Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Kikwete akataa kiti chake, afisa mwandikishaji akikalia

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter AFISA wa kituo cha kuandikisha wapiga kura kwa ajili ya uchaguzi wa serikali za mitaa, Issa Kipengere juzi alikalia kiti maalum alichoandaliwa Rais Jakaya Kikwete alipokwenda kujiandikisha baada ya mkuu huyo wa nchi kukikataa kiti chake. Lakini baada ya kukalia kwa dakika chache walinzi walimtimua ofisa huyo kwenye kiti hicho licha ya kupewa ruhusa na Rais Kikwete. Kabla ya rais kufika kwenye kituo hicho cha Shule ya Msingi ya Bunge, wasaidizi wake waliweka kiti hicho ndani ya chumba cha kuandikishia wapiga kura na baada ya kufika ofisa huyo alisimama kumkaribisa Kikwete, lakini badala yake rais alikwenda kukalia kiti kingine. "Ahaa, wewe kaa tu mimi nitakaa katika hiki kiti (cha mwandikishaji) halafu wewe ndio ukae katika hicho kiti (cha rais)," alisema Rais Kikwete alipoombwa na ofisa huyo wa kituo hicho namba moja akalie kiti kilichoandaliwa na wasaidizi wake. "Mimi hapa nimekuja kujiandikisha hivyo ninastahili kukaa hapa na wewe (ukae) hapo." Hata hivyo Kipengere alikataa kukikalia kiti hicho na mara baada ya rais kuondoka kituoni hapo, ofisa huyo alikalia kiti hicho cha rais, lakini hakukifaidi kwa muda mrefu kwani afisa usalama mmoja kutoka Ikulu alimkaripia vikali kwa kitendo hicho. "Wewe unakaa katika kiti cha rais?, kwa nini unafanya hivyo, ina maana hata siku nyingine unaweza...,"alifoka ofisa huyo wa usalama. Kipengere, 45, ambaye ni mwalimu wa Shule ya Msingi Bunge aliiambia Mwananchi baadaye kuwa kuwa hiyo ni mara yake ya kwanza kukaribiana na Rais Kikwete. "Nimejisikia ni mtu mwenye bahati kumuandikisha, kuwa karibu naye, na kuonana naye ana kwa ana Rais Kikwete. Sijawahi kupata nafasi kama hii katika maisha yangu," alisema Kipengere. Kikwete pia aliwahi kukataa kukaa kiti kilichoandaliwa na wasaidizi wake wakati wa misa ya kumuaga mbunge wa zamani wa jimbo la Mbeya Vijijini, marehemu Richard Nyaulawa iliyofanyika jijini Dar es salaam baada ya maofisa hao wa usalama wa taifa kumuandalia kiti ambacho kilikuwa kikitumiwa na padri aliyekuwa akiendesha misa hiyo. Rais, ambaye juzi alivalia mavazi ya kawaida tofauti, hakuridhishwa na idadi ndogo ya watu aliowakuta kwenye kituo hicho. "Ehe ina maana kuwa mimi ndio mtu wa 12 kujiandikisha katika hiki kituo, sijui kama tutafika watu 200 nina hofu juu ya hili,"alisema Rais Kikwete mara baada ya kujiandikisha katika kituo hicho Hadi kufikia juzi watu 30 tu ndio waliokuwa wamejitokeza kujiandikisha kwenye kituo hicho kilicho Kata ya Kivukoni kwa ajili ya uchaguzi huo uliopangwa kufanyika Oktoba 25. Rais Kikwete alisema watu wengi hasa wa mijini uenda wasijitokeze kujiandikisha na kupiga kura kwa wingi katika uchaguzi huo kutokana na kuamini kuwa uchaguzi huo si muhimu tofauti na chaguzi za rais, wabunge na madiwani.
Tags:

0 comments

Post a Comment