Subscribe to receive latest Updates

Online :

You Are Here: Home - - Hali si nzuri ndani ya NEC

IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII: counter
Amweka kwenye kipindi cha majaribio
Mengi naye aguswa ndani ya NEC
Ya Mkapa yawatisha wajumbe

MWENYEKITI wa Chama cha Mapinduzi (CCM) amemtega Spika Samuel Sitta ambaye ana muda hadi Novemba mwaka huu kujirekebisha, Raia Mwema imeambiwa.

Mtego huo ambao kwa upande mmoja unapalilia zaidi mpasuko wa ndani baina ya kundi la Sitta na jingine ambalo yeye amekuwa akidai linamtafuta, ulihitimishwa juzi pale Sitta alipotakiwa kujitetea ili asinyang’anywe kadi ya uanachama hatua ambayo dhahiri ingeshusha kila aina ya ndoto aliyonayo.

Baadhi ya wana CCM waliozungumza na Raia Mwema wakirejea Mkutano wa Halmashauri Kuu ya chama hicho ulioanza mwishoni mwa wiki iliyopita wanasema mbali na kumpatiliza Sitta, Kikwete pia aliruhusu kutikiswa kwa mtu wa karibu na Sitta, mfanyabiashara maarufu, Reginald Mengi, ambaye kama Sitta, amekuwa akisema kwamba yumo katika vita dhidi ya ufisadi ili kumsaidia Rais Kikwete anayeiongoza.

Habari za ndani ya CCM kutoka katika vikao rasmi na visivyo rasmi, zinaeleza kwamba Rais Kikwete ameamua, kutumia mtindo wa “kuuma na kupuliza” kwa marafiki zake, Sitta na Mengi kwa kuruhusu mjadala kwenda katika mpangilio ulioandaliwa mahususi kwa ajili ya ‘kuwashughulikia’ Sitta na Mengi, na kwa maana hiyo kundi la wabunge ambalo limekuwa likijitambulisha na Sitta.

Taarifa za ndani zinasema, katika kikao hicho, mbali ya Sitta kujadiliwa, mmoja wa wabunge alibanwa kwa kumshirikisha Mengi katika shughuli za CCM ikidaiwa kwamba mfanyabisahara huyo si mwana CCM.

Hata hivyo, habari zinasema kwamba pamoja na Mengi kuwa mwana CCM na mtu anayekisaidia chama hicho kwa muda mrefu, mfanyabiashara huyo amekuwa karibu na Rais Kikwete na amekuwa akimtaja na kumsifia Rais hadharani.

“Karibu wajumbe 40 walizungumza dhidi ya Sitta. Walikuwa wakitoa wito afukuzwe kwa jinsi anavyoliendesha Bunge ambalo katika siku za karibuni limekuwa likiibana sana Serikali.

“Aliomba sana msamaha, lakini dhahiri hakuna hata mmoja aliyekuwa akimsikiliza, hata wachache waliojaribu kumuunga mkono walizomewa wasiweze kuendelea kusema lolote.

“Kwa hiyo kwa sasa ni kama Sitta yupo katika kipindi cha majaribio. Hatima yake itategemeana na jinsi anavyoliendesha Bunge kati ya sasa na Novemba. Hiyo kamati iliyoundwa imepewa mwanya wa kuitisha kikao cha dharura kama itaona kuwa anakwenda ndivyo sivyo,” anasema mmoja wa wajumbe wa NEC aliyezungumza na Raia Mwema kwa masharti ya kuwa hatajwi kama chanzo cha habari hii.

Mjumbe mwingine aliiambia Raia Mwema kwamba pengine msumari wa mwisho katika jeneza la Sitta utakuwa umepigiliwa na mkongwe, Kingunge Ngombale Mwiru ambaye alimsema Sitta kwamba japo amekuwa akidai kwamba anaendesha Bunge kwa mtindo wa Uingereza (Jumuiya ya Madola), uendeshaji wake haukuwa sawa na huo wa Uingereza.

“Kwanza Ngombale alichanachana Waraka wa Wakatoliki akidai ni ilani ya kisiasa na kwamba haiwezekani nchi ikawa na ilani zaidi ya moja kwa wakati mmoja, kisha akamrukia Sitta.

Yalizungumzwa mengi, pamoja na kumtetea Mkapa (Benjamin) na wapo walioonya kwamba kwa kuruhusu Mkapa kukwaruzwa, Kikwete alikuwa anaandaa kaburi lake mwenyewe,” anasema mjumbe huyo.

Lakini mjumbe mwingine, mfuasi wa kundi moja kati ya makubwa yanayopingana kwa sasa ndani ya CCM ameiambia Raia Mwema hata hivyo kwamba msimamo wa Kikwete katika suala la Sitta unaweza usiwe na maslahi makubwa kwa chama siku za usoni.

“Kikwete anaonekana hataki kuwaudhi marafiki zake wote wakiwamo hata wale ambao alionekana kuwatosa kutokana na kuhusishwa kwao na kashfa mbalimbali ambazo Sitta na kundi lake wamekuwa wakizisemea. Nadhani alipaswa kuwa na msimamo wa wazi katika hili maana linahusu mustakabali wake kisiasa na wa chama chetu.

“Sasa wananchi wana uelewa kuliko wakati mwingine wowote na kwamba mwaka mmoja si mbali kuelekea kwenye uchaguzi mwingine na hii ni hatari sana kama hakutatokea jambo lolote zito,” alisema mwanasiasa huyo katika mazungumzo ya simu kutoka Dodoma alikokuwa akihudhuria vikao hivyo.

