You Are Here: Home - - TANZANIA YAKABITHI URAIS WA UMOJA WA AFRIKA ADDIS ABABA....
IDADI YA WATU WALIOSOMA HABARI HII:
Tanzania leo inamaliza kipindi cha mwaka mmoja cha kuwa Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), kwa sifa kemkem baada ya kutumikia mataifa ya Afrika kwa upendo na mafanikio makubwa.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, anayehudhuria makabidhiano hayo mjini hapa, alisema jana kuwa kwa kipindi cha mwaka mmoja wa Tanzania kuwa Mwenyekiti wa AU kupitia Rais Jakaya Kikwete, bara limepata huduma bora za kiwango cha juu na za kuridhisha.
Membe alisema huduma hiyo imeleta matunda mengi ya mafanikio kwa mataifa hayo ambayo si rahisi kusahaulika. Akizungumza baada ya mkutano wa Baraza la Watendaji la AU uliomalizika juzi usiku, Membe alisema Rais Kikwete amewezesha na kuacha mafanikio mengi katika kipindi hicho, ikiwamo ukombozi wa kisiwa cha Anjouan nchini Comoro.
Alisema suala la Comoro lilijulikana na AU kwa muda mrefu, lakini Tanzania ilipokuwa na dhamana wa Uenyekiti ililivalia njuga suala hilo na matokeo ya haraka yaliyokuwa na mafanikio makubwa yalipatikana.
Alisema nchi ilituma wanajeshi zaidi ya 700 katika visiwa hivyo kushiriki na kuunda Jeshi maalumu la AU la Operesheni Demokrasi hiyo ambayo walilenga kumsaidia Rais wa Comoro kustawisha utawala wake nchini humo.
Kuhusu athari za Uchaguzi Mkuu zilizotokea nchini Kenya, Membe alisema pia Rais Kikwete alimaliza mgogoro huo uliotikisa siyo tu nchi hiyo, bali dunia nzima jambo lililowezesha atunukiwe Shahada ya Heshima ya Uzamivu.
“Pia kulikuwa na jitihada za kuleta amani na utulivu huko Burundi. Kikundi cha Waasi, Palipehutu (FNL) walikubali kuacha kutumia jina lao la zamani ambalo lilikuwa la ukabila, Serikali ya Burundi ikaachilia wafungwa 1,800 waliokuwa wa kundi la waasi, askari 33 wa FNL waliajiriwa na majuzi Rais Kikwete aliagiza wanachama wa makundi haya wanaoishi Dar es Salaam kurudi nyumbani,” alisema Membe.
Aidha, alisema pia kuwa Rais Kikwete alimaliza tatizo la muda mrefu lililokuwa likikabili watumishi katika Sekretarieti ya AU kwa kufanikisha kuongezwa mishahara ikiwamo kulipwa malimbikizo, posho za matibabu na elimu ambazo walikuwa wanadai kwa miaka mitano iliyopita.
“Rais pamoja na Waziri Mkuu wa Ethiopia, Meles Zenawi, wamejenga msingi madhubuti kwa makao makuu mapya ya AU,” alisema. Alisema AU chini ya Rais Kikwete imeonyesha uongozi madhubuti na mwisho mzuri wa madaraka kwa kile alichokieleza kuzisimamisha uanachama Mauritania na Guinea zilizojihusisha na mapinduzi Agosti na Desemba mwaka jana.
“Kwa kipindi chote hicho cha mwaka mmoja, aliongoza mikutano minne iliyolenga kukuza ushirikiano baina ya Afrika na washirika wa maendeleo,” alisema Membe. Hata hivyo, Membe alisema kuna masuala ambayo hayajapatiwa ufumbuzi na yanahitaji kuendelea kufanyiwa kazi kwa bidii, ikiwamo mgogoro wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Somalia na Darfur.
Kwa mujibu wa Katiba ya AU, kipindi cha mwaka mmoja cha nchi kushikilia Uenyekiti wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi husika anakuwa Mwenyekiti wa Baraza la Watendaji la Umoja huo. Wakati mkutano huo unafunguliwa rasmi leo, Rais Kikwete amesifu maendeleo chanya yaliyopatikana katika kushughulikia Mgogoro wa Mashariki mwa DRC.
Akizungumza katika mkutano wa kimataifa wa wakuu wa nchi za Maziwa Makuu (ICGLR), Rais Kikwete aliwashukuru kwa michango yao marais wa zamani Olusegun Obasanjo wa Nigeria na Benjamin Mkapa wa Tanzania kwa michango yao katika jumuiya za kimataifa na Umoja wa Mataifa. Alisema inatia matumaini kwamba tangu mkutano kama huo ufanyike Kenya Novemba mwaka jana, mwonekano mpya wa mabadiliko ya ajabu yametokea mashariki ya DRC.
Kikwete alizishauri nchi wanachama kwa pamoja kuunda chombo cha pamoja cha amani na ulinzi chini ya nchi za Maziwa Makuu na kueleza kuwa operesheni ya pamoja itasaidia kufikia malengo katika nchi hizo mbili. Rais Kikwete ambaye leo anamaliza uongozi wake wa uenyekiti wa AU, pia alichukua nafasi hiyo kuwashukuru viongozi wa nchi za Maziwa Makuu (ICGLR) kwa ushirikiano waliouonyesha katika kipindi cha uongozi wake.
0 comments