Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Sophia Simba aipasua CCM

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utawala Bora) ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake wa CCM (UWT), Sophia Simba, amekigawa chama tawala katika makundi makubwa mawili. Kundi la kwanza ni la vigogo wa chama wanaompinga vikali, wakiwamo Mbunge wa Same, Anna Kilango-Malecela, Christopher ole Sendeka (Simanjiro), Mzee John Malecela (Mtera), Dk. Harrison Mwakyembe (Kyela), ambao miongoni mwao, Anna Kilango ambaye ni mke wa Makamu Mwenyekiti wa CCM, Malecela, amemwekea mawakili maarufu 10 kumburuza mahakamani kwa madai ya kumdhalilisha na kumchafulia jina. Kundi jingine linamkingia kifua, likiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Pius Msekwa, ambaye jana alimtetea Waziri Simba akisema, ‘hana hatia.’ Mtafaruku unaomzunguka Waziri Simba unatokana na hatua yake ya ‘kusema hovyo’ kwenye kikao cha Kamati ya Usuluhishi inayoongozwa na Rais mstaafu, Ali Hassan Mwinyi, siku chache zilizopita, alipowashambulia kwa maneno makali wabunge wapambanaji wa ufisadi. Habari za uhakika ambazo Tanzania Daima imezipata, zinasema kuwa katika kesi hiyo ambayo bila shaka itavuta hisia za watu, itafunguliwa wakati wowote sasa, baada ya Sophia Simba kukaidi notisi ya siku 14 aliyopewa na mawakili hao kumuomba radhi mbunge mwenzake. Wakati wa kikao kilichopita cha Baraza Kuu la Jumuiya ya Wanawake (UWT), baadhi ya wajumbe walihoji kama Waziri Simba amepata notisi ya kusudio la kufunguliwa kesi. Yeye alikiri kupata notisi hiyo ya siku 14, zilizomalizika jana. Hata hivyo, Baraza Kuu halikuweza kujadili suala hilo ndani ya kikao hicho kwa vile Mama Kilango si mjumbe. Hivi karibuni, kwenye kikao cha Kamati ya Mzee Mwinyi mbele ya wabunge wa chama hicho tawala, wakati akichangia hoja kuhusu chanzo cha wabunge kulumbana wao kwa wao, Waziri Simba alimshambulia Mama Kilango kwamba si msafi kiasi cha kuwatuhumu wenzake kwamba wanahusika na ufisadi. Waziri Simba alimtuhumu Mama Kilango kuwa si msafi, na kwamba baadhi ya watu anaowaita mafisadi leo ndio waliofadhili harusi yake na Mzee Malecela. Alienda mbali kwa kusema bila juhudi za Rais mstaafu wa awamu ya tatu, Benjamin Mkapa, mama huyo asingeolewa na mkongwe huyo wa siasa nchini. Waziri Simba alidiriki kudai kuwa hata harusi ya Kilango na makamu huyo wa zamani wa CCM ilifadhiliwa na mtuhumiwa wa ufisadi, Jeetu Patel. Patel kwa sasa ana kesi katika Mahakama ya Kisutu akituhumiwa kuiibia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kwa kuchota takribani sh bilioni 11 kutoka katika Akaunti ya Malipo ya Madeni ya Nje (EPA). Akijieleza kwenye kamati hiyo, Simba alimtuhumu pia Malecela, ambaye aliwahi kuwa waziri mkuu katika serikali ya awamu ya pili, kwamba wakati akiwania kuteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM mwaka 2005, Jeetu alimpa sh milioni 200 kwa ajili ya kampeni zake. Malecela, ambaye wakati huo alikuwa makamu mwenyekiti wa CCM, aliondolewa mapema kwa nguvu ya Mkapa, hata bila kujadiliwa na vikao. Akizungumza kwa kujiamini na ujasiri, Simba