WAZIRI Mkuu wa zamani, Jaji Joseph Warioba, ameonyesha wasiwasi kuhusu uongozi wa nchi, akisisitiza kuwa umekuwa karibu mno na matajiri, na nchi inaendeshwa kwa kuwasilikiliza matajiri zaidi, kuliko wananchi wa kawaida.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba, hata katika sekta ya utumishi wa umma, viongozi wamekuwa wakilipwa mishahara minono yenye tofauti kubwa na ya kima cha chini.
Mbali na mtazamo huo, Warioba ameonyesha wasiwasi pia kuhusu kesi za ufisadi, kushangazwa na viongozi wa wanaotilia shaka viongozi wa dini wanaojitoa kutoa elimu ya uraia.
Katika mazungumzo yake na baadhi ya vyombo vya habari ofisini kwake jijini Dar es Salaam jana Jumanne, Warioba alizungumzia pia kuporomoka kwa maadili, kuimarika kwa matabaka na mitandao ndani ya vyama vya siasa, kikiwamo Chama cha Mapinduzi (CCM).
“Tanzania bado ni nchi ya amani na utulivu, lakini kuna dalili za umoja kuanza kutoweka, tumeanza kugawanyika katika vikundi…kuna matabaka yapo wazi kabisa,” alisema na kuongeza:
“Tofauti ya kimapato ni kubwa hata ndani ya Serikali, kima cha chini kimetofautiana sana na mishahara ya wakubwa, achilia mbali posho wanazopata, kima cha chini 100,000 lakini cha juu kimefikia hadi milioni tano.
“Hii ni hatari, na matokeo yake ni kuwapo kwa watendaji wa chini walioamua kupigania maslahi yao hata kwa kuvujisha siri.
“Uongozi umekuwa karibu mno na matajiri kuliko wananchi wa kawaida, wanaovujisha siri ni hao wasioridhishwa na hali hii,”
“Wameanza kuchukua hatua za kutetea maslahi yao kwa migomo na mambo mengine kama kuvujisha siri. Nimeshangaa watu wanatoka Ngorongoro wameacha uongozi wa kijiji, wilaya na mkoa huko hadi wanafika mbele ya lango la Ikulu,”
“Tusipoangalia tutafika kubaya. Ni wazi viongozi wameanza kupoteza imani kwa wananchi, na wananchi wameanza kutenda mambo yao wenyewe ili kujitetea…kuna credibility gap na hii ni hatari,” alisema Warioba, aliyewahi kuwa Mwanasheria Mkuu na Waziri wa Katiba katika Serikali ya Mwalimu Julius Nyerere na baadaye Waziri Mkuu katika Serikali ya Ali Hassan Mwinyi.
Alishtushwa na kuibuka kwa udini na ukabila kiasi cha kuingia hata ndani ya mijadala bungeni, akitaja suala la Mahakama ya Kadhi, na kujiunga kwa Tanzania kwenye Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC), akikosoa mijadala hiyo kwa kurejea hoja za Tanganyika zilizoanzishwa na kundi la Wabunge la G55.
“Mwaka 1993 kundi la G55 liliibuka baada ya Zanzibar kutaka kuingia OIC, ni kundi lililoijadili OIC kama hoja ya kitaifa na si ya dini fulani, kwenye kundi hilo walikuwamo Waislamu na Wakristo, walitetea utaifa na kusimamia hoja yao kitaifa.
“Leo hoja za Mahakama ya Kadhi na OIC zinajadiliwa kwa mgawanyiko wa kidini, Mwislamu anaunga mkono, Mkristo anapinga si kwa kuangalia tatizo au uzuri wa hoja kwa Taifa. Imejitokeza hata bungeni, hii ni hatari,” alisema na kuhimiza masuala hayo yajadiliwe kwa mtazamo wa kitaifa na si makundi au maslahi ya dini fulani.
Kwa upande mwingine, alijadili hoja hiyo kwa kuutazama waraka wa Kanisa Katoliki, akisema haoni tatizo lake zaidi ya kuhimiza elimu ya uraia na kupatikana viongozi waadilifu.
“Tutafikia mahala tutawataka viongozi wa dini kabla ya kwenda makanisani kuhubiri ubaya wa rushwa tutataka kushauriana nao kwanza, tunakwenda wapi?
“Mimi si Mkatoliki, lakini nasoma elimu ya uraia wanayotoa na si mwaka huu, kuanzia mwaka 1994, 1999 na 2004, lugha imekuwa ikibadilika kulingana na wakati…sasa tusijadili au kupinga mambo kwa kutazama mwingiliano wa maslahi ya vikundi, tutazame manufaa kwa Taifa.
