Tanzania yaingizwa katika kashfa nzito ya silaha DRC | |||||||
Jackson Odoyo WAKATI Umoja wa Mataifa (UN) ukiitupia shutuma nzito Tanzania kuwa inasaidia kusafirisha silaha kwenda kikundi cha waasi nchini Congo, serikali imekanusha na kutaka iombwe radhi. Ripoti iliyotolewa mwishoni mwa wiki na kikundi cha UN kilichokuwa nchini DRC kutathimini hali ya usalama, imeeleza kuwa Tanzania imekuwa ikisaidia silaha kikundi cha waasi wa nchi hiyo. Kikundi hicho cha wataalamu wa UN kilichokuwa eneo la mashariki ya DRC kimeeleza kuwa kimeshindwa kuwapatanisha waasi hao kwa kuwa wanapata misaada na nchi jirani, ikiwemo Tanzania. "Nyaraka zimedai kuwa rasilimali za madini zimeendelea kuhujumiwa na kwamba pia kuna ongezeko kubwa la vitendo vya ubakaji na mauaji ya raia," inasema taarifa hiyo iliyovujishwa kwenye vyombo mbalimbali vya habari duniani ambayo Baraza la Usalama la umoja huo limepanga kuijadili. Ripoti hiyo pia imewatuhumu baadhi ya askari wa Congo kuvisaidia kwa silaha vikundi vya waasi wakilipwa mamilioni ya dola zilizopatikana kutoka kwenye migodi waliyovamia. Taarifa hiyo imekuja wakati Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi 25 zinazosaidia mtandao wa kimataifa wa kulinda amani nchini Rwanda. Hata hivyo, ripoti nyingine za taasisi za kimataifa zilizowahi kutolewa awali zimekuwa zikiituhumu Tanzania kuisaidia serikali ya Joseph Kabila kupambana na waasi wa nchi hiyo. Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe alisema juzi kuwa taarifa hiyo haina ukweli na kukitaka kikundi cha hicho kuiomba radhi Tanzania kwa tuhuma hizo zisizokuwa na msingi. Alisema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari mjini Port of Paris- Trinidad na taarifa yake kusomwa na kituo cha televisheni cha TBC1 katika taarifa ya habari ya saa 1:00 asubuhi jana. Alisema taarifa hiyo iliyotolewa na kikundi hicho si sahihi vinginevyo kithibitishe kwa kueleza silaha hizo zimetoka wapi na kugawiwa kwa nani kupitia njia gani. "Tunaamini kwamba taarifa hiyo haikutolewa bure, lazima kuna kitu nyuma yake. Sasa tunataka waseme na kuthibitisha ukweli huo au watuombe radhi," alisisitiza Membe. "Tungependa kutoa changamoto kwa kikundi hicho ambacho kinadai kutumwa na Umoja wa Mataifa kuthibitisha tuhuma ama kuomba radhi," alisema. "Tunataka kiseme silaha hizo zimetoka wapi na kapewa nani, maana sisi katika majeshi yetu hatuna taarifa ya kutolewa silaha," alisema Membe. Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dk Hussein Mwinyi jana alisema hawezi kuzungumzia tuhuma hizo kwa sababu hajapata taarifa kamili kutoka UN. "Siwezi kuzungmzia suala hilo leo kwa sababu taarifa hizo nimezisikia tu lakini taarifa kamili ya UN haijanifikia hivyo ni vigumu kusema chochote," alisema Dk Mwinyi na kuongeza: "Taarifa ikinifikia nitaisoma na kesho (leo), nitaitolea tamko hivyo naomba tuvute subiri," |
You Are Here: Home - - Tanzania yaingizwa katika kashfa nzito ya silaha DRC
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
0 comments