wowote bandarini. Kama suala hili ni uongo, Pinda akanushe. Na wakilipa leo waandike tarehe risiti ya leo kwa kuwa hadi ninavyoongea hayajalipiwa,” alisema Dk. Slaa. Alisema huo ni ufisadi mkubwa ambao unafanywa na CCM wakati vyama vingine vinalipa ushuru. Dk. Slaa alisema kuwa mwaka 2005 CCM ilifanya ufisadi kama huo kwa kumtumia mfanyabishara mwenye asili ya Kiasia, Jeetu Patel, na kufanikiwa kuingiza magari 235 bila kulipia ushuru pia. Alisema viongozi wote wa CCM wamewekana katika nafasi za uongozi, ndiyo sababu maadili katika nafasi za uongozi wa kiserikali na taasisi zake yamemong’onyoka. Katika hatua nyingine, Dk. Slaa ameeleza kushangazwa na kitendo cha Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Brigedia Jenerali Mstaafu Hassan Ngwilizi, kutowaeleza wapiga kura wake matumizi ya fedha za miradi zinazotolewa na wahisani mbalimbali. Akihutubia katika mkutano wa hadhara wa Operesheni Sangara, katika Kijiji cha Lukozi wilayani Lushoto juzi, Dk. Slaa alielezea wasiwasi wake kuhusu matumizi mabaya ya fedha hizo zinazotolewa kwa maendeleo ya vijijini mara baada ya kupewa taarifa na wananchi wa kijiji hicho. Alisema kushindwa kutoa taarifa ya matumizi na kiasi cha fedha zinazotolewa na wahisani kwa wananchi ni ufisadi unaofanywa na viongozi, hususan mbunge wa jimbo hilo, ambaye ni mmoja wa wahusika wakubwa wa kusimamia miradi ya maendeleo vijijini. Akifafanua kuhusu baadhi ya fedha zinazotolewa na wahisani kwa maendeleo ya wananchi vijijini kupitia halmashauri za wilaya alisema ni pamoja na zinazotolewa na Mfuko wa Capital Development Fund (CDF) na Local Gavernment Programme (LGCP), ambazo hutolewa kwa kila mtu anayeishi vijijini. “Mnataka kuniambia kuwa hamjui kama kuna fedha zinatolewa na wahisani kwa ajili ya maendeleo ya vijijini na wala hamjawahi kuzisikia? Kama ni kweli muulizeni mbunge wenu, huyo ndiyo anajua ziliko, maana mimi ni mbunge kama yeye najua zinatolewa fedha hizo na kama hamjaziona basi ziko mfukoni mwake,” alifafanua. Alisema kuwa wahisani mbalimbali hutoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zinaelekezwa kwa wananchi kupitia halmashauri za wilaya, hatimaye kuwasilishwa kwa uongozi wa vijiji ambao nao hupanga matumizi na kuyawasilisha kwa halmashauri kuu. Katika ufafanuzi wake kwa wananchi kuhusu fedha hizo, Dk. Slaa alibainisha kuwa, wahisani hutoa kiasi cha dola za Kimarekani 1.5 kwa kila kichwa, kwa maana ya kila mtu hata mtoto mchanga. “Nataka mfahamu wazi kwamba, kila mtu aliyepo hapa hupata dola za kimarekani 1.5 kila siku ambazo hutolewa na wahisani, ambazo ni sawa na sh 3,050 kwa kila mtu kwa siku. Jiulizeni, ni fedha kiasi gani hizo kwa miezi sita? Kama hamjui au hamjawahi kusikia kitu kama hicho, basi mafisadi wanazitafuna,” alisema. Awali wananchi wa kijiji cha Lukozi walimweleza Dk. Slaa katika mkutano huo kuwa, hawajawahi kuelezwa au kusikia fedha zinazoletwa kwao kutoka kwa wahisani, jambo ambalo limezidi kuwaongezea hofu kubwa kwa uongozi wa CCM na serikali yake katika kuendeleza wimbi la ufusadi. Akielezea zaidi kuhusu mwenendo wa mbunge wa jimbo hilo, Dk. Slaa aliongeza kuwa, mbunge huyo amekuwa akijihusisha na masuala ya ufisadi ikiwemo kutetea makandarasi wabovu hata kama hawakubaliki na vyombo vinavyosimamia sheria za nchi kama Bunge. “Nawambieni huyu mbunge wenu mimi namfahamu kuliko mnavyomfahamu nyinyi, aliwahi kumtetea bungeni mkandarasi anaitwa Martin Thomas, ili aendelee na ujenzi wa barabara yenu, jambo ambalo mimi nilipinga vikali. Hata katika hili naanza kupata wasiwasi kuwa kuna ufisadi hapa, muulizeni hizi fedha ziko wapi?” Katika hatua nyingine Dk. Slaa ambaye pia ni mbunge wa Jimbo la Karatu kupitia CHADEMA, aliwataka wananchi wa Mkoa wa Tanga, hususan wa Wilaya ya Lushoto kuwahoji Ngwilizi na Katibu Mkuu wa CCM, Yusuf Makamba kuhusu sh bilioni 40 zilizoibwa kutoka Benki Kuu na Kampuni ya Kagoda. “Hivi mnajua kuwa kuna wizi wa mabilioni ya fedha yaliyochotwa na viongozi wa CCM, mimi ni mmoja wa viongozi wa kwanza kutaja majina ya mafisadi waliochota mabilioni hayo, kama hamjui waulizeni Ngwilizi na Makamba, wanajua, ni fedha nyingi sana ambazo akipewa mtu mmoja sh bilioni 155 na akawa anatumia sh milioni moja kila siku, atazitumia kwa miaka 465,” alisema. Wakati huo huo, serikali mkoani Tanga inahaha kuizuia CHADEMA kurusha helikopta kwa madai kuwa inahatarisha amani na usalama wa watu. Habari za uhakika kutoka ndani ya CHADEMA zimeeleza kuwa tayari uongozi wa Mkoa wa Tanga umeiandikia barua Mamlaka ya Mawasiliano nchini kuitaka kuzuia helikopta inayotumiwa na viongozi wa ngazi ya juu ya chama hicho isitue katika mikutano ya Operesheni Sangara inayoendelea mkoani hapa kwa sasa. “Tunazo taarifa hizo, na tayari uongozi wa mkoa kupitia Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa umeiandikia barua Tume ya Mawasiliano kwa lengo la kuzuia matumizi ya helikopta katika mikutano yetu, wakidai kuwa inahatarisha amani na usalama wa watu jambo ambalo si kweli, ni hofu ambayo imewakumba viongozi wa CCM na serikali yake, tunajua Operesheni Sangara inawaumiza vichwa sana, ndiyo sababu kubwa,” alifafanua Mkurugenzi wa shughuli za Bunge wa chama hicho, John Mrema, alipoulizwa na Tanzania Daima. CHANZO: TANZANIA DAIMA
Tags:

0 comments

Post a Comment