“Mwalimu Nyerere alikuwa Mkatoliki mcha Mungu, kila siku ya kawaida alikuwa anakwenda kanisani saa 12 kusali, lakini hata siku moja hakuingiza masuala ya dini kwenye uongozi wa nchi.
“Leo viongozi wa siasa ndio tatizo, wanaingiza siasa kwenye dini. Viongozi wa dini si tatizo, tatizo viongozi wa kisiasa, kwenye Pasaka au Krismasi wanaandaa hafla na kukaribisha viongozi wa dini na kupiga siasa, mwezi Ramadhani hata wasio Waislamu wanaandaa futari, sikukuu za kidini zinatumiwa na wanasiasa kupiga siasa,” alisema.
Alionyesha wasiwasi wake pia kuhusu kesi za ufisadi, zikiwamo za EPA akitilia shaka kuwa zimekuwa na misingi ya kisiasa zaidi kuliko misingi imara ya kisheria.
“Niombe Rais asihusishwe kwenye masuala ya kesi hizi, vyombo vinavyohusika vichunguze na kufungua mashitaka wasimhusishe Rais kuelezea.
“Kwa sababu kwa mfano EPA, wametueleza kampuni 22 zimeiba na nyingine zimerudisha fedha na hiyo ni taarifa ya Rais, leo baadhi wameshitakiwa, lakini fedha walizorudisha zimepangiwa matumizi.
“Inakuwaje kama wakishinda kesi? Watendaji waliomshirikisha Rais wataweza kusema aliwashurutisha,” alisema Warioba.
Akitoa mfano, alisema kesi ya aliyekuwa Kamishna wa Polisi Abdallah Zombe, hakuna shaka kwamba watu waliuawa, lakini kwa nini wauaji hawapatikani?
Jaji Joseph Warioba
“Kesi ziandaliwe mashitaka kwa misingi ya kisheria na si kisiasa, tuliwahi kufanya hivi kisiasa mwaka 1979 Operesheni Mitumba, na mwaka 1983 Operesheni Wahujumu Uchumi, lakini Taifa lilipata hasara kwa kuwalipa baadhi ya washitakiwa walioshinda kesi,” alionya Warioba.
Hata hivyo, katika hatua nyingine alitaka utata wa kifisadi katika masuala ya kampuni za Deep Green na Meremeta upatiwe majibu kwa wananchi ambao tayari wamepewa taarifa zinahusu masuala hayo.
“Jamii imekwishapewa taarifa kuhusu masuala kama ya Deep Green na Meremeta, yameshafika huko na wananchi wanasubiri taarifa, si vizuri kukaa kimya…ukimya ni kujiandalia matatizo makubwa zaidi,” alishauri Jaji Warioba.
Akizungumzia baadhi ya wabunge kuwa mstari wa mbele kupinga ufisadi, Warioba alisema waachwe waendelee na angefurahi zaidi kama kundi hilo lingeongezeka idadi.
“Kumekuwa na kauli za utata miongoni mwa viongozi wa juu wa CCM kuhusu kilichotokea kwenye kikao cha NEC Dodoma, sijui tumwamini nani kati yao, maana kila mmoja amekwisha kusema lake.
“Lakini ukiangalia utaona kuna wanaopinga maovu, na kuna wengine wanataka kasi ipunguzwe, mimi nataka waongezeke wanaopinga na kuungwa mkono,” alisema Warioba huku akionekana dhahiri kupinga mitandao ya kisiasa ndani ya vyama, hususan CCM.
Kwa mujibu wa Jaji Warioba kwa ujumla, nchi inakabiliwa na ombwe la uongozi kuanzia ngazi ya mitaa, vijiji, wilaya na maeneo mengine.
Alisema yapo masuala kadhaa ya kuangalia kabla ya Uchaguzi Mkuu mwakani, ili kujiepusha na kile alichoita EPA na Deep Green nyingine.
“Wapo viongozi, na wengine wabunge wanalalamika fedha kutawanywa huko kwenye majimbo, haya yamesikika viongozi wamekaa kimya.
“Hivi karibuni nimesoma kwenye gazeti kuna kadi bandia za CCM zimekamatwa zilizochapishwa ili zitumike kumpa ushindi mgombea fulani.
“Sasa kwenye baadhi ya maeneo nchini, mshindi ndani ya CCM ndiye mshindi wa nafasi ya uongozi wa ki-serikali, matukio kama haya ni hatari. Tulipiga kelele kuhusu sheria ya takrima hadi tunakwenda kwenye uchaguzi bado msimamo halisi wa kisheria haujajulikana,” alisema katika mazungumzo hayo ambayo Raia Mwema itayachapisha katika toleo lijalo.
0 comments