Kocha wa Yanga Kondic Dusan(Kulia) akiwa na msaidizi wake, Spaso Solokovisk. Kondic ambae timu yake inacheza na Al- Ahly wikiendi ijayo katika mechi ya Ligi ya Mabingwa amelalamika kwamba wachezaji wake wote zaidi ya saba waliokuwa kwenye timu ya Taifa ni wagonjwa na hajui la kufanya. |
You Are Here: Home - HABARI ZA MICHEZO - mAXIMO KOCHA WA TIMU YA TAIFA ADAIWA KUUA WACHEZAJI WOTE WA YANGA
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Kondic: Maximo umeua wachezaji wangu wote
Na Michael Momburi
KOCHA wa Yanga, Kondic Dusan amesema hana raha kwani wachezaji wote waliokuwa kwenye kikosi cha Taifa Stars wapo katika hali mbaya.
Ingawa hakumtaja Kocha wa Taifa Stars, Marcio Maximo, Kondic amekuwa akilalamika mara kwa mara wachezaji wake wengi kuitwa kwenye kikosi cha Stars na kuingilia ratiba ya klabu hiyo.
Yanga inajiandaa na mechi ya raundi ya kwanza ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri ambayo wenyeji wametangaza rasmi kwamba itachezwa jijini Cairo Jumapili ya wikiendi ijayo.
Kondic aliiambia Mwanaspoti mazoezini kwenye Uwanja wa Uhuru Alhamisi usiku, kwamba, hali ya wachezaji wote waliokuwemo kwenye kikosi cha Stars si nzuri na inamuweka katika wakati mgumu.
Wachezaji wa Yanga waliokuwa na kikosi cha Stars kwenye fainali za CHAN ni Shadrack Nsajigwa, Nurdin Bakari, Kigi Makassi, Godfrey Bonny, Nadir Haroub 'Cannavaro', Athuman Idd, Amir Maftah, Mrisho Ngassa, Jerry Tegete na Abdi Kassim.
"Sina raha kabisa, usinione ninavyozungumza na wewe. Niko kwenye wakati mgumu sana wachezaji wangu tegemeo waliokuwa safarini wamerudi lakini wote ni matatizo," alisema Kondic kwa hasira kocha huyo wa Serbia.
"Kila mmoja ni mgonjwa hakuna mzima hata mmoja, halafu angalia nina siku ngapi kabla ya kuingia kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly tena ugenini.
"Ngassa na Cannavaro hawapo mazoezini matatizo ni hayo hayo kwamba hawako vizuri na wana majeraha madogo madogo ndio maana nimewaruhusu wapumzike.
"Hao wengine umewaona hapo wamekuja na wanafanya mazoezi lakini kila mmoja ana tatizo; mara msuli unauma, mara goti! Hakuna hata mmoja ambaye yuko kamili, yaani hapa inabidi kufanya kazi ya ziada sana na kutegemea ripoti ya daktari.
"Vinginevyo hali itakuwa ngumu sana halafu muda tulionao ni mfupi mno. Sina raha kabisa, najaribu kufanya kazi kadri inavyowezekana niangalie hali za hawa wachezaji zitakuwaje katika siku zilizobaki,"alisisitiza Kondic ambaye alisema mambo mengine yanakwenda vizuri mazoezini.
Katika hatua nyingine, Kondic alisema kwamba kiungo wake, Athuman Idd 'Chuji' amemwambia kwamba hana tofauti zozote na kocha Marcio Maximo kama inavyoripotiwa.
"Nimezungumza naye kaniambia kwamba hana matatizo yoyote na Maximo wala Taifa Stars na mimi nadhani kama kungekuwa na tatizo Maximo angeshaniambia lakini huyo kocha hajanieleza au kunipigia simu,"alisisitiza Kondic kwa kifupi na kusisitiza kwamba labda abanwe mwenyewe Idd anaweza kusema zaidi.
Lakini hata hivyo mchezaji huyo ambaye amejitoa kwenye timu ya Taifa amekuwa mgumu kutoa tamko.
Katika mazoezi ya juzi jioni ambayo wachezaji Ngassa na Cannavaro ndio pekee waliokosekana, mabingwa hao watetezi walikuwa wakichezea mipira uwanjani kwa zaidi ya saa mbili na baadaye wakatumia dakika chache kunyoosha viungo kabla ya kupanda gari na kuelekea kambini kwenye Hoteli ya Tamal iliyoko karibu na Mwenge karibu na ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) jijini Dar es Salaam.
Timu hiyo imetimuliwa kwenye Hoteli ya Lamada baada ya kushindwa kulipa fedha wanazodaiwa.
0 comments