Katika vikao vyake vya juu mjini Dodoma vilivyomalizika juzi, CCM imeunda timu ya viongozi wake ndani ya Kamati Kuu yake kuchunguza mwenendo wa uhusiano kati ya chama hicho, Serikali na Bunge, mambo ambayo ndiyo msingi wa tuhuma dhidi ya Spika Sitta na watu walio karibu naye.

Rais mstaafu Ali Hassan Mwinyi, Spika za zamani ambaye pia ni Makamu Mwenyekiti wa CCM, Pius Msekwa na waziri wa zamani, Abdulrahman Kinana ndio wanaounda timu ya kufuatilia mwenendo wa Sitta.

Mkakati uliotumika katika kumjadili Sitta unashabihiana kwa staili na ambayo amekuwa akiitumia Spika huyo kujadili mambo nyeti ndani ya Bunge kwa kuwapanga wabunge anaowaamini, kuzungumza. Haikuweza kufahamika mara moja orodha hiyo ya wazungumzaji iliandaliwa na nani.

Taarifa zaidi zinaeleza kuwa baadaye Sitta alipewa “ushauri wa busara” ili aombe radhi wajumbe hao, ikielezwa kuwa ni hatua ambayo ilikuwa ikiungwa mkono na Rais Kikwete. Kikwete anadaiwa kuunga mkono Sitta kuomba radhi kwa vile hakuwa “tayari kupoteza Spika katika kipindi hiki, na wala CCM haiwezi kupoteza mbunge wakati huu”.

Taarifa zaidi zinasema huu si mwisho wa suala la Sitta na chochote kinaweza kutokea siku za baadaye, huku taarifa nyingine zikieleza kuwa Rais Jakaya Kikwete amekuwa na kikosi kazi cha siri kinachochunguza mwenendo wa kundi hilo.

Inadaiwa kuwa moja ya kazi zilizokwishafanywa na kikosi kazi hicho ni pamoja na kupima upepo wa kisiasa katika Jimbo la Urambo Mashariki, linaloongozwa na Sitta. Kikosi kazi hicho kilipewa jukumu la kukusanya taarifa huru kuhusu Sitta na wale wanaodaiwa kumwandamana kwa mbinu chafu, na kati ya mambo yanayodaiwa yamepatikana ni kutumiwa kwa mmoja wa mawaziri kufanikisha mbinu hizo zinazodaiwa ni chafu.

Sitta ambaye amekuwa akijigamba kwa wanasiasa wenzake akiwataka wawe na ngozi ngumu ya kuhimili mikikiki ya siasa, mikakati iliyosukwa safari hii ndani ya NEC imedhihirika kumtoa jasho na hata kumweka katika mtazamo mpya kuwa anayo kazi kubwa ya kufanya dhidi ya mikakati mingine ijayo.

“Kwa kweli tukubali kuwa hali si nzuri katika chama chetu, si nzuri kwa sababu zimejitokeza hoja za kupingana…hapana hata kidogo, ni kwamba si nzuri kwa sababu nguvu ya fedha imeteka busara za baadhi ya wajumbe wa vikao muhimu kama NEC. Na kama Watanzania wataamua vinginevyo basi vikao hivi vya NEC na hata CC vitazidi kupoteza maana.

“Itakapofikia hivyo, itakuwa hatari zaidi kwa CCM kwani vikao kama hivyo ndivyo vinavyopitisha majina ya wagombea nafasi za ubunge, na urais. Watu wakipoteza imani na wajumbe wa NEC, inayopitisha mgombea urais maana yake chama ndiyo kinang’oka madarakani,” alisema mjumbe mmoja wa CCM, ambaye hakutaka kutajwa jina kuelezea kwa ujumla mazingira ya NEC ya wiki iliyopita.

Kabla ya kuanza kwa vikao vya CC na NEC, ambayo safari hii Rais mstaafu Benjamin Mkapa alihudhuria, miongoni mwa wanachama wa CCM walioonyesha mtazamo wao wa kutaka Sitta ang’oke ni pamoja na Mbunge wa Ukonga, Dk. Makongoro Mahanga, ambaye si tu alimlenga Sitta, bali pamoja na wabunge wengine wanaodaiwa kupiga vita ufisadi.

Siku chache baada ya Bunge kumalizika, viongozi wa wakuu wa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Mwenyekiti Hamadi Yusuf Masauni na Katibu Mkuu, Martin Shigela, walikutana na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam na kuwaeleza mambo mbalimbali likiwamo suala la kuwapo baadhi ya viongozi kujipatia umaarufu kwa kudai kupinga ufisadi na kusisitiza kuwa kinara wa vita dhidi ya ufisadi ni Rais Jakaya Kikwete.

Wachunguzi wa mambo ya kisiasa mjini Dodoma wanaamini kuwa tishio la sasa dhidi ya Sitta linalenga kuzima makali ya Bunge katika mkutano wake ujao, ambako Serikali itapaswa kutoa taarifa kadhaa ikiwamo ya kuhitimisha sakata la Richmond.

Katika mkutano uliopita wa Bunge, taarifa ya Richmond ilikataliwa na Bunge kwa madai kuwa ililenga kuwasafisha watuhumiwa badala ya kutekeleza maazimo ya mhimili huo wa taifa.

Tags:

0 comments

Post a Comment