alimtuhumu Mama Kilango kuwa kelele zake zote zinatokana na nongwa ya kuukosa ‘ufesti ledi’ (kuwa mke wa rais). Naye Kilango alisema alishuhudia wakati makombora hayo yakirushwa, akaeleza kwamba anajiandaa kujibu mapigo. Mbali na Mzee Malecela na mkewe, Waziri Simba pia alimgeukia Mwenyekiti Mtendaji wa IPP, Reginald Mengi akimtuhumu kuwa anaendesha vyombo vya habari vinavyoichafua CCM na serikali yake kwa maslahi yake binafsi. Pia alimshambulia Mbunge wa Kyela, Dk. Mwakyembe na Mbunge wa Simanjiro, Sendeka, akiwatuhumu kuwa ni watu wenye njaa na kwamba, wanalipwa fedha kufanya kazi hiyo. Waziri Simba alisema hata tuhuma dhidi ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Andrew Chenge na Mbunge wa Monduli, Edward Lowassa, zimetokana na chuki binafsi. Alisema uchunguzi wa kashfa ya rada ulishamalizika na Chenge akasafishwa na kuongeza kwamba, hata uchunguzi wa Richmond umebaini kulikuwa hakuna rushwa, kwa mujibu wa mtoaji habari wetu. Wakati Kilango akijiweka sawa kufungua kesi, ndani ya CCM, hatua hiyo imezua mjadala mkubwa. Baadhi ya wanachama wanataka mahasimu hao wawili wapatanishwe ndani ya vikao na wengine wanataka suala hilo litinge kortini ili haki itendeke. Baadhi ya wanaomsakama Simba wamefika mahali pa kumshauri Rais Jakaya Kikwete amtimue kazi. Hata hivyo, Msekwa alisema jana kuwa, Waziri Simba hakukosea, na kwamba alikuwa sahihi kutumia uhuru wake ndani ya chama kuibua hoja ambazo zilipaswa kuwa siri. “CCM haiwezi kumchukulia hatua Mheshimiwa Simba kwa kusikiliza maneno ya uvumi, ambayo yamekuwa yakiandikwa na kusikika katika vyombo vya habari,” alisema Msekwa. Kwa sababu hiyo, Msekwa alisema chama hakiwezi kuchukua hatua zozote dhidi yake. Alitoa kauli hiyo wakati wa hafla ya kusaini makubaliano ya miaka mitano ya ushirikiano kati yake na Chama Cha Kikomonisti cha Cuba (CPC) ambapo Cuba iliwakilishwa na Balozi wake nchini, Ernesto Gomez Diaz. Msekwa ambaye alikuwa mjumbe katika kamati ya watu watatu ya kutafuta chanzo cha mgogoro wa wabunge wa CCM na mawaziri, alisema anayeona Waziri Simba amekosea kutokana na kauli yake, anapaswa kupeleka ushahidi wa maneno na wa kisheria ili CCM iweze kuchukua hatua na si kuzungumza tu. Wadadisi wa masuala ya kisiasa nchini wanasema, mgawanyiko huu wa makundi ya vigogo kuhusu kauli za Simba, unaongeza ufa katika chama ambacho kwa miaka miwili mfululizo kimekuwa kinahaha kujinusuru na tuhuma za ufisadi zinazowakabili makada wake wakuu, ambazo kwa mara ya kwanza zilirushwa na viongozi wa vyama vya upinzani mwaka 2007. Wanadai kwamba kwa kuwa Rais Kikwete ndiye alimteua Simba kuwa mbunge na waziri, na kwa kuwa amegoma kumchukulia hatua kutokana na jinsi alivyowasilisha kauli zake, naye anaingizwa katika kundi linalombeba Simba, akiwa upande wa makamu wake, Msekwa. Na ingawa Mzee Malecela, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa CCM kabla ya Msekwa, ni mjumbe wa kudumu wa Halmashauri Kuu ya CCM, mashambulizi haya dhidi yake na mkewe yanamfanya kuwa katika kundi linalomtetea Kilango na kumsakama Simba.
Tags:

0 comments

Post a Comment